Na Fidelis Butahe
WALIMU wa Shule ya Msingi Buguruni Kisiwani, Dar es Salaam wamegoma kufundisha wakishinikiza kuachiwa huru kwa mwenzao, Rosemary Haule waliyedai kuwa yuko katika Gereza la Segerea.
Walimu hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini, waliliambia gazeti hili jana kuwa Haule alikamatwa na kuwekwa mahabusu baada ya kumchapa mwanafunzi anayesoma darasa la nne katika shule hiyo.
Wakisimulia mkasa huo walidai kuwa mwanafunzi huyo alichapwa Februari 4, mwaka huu na mzazi wake alifika shuleni hapo na kudai kuwa mwanaye huyo alipata matatizo ya macho baada ya kuchapwa.
“Sisi baada ya tukio lile tulimchukua na kumpeleka Hospitali ya Amana baada ya kutueleza kuwa anaumwa macho, ila cha kushangaza ni kwamba matatizo ya macho alikuwa nayo kabla hata ya kuchapwa,” alisema mmoja wa walimu hao. Licha ya kupatiwa dawa tulimpeleka katika Hospitali ya CCBRT kwa tiba zaidi, alipona na kurejea nyumbani kwao.”
Mwalimu huyo aliendelea kueleza; "cha ajabu Mwalimu Haule alikamatwa na Polisi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Buguruni ambako alifunguliwa mashtaka,"
“Wiki moja na nusu baada ya Hamisi kupona ndipo Polisi walikuja kumkamata Haule, hivi tunavyozungumza jana (juzi), kafikishwa mahakamani na sasa yuko Gereza la Segerea,” alidai mwalimu huyo.
Mwananchi jana lilifika katika shule hiyo na kukuta walimu wakiwa katika kikao huku wanafunzi wakieleza kuwa walikuwa hawajafundishwa tangu asubuhi.
“Tangu asubuhi hakuna mwalimu aliyeingia kufundisha, isipokuwa aliingia mmoja kwa ajili ya kukusanya fedha za mtihani tu. Tunasikia kuwa wamekwenda kumwona mwenzetu aliyechapwa na mwalimu…, aliumia yuko nyumbani,” alisema mwanafunzi mmoja wa darasa la saba shuleni hapo.
Hata hivyo, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Sanga alisema kuwa walimu hawajagoma na wanaendelea na kazi kama kawaida.
“Hapa hakuna aliyegoma, walimu wanaendelea na kazi kama kawaida,“ alisema Sanga.
Juzi, Mwalimu Rosemary alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu shtaka la kujeruhi mwanafunzi wake huyo baada ya kumchapa.
Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Aida Kisumo alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Februari 2, mwaka huu shuleni hapo.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, siku ya tukio saa 7:00 mchana shuleni hapo, mshtakiwa anadaiwa kumpiga mwanafunzi (jina tunalo) viboko na kumkwaruza kwa kucha sehemu mbalimbali za mwili, ikiwamo machoni na kumsababishia majeraha makali.
Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka alikana na Hakimu Tarsila Kisoka aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 22, mwaka huu itakapotajwa tena, mshtakiwa alirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
No comments:
Post a Comment