Kwa nini tunashindwa kuelewa ukweli huo mdogo ambao hata watoto wa shule za msingi wanaufahamu?
Kuna wakati wapenda muziki walikaa na kuamua eti mtindo wa dansi nchini uitwe “Achimenengule”! Kilichofuata ni kwamba uamuzi huo uliishia kwenye meza walizokuwa wamezikalia wakati wa majadiliano hayo.
Hapakuwa na “Achimenengule” wala nini hadi leo!
Mtindo wa mavazi au kitu chochote huwa havipangwi, hujitokeza vyenyewe kwa kukubalika kimyakimya kwa watu – si kwa kutangazwa!
Hivi hatuna kitu cha maana cha kujadili kwa manufaa ya watu wengi? Kwa nini Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni inakubali kujishusha kiasi hicho wakati majuzi tu ilishindwa kuisafirisha timu ya wanawake ya taifa ya soka kwenda Namibia wakati kila mwaka inapewa bajeti nono na bunge?
Iwapo tatizo ni Watanzania kutaka kujulikana nje ya nchi, basi dawa yake ni ndogo sana. Mtanzania anayetaka kujulikana akiwa nje ya nchi hii ni kuvaa nguo yoyote na akaiandika kwa maandishi makubwa sehemu yoyote, kwa mfano: “I am a Tanzanian” (kwa Kiingereza), “Je suis un Tanzanien” (Kifaransa) au “Yo soy on tanzano” (Kihispania).
Yote hayo yanamaanisha kwamba: “Mimi ni Mtanzania”.
Hiyo inatosha kabisa kuwafanya watu wakufahamu kwamba unatoka katika nchi mojawapo za bara maskini la Afrika. Inatosha!
Huna haja ya kuchora picha ya twiga au mlima Kilimanjaro kwani twiga ni wengi sana duniani achilia mbali milima mirefu zaidi ya Kilimanjaro.
Hata hivyo, kwa kifupi kabisa: Watu waliopania kwamba Tanzania lazima iwe na vazi la taifa ambalo litawatambulisha wakiwa ndani na nje ya nchi hii, wasipoteze muda kulitafuta – watumie mavazi ya Kimasai!
Ni mavazi yenye kuvutia na ni ya kipekee ambayo Mtanzania akivaa nje ya nchi hii ni hakika watu watamshangaa na kumfurahia.
Kama vazi hili watu hawalitaki basi ni heri tujadili jinsi ya kuzipatia shule za sekondari za kata kompyuta, tujadili jinsi ya kusomesha na kuwalinda maalbino nchini, tujadili jinsi ya kupunguza bei za betri za radio ili mamilioni ya maskini nchini waweze kuzitumia kirahisi kwa radio na tochi zao.
Kujadili mashati na magauni ya kuvaa wakati tuko kwenye ndege tukielekea Ulaya au wakati tuko kwenye semina za kujadili posho ni kupoteza wakati na raslimali za taifa bure.
Hivi Watanzania hatuna cha maana cha kufanya kwa ajili yetu na wajukuu zetu?
No comments:
Post a Comment