Wednesday, January 27, 2010

Wanajeshi waliomuua Fundikira wafikishwa Mahakamani!




Watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya mtoto wa Chifu Abdallah Fundikira, marehemu, Swetu Fundikira, MTM 1900 Sajenti Roda Robert(42) wa kikosi cha JKT-Mbweni na MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa JWTZ-Kunduchi wakiwa katika chumba cha Mahakama leo


Washtakiwa wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Geni Vitus Dudu na mashtaka yameendeshwa na wakili wa serikali Monica Mbogo aliyekuwa akisaidiwa na Beatrice Mpangala

Mh. Dudu aliwaeleza washitakiwa hao kwamba kwa mujibu wa kosa linalowakabili hawatakiwi kujibu chochote na kwamba kosa hilo halina dhamana kwa sababu hiyo mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu na kuairisha kesi hiyo Februali 10 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa. Akaamuru washitakiwa wote wamepelekwe rumande.

Ndugu wa marehemu Swetu walikuwepo mahakamani na kusikiliza kesi kwa utulivu, huku wakisema wana imani kwamba haki itatendeka.


Swetu Fundikira alifariki dunia Jumapili asubuhi katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambakoo alilazwa toja Ijumaa usiku baada ya kupigwa sana na wanajeshi watatu, wawili wakituhumiwa kuwa ni hao pichani na mwingine wa tatu haijulikani alipo na msako unaendelea.

Marehemu Swetu alizikwa jana kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar. Kifo chake kimezua zogo kubwa miongoni mwa wananchi ambao wanadai uongozi wa majeshi yote ya ulinzi na usalama uwe wakali kuhakikisha askari wachache wenye mtindo wa nidhamu hawapewi nafasi ya kuchafua majina mazuri waliyo nayo pamoja na ushirikiano mwema kati yao na jamii.

Rafiki asimulia kipigo hadi kifo cha Fundikira kutoka kwa JWTZ



Marehemu Swetu akiwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) Muhimbili muda mfupi kabla ya kukata roho kama zilizvyonaswa na shushushu wa Uwazi
ASKARI wawili wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), wanaodaiwa kumuua mbunge wa zamani, Chifu Abdallah Fundikira, Swetu Fundikira(45), wanatarajiwa kupandishwa kizimbani leo.

Askari hao, ambao ni mtu na mke wake kutoka kambi ya Lugalo, wanadaiwa kumuua kijana huyo, Swetu Fundikira baada ya kumpiga wakiwa na mwanajeshi mwingine mmoja katika ugomvi wa barabarani uliotokana na askari hao kudai kuwa walifanyiwa fujo na kutukanwa na mareheremu Swetu.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, askari hao, Sajenti Rhoda Robert, ambaye ni askari wa Jeshi la Wananchi kutoka Lugalo, na Koplo Ali Ngumbe ambaye ni mume wa Sajent Rhoda, wanatarajiwa kupandishwa kizimbani leo baada ya taratibu za kuwapandisha kizimbani jana kutokukamilika.

"Watuhumiwa hao walipaswa kupandishwa kizimbani jana, lakini hawakuweza kupandishwa kwa sababu taratibu hazikukamilika ikiwa ni pamoja na maandalizi ya hati ya mashtaka.

"Kwa hiyo, kesho ni lazima watapandishwa kizimbani, ingawa sina uhakika zaidi watashtakiwa katika mahakama gani, lakini ni kati ya Kinondoni na Kisutu. Uwezekano mkubwa ni katika Mahakama ya Wilaya ya Kinodnoni kwa sababau ndiko tukio lilikofanyika," kilisema chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya jeshi la Polisi.

Swetu alifariki dunia Jumapili usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na kipigo cha wanajeshi hao, na watuhumiwa hao walitiwa mbaroni na askari polisi wa kituo cha Salender Bridge, na kupelekwa katika kituo cha polisi Oysterbay.

Habari kutoka kwa watu walioshuhudia tukio hilo, zilisema kuwa askari hao walimpiga kijana huyo juzi katika eneo la Kinondoni A kwa kwa Manyanya madai kuwa aliwachomekea gari lake, na kwamba baada ya kumpiga walimchukua na kumuingiza ndani ya gari lao na kuondoka nalo ambapo waliendelea kumpiga huko njiani.

"Tulidhani wanampeleka hospitalini kumbe walipofika karibu na Hospitali ya Muhimbili walimshusha na kuendelea kumpiga na raia mwema alipowaona alitoa taarifa katika kituo cha Salender Bridge. Askari polisi walifika eneo la tukio na kuwakuta wakiendelea kumpiga ndipo wakawatia mbaroni wanajeshi hao," alisema shuhuda huyo.

Kamanda wa polisi Kinondoni, Elias Kalinga alisema mbali na watuhumiwa hao, , mwanajeshi mwingine aliyefahamika kama Private Mohamed Ngumbe, ambaye pia alikuwa kwenye gari moja na watuhumiwa hao, hajakamatwa na bado anasakwa.

"Askari hao walimpigia honi marehemu wakitaka awapishe, lakini akakataa ndipo walipompiga baada ya kukataa kuwapisha," alisema Kamanda Kalinga.

Friday, January 15, 2010

Kampeni ya kuzuia Malaria

Serikali imeanzisha kampeni ya kupambana na ugonjwa wa malaria inayojulikana kama "Zinduka Malaria haikubaliki" ambayo itazinduliwa na Rais Jakaya Kikwete Februari 13, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kampeni hiyo ilianzishwa jana jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi.

Kadhalika, Profesa Mwakyusa, amesisitiza kuwa serikali itatumia dawa ya DDT pamoja na njia nyingine ili kutokomeza ugonjwa wa malaria hapa nchini.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam na kusema serikali pia itatumia nyenzo zilizopo kwa kushirikiana na wananchi ili kupunguza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2013.

Aliongeza kuwa lengo la serikali ni kupunguza malaria kwa asilimia 80 kufikia mwaka 2013 na kwamba hatua nyingine itakayosaidia zoezi hilo ni pamoja na serikali kuanza kutumia kifaa kipya cha utambuzi wa vimelea vya ugonjwa huo.

Profesa Mwakyusa alisema serikali imeweka mikakati ya kutokomeza ugonjwa huo ikiwemo kuanza kugawa vyandarua viwili kwa kila kaya ifikapo Aprili, mwaka huu na kuhamasisha mama wajawazito kuvitumia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, alisema vita vya kupambana na malaria si ya mtu mmoja au serikali pekee bali ni ya jamii nzima.

Alisema ili kuweza kupiga vita ugonjwa huo, ni lazima watu wajue madhara yake katika jamii.

"Mtu akifahamu kwanini anakwenda vitani kupigana ndiyo ataweza kupigana vizuri zaidi," alisema.

Alisema Balozi wa zamani wa Marekani hapa nchini, Mark Green, ambaye anaongoza kampeni ya kupambana na ugonjwa huo katika nchi za Afrika, ndiye aliyemuomba kusaidia katika kampeni hiyo.

Aliongeza kuwa mfanyabiashara akichuma na kupata faida anatakiwa kurudisha sehemu ya faida aliyopata kwa jamii ambayo imemwezesha.

Alisema wafanyabiashara wanatumia watu kuzalisha mali na kwamba wazalishaji hao wanapougua tija inapungua na kwamba mtu yeyote anayetaka kupata faidi lazima ahakikishe wafanyakazi wake wana afya nzuri.

Mengi alisema Watanzania wengi wamejiajiri wenyewe na kwamba wanapougua malaria kipato chao hushuka hivyo kuwafanya wafanyabiashara kushindwa kuuza bidhaa zao kwa watu wasiokuwa na kipato.

Aidha, Mengi alisema umaskini unaongezeka kwa mtu anayeugua malaria na kwamba wananchi lazima wawaonee huruma wenzao wanapopatwa na tatizo hilo.

Aliipongeza serikali kwa kuonyesha njia madhubuti ya kutokomeza ugonjwa huo hapa nchini.

Naye Balozi wa zamani wa Marekani hapa nchini, Mark Green, aliwataka wananchi kushirikiana kwa pamoja katika kutokomeza ugonjwa huo ikiwemo kujikinga wasiupate.

Kobe wa ajabu-Umri zaidi ya Binadamu!


Kobe mkubwa anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka zaidi ya 120, (pichani), bado anaendelea kuishi kwenye shamba la kahawa la Kibo na Kikafu, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Kobe huyo anadaiwa kuwa na nguvu kubwa kiasi cha kuweza kuangusha hata baadhi ya vitu likiwemo gari.

Inadaiwa kwamba kobe huyo amekuwepo katika shamba hilo tangu enzi za ukoloni kabla ya Tanzania haijapata uhuru.

Meneja wa shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 2,054, Jackson Matenge, alisema kobe huyo anajulikana kwa jina la Tony na kwamba hivi karibuni alionyesha uwezo wake baada ya kulipindua lori la tani saba na kusababisha ajali.

Alisema kobe huyo alikuwa amelala barabarani ambapo lori hilo liliegeshwa mahali alipokuwepo na aliponyanyuka, alilipindua lori hilo lakini hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa.

Naye Mwenyekiti wa Vyama vya Msingi vya Masama Saawe, Modio na Masama, Roo na Sonu Ngira, Hatibu Mwanga, alisema mwaka 1952 akiwa na umri wa

miaka minne, walikuwa wakicheza na kobe huyo akiwa mkubwa kama alivyo na kwamba hadi sasa ana miaka 58 lakini bado ana nguvu.

Alisema wakoloni waliokuwa wanamiliki shamba hilo kabla ya serikali kuyataifisha mwaka 1975, ndio waliomuweka shambani humo ambapo baada ya kuondoka walirudi na kutaka kumnunua kwa zaidi yaSh. milioni 100 lakini wanachama walikataa na kudai kuwa hiyo ni sawa na hirizi ya shamba hilo.

Alisema wazungu hao walirudi tena na kuomba kuuziwa kobe huyo lakini bado walikataliwa na kwamba idadi kubwa ya wazungu hufika katika shamba hilo kwa ajili ya kumuona kobe huyo na kupiga naye picha.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Norman Sigalla aliutaka uongozi wa shamba hilo kumjengea mazingira mazuri ya kuishi kobe huyo ili aweze kutumika kama sehemu ya utalii kwa watalii wa ndani na nje.