Tuesday, June 2, 2009

faidika na BBC 2009 inapatikana hapa

London, Juni 01 2009. BBC Idhaa ya Kiswahili imezindua shindano la tatu la kutafuta kijana mjasiriamali, ambaye ataleta mabadiliko katika jamii.


Taarifa hiyo imetolewa leo katika Dira ya Dunia, kipindi cha jioni cha BBC Idhaa ya Kiswahili. Shindano la Faidika na BBC linawaalika vijana wenye mawazo ya kibiashara na wanaozungumza Kiswahili,wenye umri wa miaka kati ya 16 hadi 24, kuwasilisha michanganuo yao ya kuanzisha biashara ambayo italeta mabadiliko katika jamii. Michanganuo hiyo ilenge kuanzisha biashara kwa mtaji wa dola elfu tano za Marekani.


Mwaka huu, kutakuwa na shindano la kitaifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baada ya vijana wa huko kuomba kushirikishwa kikamilifu. Hali kadhalika, mashindano ya kitaifa ya nchi za Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda na Tanzania, yatakuwepo.


Kila mshindi wa kitaifa atatunukiwa tuzo maalum pamoja na cheti.Katika fainali, ambayo mwaka huu itafanyika mjini Mombasa, nchini Kenya, washindi sita kutoka mataifa hayo sita, watapambana kutafuta mshindi.


Mshindi wa kwanza mbali na kupatiwa kitita cha dola elfu tano kuanzisha mradi wake, pia atazawadiwa tuzo maalum ya Faidika na BBC.Mchanganuo hautakiwi kuzidi maneno elfu moja na mia tano (1,500).


*Burundi
Faidika na BBC 2009,
Building Maison de la Bible,
Avenue de la Mission,
2eme etage,
en face de PAR,
Bujumbura
BP 6790DR


*Congo
Faidika na BBC 2009,
Radio Maendeleo,
PO Box 3133,
Bukavu


*Kenya
Faidika na BBC 2009,
5th Floor,
Longonot Place,
Kijabe Street,
PO Box 58621,
Nairobi


*Rwanda
Faidika na BBC 2009,
PO Box 2790,
Kigali


*Tanzania
Faidika na BBC 2009,
PPF Building, 8th Floor,
Sokoine Drive and Morogoro Road,
PO Box 79545,
Dar es Salaam




*Uganda
Faidika na BBC 2009,
1A,
Ruth Towers,
Plot 15A,
Clement Hill Road,
PO Box 7620,
Kampala

Solomon Mugera, Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC amesema "Faidika na BBC ni zaidi ya msaada wa kifedha kwa mshindi. Wazo kuu la Faidika ni kuwa vijana hawana ulazima wakwenda mbali ili kupata mafanikio, na kuwa wazo zuri tu la ubunifu linaweza kubadili maisha yao, na ya jamii inayowazunguka.


Katika Idhaa ya Kiswahili ya BBC, tuko makini kuelimisha wasikilizaji wetu kuhusu masuala ya kifedha na biashara, na hivi karibuni tutaanzisha kipindi maalum cha biashara ambacho kitatoa maelekezo na ushauri wa kibiashara ambao utasaidia vijana na wafanyabiashara wanaochipukia."


Naye meneja wa mradi wa Faidika na BBC, Salim Kikeke, amesema: " Vijana wana mawazo mengi ya ubunifu. Michanganuo tuliyopata mwaka jana ilikuwa ya kusisimua mno. Bila shaka mwaka huu pia tutaona wazo bora ambalo litawashangaza hata majaji."


Mshindi wa mwaka jana, Ashura Kisesa kutoka Burundi, alitoa wazo la kujenga vyoo vya kulipia katika miji ya Afrika Mashariki na kati. Kusoma zaidi kuhusu Ashura Kisesa na kufahamu zaidi kuhusu shindano la Faidika na BBC ingia kwenye mtandao katika
bbcswahili.com/faidika.Mwisho //


Kwa wahariri:Taarifa hii kwa vyombo vya habari pia inapatikana kwa lugha ya kiingereza. Solomon Mugera na Salim Kikeke wanapatikana kwa ajili ya mahojiano.


BBC Idhaa ya Kiswahili ni Shirika la Utangazaji ambalo hutoa huduma zake kupitia radio na kwenye mtandao kwa wasikilizaji wanaozungumza Kiswahili barani Afrika na ulimwengu mzima kwa ujumla.


BBC Idhaa ya Kiswahili inapatikana kupitia vipimo vya FM na pia kupitia radio washirika nchini Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Kenya, Malawi, Rwanda, Tanzania na Uganda. Vipindi vya BBC Idhaa ya Kiswahili pia vinasikika kupitia mtandao katika bbcswahili.com, ambapo pia unapata habari za kila saa, makala na uchambuzi kuhusu Afrika Mashariki na dunia nzima vilevile.


BBC World Service - Idhaa ya Dunia, ni shirika la habari la kimataifa la utangazaji linalotoa huduma za matangazo kwa lugha 32 mbalimbali. Shirika hili linatumia njia kadhaa kuwafikia wasikilizaji wake milioni 182 ulimwenguni kote, kwa kupitia Masafa mafupi, masafa ya kati, FM, satellite na viunganishi.


Vituo washirika vya radio vipatavyo 2,000 hupitisha matangazo ya BBC, huku vituo kadhaa vukirusha taarifa zake kupitia simu za mkononi na vifaa mbalimbali visivyotumia nyaya.


Wavuti wa BBC unatoa habari mbalimbali kwa maandishi, sauti na video, na vilevile kutoa nafasi kwa wasikilizaji kushiriki moja kwa moja katika vipindi kufuatana na matukio ya duniani. Kwa taarifa zaidi tembelea bbcworldservice.com.

No comments: