WACHIMBAJI, Salim Swalehe (48) na Adamu Mussa (34) ni miongoni mwa wachimbaji zaidi ya 30 walinusurika kufa kwa maporomoko ya maji na tope kwenye migodi ya machimbo ya Tanzanite Mererani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, ijumaa iliyopita.
Wachimbaji hao, ambo hadi sasa hawaamini kama kweli walipambana na kunusurika kifo, kwa nyakati tofauti, wanaelezea jinsi walivyohangaika kwa kutumia kila mbinu kujiokoa kwa zaidi ya saa 12 katika mgodi walimokuwamo wakati maji yakijaa na kuangukiwa na mawe na tope zito.
Swalehe ambaye aliokoka wakati wenzake sita wamefariki katika mgodi unaomilikiwa na mchimbaji Benjamin Mwanga, amesema alikwisha kukata tamaa kuendelea kuishi duniani wakati akijitahidi kujiokoa.
Anasimulia kuwa, alijificha pangoni ambako maji yalimfuata na kumzidi nguvu hadi akalazimika kunywa mengi.
Swalehe ambaye alijiokoa baada ya kuhangaika kutoka chini ya mgodi huo kuanzia majira ya saa 2:00 usiku hadi saa mbili asubuhi Jumamosi, anasema hakutegemea kuokoka katika kifo kwani aliwashuhudia wenzake watatu wakifa baada ya kunywa maji mengi na kuishiwa pumzi.
" Mimi ni Mungu tu kanisaidia, kwanza wakati maji yamekuwa mengi mchimbaji mwenzangu, Fadhili Juma alipanda juu kidogo ndani ya mgodi kutazama na ghafla tulimuona akiwa amerudi huku damu zikimvuja na mawe makubwa yakimfuta na hapo tulijua tayari kifo kimetufika na ndipo tulianza kuhangaika, " anasema Swalehe.
Anaongeza kuwa, alijitahidi kujivuta kwa tumbo mithili ya nyoka kwa kupitia njia za mitobozano, lakini alikutana vipingamizi vya maji kisha, kujificha katika moja ya maeneo ya kupumzikia chini ya mgodi.
Mchimbaji huyo, anasema akiwa katika eneo hilo, kila muda ulivyosonga mbele, maji yalikuwa yakijaa kidogo kidogo na yalipofika mdomoni, alijua tayari amekufa kwa sababu alianza kuyanywa.
Anasema baada ya kunywa maji, ghafla aliona yakianza kupungua hadi chini ya kidevu chake, baadaye tumboni hatua ambayo kidogo ilimrejeshea matumaini kwa kuwa alikuwa akipata pumzi nyingi.
Anaongeza kusema kuwa, baada ya kupata matumani , alianza tena jitihada zake za kutaka kujiokoa , wakati huo, ilikuwa ni majira ya saa tisa usiku na alitembea kwa umbali mrefu kwa kuburuza tumbo huku akikutana na miili ya wenzie ambao walikuwa tayari wamefariki.
"Mimi kwa kuwa ni mzoefu kidogo, nilianza kuwaza mitobozano zaidi kwani baada ya kuona maji yamepungua nilijua nikiendelea kukaa hapo hapo sintaweza kutoka na nitakufa tu, " anasema Swalehe.
Anasema baada ya kutembea kwa muda, aliona njia ya kutokea ikiwa na matope na kuanza kuipita huku akipishana na matope yaliyokuwa yanaporomoka kwenda chini hadi alipofika juu, majira ya saa 3:00 asubuhi.
" Nashukuru Mungu nimefika duniani siamini kama kweli nimeokoka na kifo, " anasisitiza.
Katika mgodi huo alipookoka Swalehe, wenzake zaidi ya sita walifariki dunia akiwamo mtoto wa mmiliki wa mgodi huo, Kelvin Mwanga ambaye alikuwa ni mwanafunzi nchini Uganda.
Mchimbaji mwingine, Adam Mussa ambaye alikuwa anachimba katika mgodi unaomilikiwa na Elisante Stanley ambako wachimbaji wanane wamekufa anasema, bila jitihada zake, mgodi huo ungeua watu 16 kwani yeye binafsi aliokoa vijana watano.
"Tulikuwa wote chini na wenzangu wakati tunachimba ghafla mpira wa kuleta hewa mgodini ulipasuka, hivyo mimi nikapanda juu na kuwaacha wenzangu chini nikiwa na vijana watano ambao sio wazoefu kabisa, "anasema Mussa.
Anasema ghafla aliona maji mengi yakitoka juu ya mgodi kwenda chini mithili ya mto na ndipo aliwambia wenzake wakae pembeni.
Mussa anaongeza kuwa, wakati wako hapo maji yaliongezeka zaidi na bila wenzake wanane waliokuwa chini zaidi kutoka na hapo aliamini tayari kifo kimewafika.
"Niliwambia hawa vijana tulieni tujiokoe la sivyo leo tunakufa wote.... walianza kulia lakini nikawambia nyamazeni nikachukua pipe (bomba) ya hewa tukaikunja na kuelekeza maji chini kutoka pale tulipokuwa kweli iliwezekana," anasema Mussa.
Hata hivyo, anasema licha ya kuanza kupunguza maji lakini mengine yaliyokuwa juu yaliendelea kushuka chini na hapo aliwamtuma moja ya vijana kutafuta mpira mwingine ili wapunguze maji.
Anasema baada ya mwenzao kurudi alianza tena kupunguza maji kuelezea chini kabisa ya mgodi lakini haukusaidia ndipo aliwambia wenzake waondoke katika eneo hilo ambalo hutumika kama sehemu ya kupumzika chini.
" Nilianza na sisi kutafuta sehemu ya kutoka huku maji na mawe kama maporokomo yakitupiga vichani lakini tulioendelea kupanda juu mimi nilikuwa nyuma ya wenzagu nikiwaelezeka, " anasema Mussa.
Anaendelea kusimulia kuwa, kuanzia majira ya saa tatu usiku hadi saa 10:00 usiku, walikuwa wakihangaika kwenda kila sehemu ambako kuna mtobozano, wakijitahidi kupita bila mafanikio.
" Mimi nilikumbuka kuna mtobozano mwingine na nikawambia wenzangu wanifuate na nilipofika tulimkuta mwenzeru mmoja akiwa hapo akijitahidi kupita lakini alikuwa tayari amefariki, " anasema Mussa.
Anasema nao walianza kumwondoa ili wapite bila ya mafanikio kwani alikuwa amenasa katikati ya mlango wa kupitia kutokana na jiwe kubwa kumzidi.
Anasema baada ya kuhangaika kwa muda ndipo walipata njia nyingine ambayo ilikuwa na maji kiasi na kufanikiwa kutoka.
" Tunamshukuru Mungu kwani ndiye ametuokoa wenzetu wanane wamefariki, " anasema Adam.
Hadi jana katika mgodi huo, wa Elisante walikuwa wametoa chini miiili mitatu ya wachimbaji waliokufa, ukiwemo wa Kulwa Petro ambao ndio ulikuwa umeziba njia ya kutokea.
Hata hivyo, wachimbaji wote waliokoka, wamesisitiza wataendelea na kazi hiyo kwa madai bado wanatafuta maisha na hawana kazi nyingine zaidi ya kuchimba madini.
"Brother hii ndio kazi yetu siwezi kusema leo ndio mwisho wangu kuchimba baada ya kutoka nikiwa hai au nitaendelea, " anasema Mussa.
Wachimbaji wadogo zaidi ya 64 wanahofiwa kufa maji, baada ya kukumbwa na mafuriko kwenye migodi walimokuwa wakichimba madini.
Maji hayo yaliingia kupitia migodi ya De Souza ambayo haitumiki ikiwa na kina kirefu.
Migodi hiyo ambayo ndiyo ilisababisha maafa ya mwaka 1998 wakati wa mvua za El Nino, maji yaliingia tena baada ya kuvunja korongo lililotengenezwa kienyeji mwaka 1998 kutokana na agizo la serikali kutaka lifunikwe pamoja na migodi hiyo.
Tukio hilo lilitokea Machi 14, mwaka 1998 , pamoja na kuua wachimbaji zaidi ya 100, swali lake bado halijajibiwa hadi maafa mengine yanatokea mwaka huu, waliopewa fedha za kufukia migodi ya De Souza hawakufanya hivyo.
Vilevile wengi wanajiuliza kuwa, kwanini haukutengenezwa mrefeji wa kitaalam kuzuia maji kuingia tena katika migodi hiyo ya disusa na kuifikia mingine.
No comments:
Post a Comment