Staa wa Bongo Fleva mwenye heshima tele, Rehema Chalamila ‘Ray C’, amefunguka kuwa ndoa aliyopanga kufunga na msanii mwenzake, Waziri Makuto ‘Lord Eyez’, haikuwa mpango wa Mungu.
Akizungumza kwa huzuni iliyoendana na unyenyekevu na presenta wa Clouds FM, Millard Ayo, Ray C alisema hakuna kitu kilichosababisha kumwagana na Mwana-hiphop huyo na zaidi sana ni utoto ndiyo uliosababisha.
“Ni utoto tu ulioambatana na mazoea ndiyo kitu kikubwa kilichotufanya tuachane, hatujawahi kugombana wala kuhisiana jambo baya lolote.
“Ilifika kipindi hata kazi tukawa hatufanyi kwa umakini, tuliweka mbele mapenzi ndipo mimi nilipofikiria na kuona tunapotea, nikamwambia mwenzangu tuvunje uhusiano wa kimapenzi na tuendelee kuwa marafiki wa kawaida.
“Hicho ndicho kilichotokea, Mungu tu hakupanga tufunge ndoa,” alisema Ray C.
Naye Lord Eyez alipovutiwa waya na mtangazaji huyo, alikuwa na haya ya kusema:
“Sijawahi kugombana na Ray C ni uamuzi tu ambao tulikaa na kuafikiana.
“Kuna vitu vilikuwa vinajitokeza na katika kuviwahi, ikabidi tuchukue uamuzi huo, kwa sasa mimi na Ray C ni marafiki tu, tunawasaliana na mmojawapo akihitaji msaada kwa mwenzie, anamjulisha.”
Mwishoni mwa mwaka jana, wawili hao walimwagana rasmi ambapo hivi karibuni Ray C aliripotiwa kufikia uamuzi wa kuokoka.
No comments:
Post a Comment