Wednesday, July 2, 2008

Mshindi wa Faidika na BBC huyu hapa


burundi yafaidika na BBC
Mshindi Ashura Kisesa kutoka Burundi alipokabidhiwa tuzo na waziri mkuu wa Uganda Profesa Apolo Nsibambi, huku mkuu wa kitengo cha Afrika na Mashariki ya Kati wa BBC, Jerry Timmins (shoto) akishuhudia.

Ashura Kisesa, raia wa Burundi, mwenye umri wa miaka 24, ameshinda zawadi ya juu ya shindano lililoendeshwa na BBC Idhaa ya Kiswahili, la kutafuta kijana mwenye kipaji cha biashara, lijulikanalo kama Faidika na BBC.
Waziri mkuu wa Uganda, Apolo Nsibambi alimkabidhi Bi Ashura tuzo maalum pamoja na hundi yenye thamani ya dola elfu tano za Marekani, ili aweze kuanzisha mradi wake wa kujenga vyoo vya kulipia, katika miji ya Afrika Mashariki na Kati.

Ashura Kisesa, msichana pekee aliyeingia kwenye fainali hizo, zilizorushwa moja kwa moja, kupitia BBC Idhaa ya Kiswahili na Televisheni ya UBC, aliwashinda vijana wengine wanne, kwa kuwashawishi majaji na jinsi atakavyotumia fedha za zawadi kuanzisha mradi wenye mafanikio na kunufaisha jamii inayomzunguka.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Uganda, Profesa Apolo Nsibambi alisema “ Wakati shindano hili likianzishwa mwaka jana, hawakuwepo wasichana katika fainali, hivyo natoa pongezi kwa Ashura.

"Natoa wito kwa BBC kuchukua hatua ithibati kuhimiza wanawake zaidi kuingia katika biashara. Hii ni jitihada nzuri ya BBC ya kusaidia vijana kuwa wabunifu na kuwafanya wawe waundaji wa nafasi za kazi, badala ya kuwa watafutaji kazi," alisema.
Ashura aliwasilisha wazo lake, mbele ya jopo la majaji, katika matangazo yaliyorushwa moja kwa moja. Majaji hao walivutiwa na jinsi Ashura alivyowasilisha mchanganuo wake, na jinsi alivyopangilia.
Mara baada ya kushinda Ashura alisema “ Nimefurahi mno kushinda. Ukosefu wa vyoo katika miji ya Afrika Mashariki na Kati, ni tatizo kubwa, na ni imani yangu kuwa nitaweza kuleta mabadiliko kupitia wazo hili la biashara”.

Naye Meneja mradi wa Faidika na BBC, Salim Kikeke alisema “ Hakika Ashura anastahili ushindi. Wazo lake la kibiashara ni zuri, na litawanufaisha watu wengi wa Afrika Mashariki na Kati. Namtakia kila la kheri, na nina hakika, huu ni mwanzo tu wa maisha bora kwake”

Wengine waliongia katika fainali hiyo ya Faidika na BBC ni Witness Omoga (22) kutoka Kenya, Rangira Aime Frederick (17) kutoka Rwanda, Apolinary Joseph Laksh (23) kutoka Tanzania, na Derrick Kajukano kutoka Uganda.

Vijana hao watakuwa na nafasi ya kupata ushauri kutoka BBC watakapotaka kuanzisha biashara zao. Jopo la majaji liliundwa na Farijala Baraza Sadi kutoka Burundi, Mutagoma Madina kutoka Rwanda, Arnold Kweka kutoka Tanzania, John Ndungu kutoka Kenya na Jasmine Nakayima Adam kutoka Uganda.
Mbali na matangazo hayo ya moja kwa moja kurushwa kupitia shirika la utangazaji la Uganda UBC, tuzo za washindi zilichongwa na msanii kutoka Uganda, Peter Oloya, huku burudani ya muziki ikiporomoshwa na mwimbaji, mshindi wa tuzo kadhaa, Maurice Kirya pia wa Uganda.

Unaweza kuona na kusikika matangazo hayo tena, kupitia bbcswahili.com/faidika.

Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na.
Christine George,
Assistant Publicist,
BBC World Service
+44(0) 207557 1142
christine.george@bbc.co.uk

No comments: