Tuesday, July 20, 2010

Sababu za kuuawa Prof. Jwani Mwaikusa, hizi hapa (labda)



WAKATI maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam walijitokeza kwa wingi kumzika Mhadhiri Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Jwani Mwaikusa mwishoni mwa wiki iliyopita, wanafamilia na baadhi ya mawakili wamedai kuwa waliofanya mauaji hayo ya kinyama si majambazi na wameyahusisha na kesi za Mauaji ya Kimbari ya Rwanda zinazoendelea mjini Arusha.

Wakizungumza na timu ya Uwazi, wanafamilia hao akiwemo mtoto wa marehemu Baraka Mwaikusa, walisema profesa alikuwa akisumbuliwa sana na kesi za mauaji ya kimbari za Rwanda ambazo alikuwa mmoja wa mawakili wa watuhumiwa.

“Baba hakuwa na deni au hakuwa akidaiwa na mtu na wala hajawahi kumdhulumu mtu, alikuwa mtenda haki. Mara nyingi katika siku hizi za mwisho wa maisha yake alikuwa akizungumzia kesi ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda ambapo kesi moja alishinda na moja alishindwa na alikuwa anapilikapilika za kuikatia rufaa, hili naweza kusema ndilo tatizo pekee ambalo baba alikuwa akihangaika nalo,” alisema Baraka mtoto wa marehemu.
Wanafamilia hao walionesha wasiwasi wao huo kutokana na kile walichodai kuwa, wauaji hao hawakuchukua kitu chochote baada ya kutekeleza mauaji hayo ya kinyama.
Naye wakili maarufu nchini, Mabere Nyaucho Marando alikwenda mbali zaidi alipopasua jipu kwa kudai kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba mauaji hayo yamefanywa na Wanyarwanda kutokana na ushindi wa mambo aliyokuwa akiibua Prof.
Mwaikusa katika Mahakama ya Kimataifa ya Arusha na kufanikiwa kushinda kesi moja.
“Profesa Mwaikusa ni the besti advocate (wakili mahiri) miongoni mwetu, alikuwa makini kuliko mawakili wengi pamoja na mimi na nilithibitisha hilo tuliposhirikiana naye katika kesi ya Jaji Joseph Warioba na Steven Wassira.

“Sasa katika kesi za mauaji ya kimbari ya Rwanda moja ya kitu kikubwa alichokifanya ni kuiomba mahakama ihamie kwenye tukio kitaalamu tunasema to visit the scene of crime (kutembelea sehemu iliyofanyika uhalifu) na ombi hilo likakubaliwa. Nashawishika kuamini kuwa baadhi ya Wanyarwanda wanaweza kuhusika katika suala zima la kumuua Profesa Mwaikusa baada ya kuona hilo,” alisema Marando.

Aliongeza kuwa kwa hulka ya Wanyarwanda ambao kuuana kwao si jambo geni, kuna uwezekano mkubwa kuwa wameingia nchini na kufanya unyama huo kwa msomi ambaye alikuwa tumaini kubwa katika tasnia ya sheria.
“Wanyarwanda wana kawaida ya kuua watu hata walio nje ya nchi yao, hivyo mimi bado nashawishika kuamini kuwa hawa wanahusika na mauaji haya,” alisisitiza Marando.

Mwanasheria huyo ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi haraka na kuwapata waliofanya unyama huo.

Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) miaka 14 iliyopita, Mei 22, 2009 Msajili wa Mahakama hiyo alimteua wakili Prof. Mwaikusa kumtetea mtuhumiwa, Fulgence Kayishema ambaye alikuwa polisi mpelelezi katika mkoa wa Kibuye, magharibi ya Rwanda na tuhuma zake ni pamoja na mauaji ya kimbari, kwa mujibu wa Msemaji wa ICTR, Roland Amoussouga.

Aidha, Prof. Mwaikusa alikuwa pia ni wakili kiongozi katika kesi nyingine kwenye mahakama hiyo, iliyokuwa inamhusu mfanyabiashara wa zamani wa Rwanda, Yusuf Mnyakazi ambaye aliwekwa katika orodha ya watuhumiwa watano wa kupelekwa nchini Rwanda na ombi hilo lilikubaliwa na mahakama hiyo.

Prof. Mwaikusa (58) aliuawa Jumatatu iliyopita nyumbani kwake Tegeta Salasala, jijini Dar es Salaam na watu wasiojulikana-, ambao pia walimuua mpwa wake, Daud Gwamaka (25) na jirani yake John Mtui (45) ambaye mara baada ya kufika nyumbani kwake alitoka na kukutana na wauaji hao waliodhani kuwa ni mmoja wa watu waliotoka katika nyumba ya profesa.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Charles Kenyela amesema kuwa watuhumiwa sita wamekamatwa na jeshi hilo kufuatia taarifa zilizotolewa kwake kupitia utaratibu wa polisi jamii.

“Nathibitisha kuwa hadi sasa tunaendelea vizuri na upelelezi wa mauaji hayo, msako mkali unaendelea katika maeneo mbalimbali ya Kanda Maalum na nahakikisha kuwa tutawatia nguvuni wote waliohusika na tukio hilo,’’ alisema Kamanda Kenyela.
Ameacha mke, Rofea na watoto wanne Baraka (28), Mussa (26), Amu (22) na Msafiri(19).
Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema roho yake, Ameni.

No comments: