Tuesday, February 10, 2009

Zombe na wenzake 9 bado kazi ipo!

HATMA ya Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na wenzake 12 itajulikana leo, wakati Jaji Salum Massati atakapotoa uamuzi wake kama washitakiwa hao wana kesi ya kujibu au la. Jaji atatoa uamuzi huo baada ya mawakili wa pande zote mbili kumaliza kutoa maelezo yao ya utetezi kuhusu kesi hiyo.

Washitakiwa ambao mahakama itaona wana kesi ya kujibu watalazimika kusimama kizimbani kujitetea ili kuepuka adhabu ya kifo. Kosa la mauaji kisheria adhabu yake ni kifo, hivyo uamuzi wa Jaji Massati atakaotoa leo ndiyo utakaoonyesha ni washitakiwa wapi wanatakiwa wajitetee na ni wapi watarudi kwao kwa furaha.

Mahakama inaweza kuwaachia washitakiwa wote kama itaona hakuna ushahidi mzito unaowafanya wajitetee au inaweza kuwaachia baadhi ya washitakiwa na wengine kulazimika kujitetea kwa kadri itakavyoona uzito wa ushahidi. Lakini pia mahakama hiyo inaweza kuamuru washitakiwa wote kuwa wana kesi ya kujibu, hali itakayowalazimu mmoja baada ya mwingine kutoa utetezi wake mwenyewe na ikilazimika kuita mashahidi ambao ni katika jitihada za kusaidia kumwepusha na adhabu ya kitanzi.

Wiki iliyopita, mawakili wa pande zote walijenga hoja kuishawishi mahakama kukubaliana na maoni yao, baada ya upande wa mashitaka kumaliza kutoa ushahidi wao. Wakati upande wa mashitaka unasisitiza kuwa Zombe na wenzake wana kesi ya kujibu, upande wa utetezi unadai hakuna ushahidi mzito unaowafanya washitakiwa hao wasimame kizimbani kujitetea.

Zombe na wenzake wanashitakiwa kwa mauaji ya Wafanyabiashara wanne ambao ni Ephrahim Chigumbi, Sabinus Chigumbi ‘Jongo’, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, ambaye alikuwa dereva wa teksi iliyokuwa ikitumiwa na wafanyabiashara hao katika shughuli zao. Washitakiwa wengine katika kesi hiyo namba 26/2006 ni Mrakibu wa Polisi Christopher Bageni, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Ahmed Makele, F. 5912 Konstebo Noel Leonard, WP. 4593 Konstebo Jane Andrew, D. 6440 Koplo Nyangelera Moris na D. 1406 Koplo Emmanuel Mabula.

Wengine ni E. 6712 Koplo Felic Sandsy Cedrick, D. 8289 Konstebo Michael Shonza, D. 2300 Koplo Abeneth Saro, D 9321 D/C. Rashid Lema, D. 4656 D/Koplo Rajab Bakari na D. 1367 D/Koplo Festus Gwabisabi. Wanadaiwa kutenda kosa hilo Januari 14, 2006 katika msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Washitakiwa walikana mashitaka hayo na wameendelea kuwa rumande tangu kesi hiyo ifikishwe mahakamani kwa mara ya kwanza Juni, 2006.

Inadaiwa kuwa siku wanayotuhumiwa kufanya mauaji hayo, washitakiwa waliwakamata wafanyabiashara hao na dereva bila vikwazo vyovyote katika maeneo ya Sinza Palestina. Kwa mujibu wa upande wa mashitaka, askari hao walidai kuwa marehemu hao walikuwa majambazi, wakati haikuwa kweli. Upande wa mashitaka unadai watu hao walikuja jijini kutafuta soko la madini waliyokuwa nayo.

Wakati wanakamatwa, wafanyabiashara hao walikuwa na kiwango kikubwa cha madini na fedha nyingi baada ya kuuza baadhi ya madini kwa mfanyabiashara mwingine Arusha ambako walikwenda kupeleka watoto wao shuleni. Inadaiwa kuwa washitakiwa wote kwa pamoja, walipanga mauaji hayo na baadaye kuhusisha tukio hilo na matukio mengine ya wizi wa kutumia silaha kwenye Kampuni ya Bidco na Al-Mar Jewellers Kariakoo ili kujaribu kujipatia madini na fedha za wafanyabiashara hao.

Upande wa mashitaka unadai pia kuwa askari walitekeleza mauaji hayo kwa kupokea amri kutoka kwa Zombe kwa usimamizi wa karibu wa Bageni na Makele. Inadaiwa pia kuwa washitakiwa (isipokuwa Zombe) waliwachukua marehemu hao hadi kwenye msitu wa Pande na kuwapiga risasi huku wakiwa wamewalaza kifudifudi. Baada ya mauaji hayo, washitakiwa wanadaiwa kukutana katika Kituo cha Polisi cha Urafiki ambapo waligawana pesa na vitu vingine wanavyodaiwa kuchukua kutoka kwa wafanyabiashara waliouawa.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Mei 27 mwaka jana na upande wa mashitaka katika kuthibitisha makosa ya mauaji yanayowakabili washitakiwa hao ulipeleka mashahidi 37. Ushahidi wao ndiyo unaufanya upande wa mashitaka kuishawishi mahakama ione kuwa washitakiwa wote wana kesi ya kujibu kwa vile ndiyo walioshiriki kuwakamata washitakiwa na baadaye wakapatikana wameuawa.

Suala la marehemu kuuawa kwa risasi halina ubishi, ila swali la msingi ambalo mahakama inalazimika kujiuliza kabla ya kutoa uamuzi wake ni kama washitakiwa ndiyo walioshiriki kuwaua marehemu hao. Jambo lingine la kujiuliza katika kesi hiyo ni kama mauaji hayo yalifanywa wakati washitakiwa wote wakiwa na nia moja ovu ya kuua au walifanya hivyo kwa bahati mbaya. Katika kujenga kesi yao, upande wa mashitaka unadai ushahidi kadhaa unaonyesha kuwa washitakiwa ndiyo walioshiriki kuwaua wafanyabiashara hao kwani waliwakamata bila mapigano yoyote Sinza.

Upande wa mashitaka unadai kuwa washitakiwa walikuwa na nia ovu ya kuwaua washitakiwa hao kwani baada ya kutimiza kitendo hicho, waligawana fedha ambazo walikutwa nazo marehemu hao. Lakini upande wa utetezi unadai hakuna shahidi aliyeshuhudia kama washitakiwa ndiyo waliofyatua risasi kuwaua marehemu, ila ushahidi wote ni wa kimazingira na wa kusikia.

Zombe anakingiwa kifua na wakili wake kuwa hajawahi kuwaona marehemu kabla ya kuuawa na hata baada ya kuuawa hakuona miili yao. Wakili huyo pia anadai kuwa hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa Zombe ndiye aliyeamuru watu hao kuuawa kwa risasi. Umma wa Watanzania una hamu ya kutaka kufahamu kile ambacho kitaamriwa na Mahakama Kuu ya Tanzania leo.

No comments: