- Kila upande wa Muungano uchimbe Mafuta na Gesi Asili yake na Mapato yawe ya Serikali ya upande husika
- Shughuli za Utafutaji kwenye vitalu vyenye mgogoro ziendelee mara moja
- Zanzibar ianzishe Shirika lake la Mafuta (PetroZan)
- Katiba mpya itofautishe utafutaji (upstream) na Biashara (uchimbaji, midstream na downstream)
Moja ya suala linalosubiriwa kwa hamu kubwa katika mjadala na
hatimaye uandishi wa Katiba mpya ni suala la Mafuta na Gesi Asilia kuwa
jambo la Muungano au liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano.
Suala hili limezusha mjadala mkubwa sana mara kwa mara nchini Tanzania
kiasi cha lenyewe kuwa ni hoja ya wale wasiotaka tuwe na Dola ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Wakati Muungano unaanzishwa mwaka 1964 Mafuta na Gesi hayakuwa
masuala ya Muungano. Nimeangalia katika Hati ya Muungano ambayo ilikuwa
ni sehemu ya Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1965, suala
hili halikuwamo katika orodha ya mambo Kumi na Moja ya Muungano. Nyaraka nilizozionazinaonyesha
kwamba suala la Mafuta na Gesi Asilia liliongezwa katika orodha ya
Mambo ya Muungano mwaka 1968. Kuna watu wanahoji kihalali kabisa kwamba
nyongeza ya jambo hili ilifanywa bila kufuata taratibu na hivyo kufanywa
kinyemela na kuna wengine wanasema jambo hili lilifuata taratibu zote
za kisheria ikiwemo kupigiwa kura na Bunge la Muungano na kuungwa mkono
na theluthi mbili ya Wabunge kutoka pande zote za Muungano.
Katika moja ya vikao vya Bunge katika Bunge la Tisa, aliyekuwa Naibu
wa Waziri wa Nishati na Madini Ndugu Adam Malima alileta kumbukumbu za
mjadala Bungeni (Hansard) za mjadala wa suala la Mafuta na Gesi ili
kuthibitisha kwamba jambo hili halikuuingizwa kwenye Katiba kinyemela.
Wakati umefika kwa Watafiti wa Masuala ya Muungano wakapekua nyaraka
hizi na kutwambia ukweli ulio ukweli mtupu wa namna suala la Mafuta na
Gesi lilivyoingizwa katika orodha ya mambo ya Muungano. Hata hivyo,
jambo hili sasa ni jambo la Muungano kwa mujibu wa Katiba na ni dhahiri
kuwa WaTanzania wa Zanzibar hawafurahiswhi nalo na hivyo kuazimia
kupitia Azimio la Baraza la Wawakilishi kwamba jambo hili liondolewe
kwenye orodha ya masuala ya Muungano. Kwa vyovote vile Katiba mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapaswa kutoa uamuzi wa mwisho
utakaomaliza mjadala huu.
Jambo la kusikitisha ni kwamba licha ya Bunge la Muungano kuamua
kuongeza suala la Mafuta na Gesi asilia katika masuala ya Muungano,
mwaka mmoja baada ya uamuzi huo likaundwa Shirika la Maendeleo ya Mafuta
Tanzania (TPDC) kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano (establishment
order). Shirika hili halikuanzishwa kwa Sheria ya Bunge au kwa Sheria ya
Makampuni kama yalivyo Mashirika mengi ya Umma hapa nchini bali kwa
amri ya Rais ya mwaka 1960. Katika amri hii ya Rais, Shirika la TPDC
halikupewa ‘mandate’ ya kimuungano. Shirika hili mipaka yake ilianishwa
kuwa ni Tanzania bara peke yake. Hivyo suala la Muungano likawekewa Shirika la Tanganyika kulisimamia!
Kama ilikuwa ni bahati mbaya au makusudi au kupitiwa kwa viongozi
wetu wa wakati huo ni vigumu kujua lakini huu ni mkanganyiko mkubwa
ambao ulipaswa kurekebishwa mapema sana.
Shirika la TPDC limekuwa likifanya kazi ya kusimamia Sekta ya Mafuta
na Gesi ikiwemo kutoa vibali vya kutafuta mafuta, kuingia mikataba na
Makampuni ya kimataifa na kuisimamia mikataba hiyo. Miongoni mwa
mikataba hiyo ni kwenye maeneo ambayo kama isingekuwa Muungano yangekuwa
ni Maeneo ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Mbaya zaidi Mikataba yote ya
utafutaji na uchimbaji Mafuta inafanywa inaingiwa na Waziri wa Nishati
na Madini Wizara ambayo sio ya Muungano. Hakuna hata eneo moja ambalo
taratibu zimewekwa kwamba pale ambapo eneo hilo ni eneo lilikuwa chini
ya himaya ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar basi mikataba isainiwe na
Mawaziri wawili wa sekta hiyo kutoka kila upande wa Muungano.
Ni dhahiri kwamba kama ni kusahau hapa kulikuwa na kusahau kukubwa
ambako hakustahmiliki kwa mtu yeyote mwenye upeo achilia mbali mwananchi
wa kawaida wa Zanzibar ambaye anaona anaonewa na kugandamizwa na Bara.
Mnamo miaka ya mwanzo ya 2000, Shirika la TPDC liliingia mikataba ya
Vitalu kadhaa vya Mafuta miongoni vya vitalu hivyo ni vitalu nambari 9,
10, 11 na 12 mashariki ya visiwa vya Pemba na Unguja. Vile vile Shirika
na Wizara ya Nishati waliingia mkataba mwingine katika Kitalu kilichopo
kati ya Pemba na Tanga (mahala ambapo kumekuwa na dalili za wazi za
kuwapo Mafuta kutokana na kuonekana kwa ‘Oil sips’ mara kwa mara.
Vitalu 9, 10, 11 na 12 vilipewa kampuni ya Shell ya Uholanzi na
kitalu cha kati ya Tanga na Pemba walipewa Kampuni ya Antrim ya Canada
ambayo baadaye waliuza sehemu ya Kampuni yao kwa Kampuni ya RAK Gas
kutoka Ras Al Khaimah huko United Aarab Emirates. Kwa kuwa Vitalu hivi
vipo katika eneo la iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kabla ya
Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikataa shughuli zozote
kufanyika mpaka suala la Mafuta na Gesi kuondolewa katika orodha ya
Mambo ya Muungano lipatiwe ufumbuzi.
Uamuzi huu wa Serikali ya Zanzibar ni uamuzi ambao ungechukuliwa na
Serikali yeyote ile yenye mapenzi ya dhati na watu wake. Uamuzi huu
ulileta mjadala mpana sana katika masuala ya Muungano na ambao hawana
taarifa waliubeza sana. Hata hivyo suala hili likafanywa ajenda katika
vikao vya masuala ya Muungano vinavyoitwa Vikao vya Kero za Muungano.
Miaka kumi suala hili linajadiliwa na Maamuzi hayafanyiki! Hivi sasa kila suala lenye kuangukia kwenye Katiba husukumwa huko na hivyo kutoa ahueni kwa wanaogopa kufanya maamuzi.
Katika medani za uchumi kila suala lina muda wake. Masuala ya
utafutaji wa Mafuta ni masuala yanayoongozwa na msimu na kuendelea
kuchelewa kufanya maamuzi juu ya suala hili kunalitia hasara Taifa,
Hasara ya Mabilioni ya Fedha na hasara kubwa zaidi ya kufahamu utajiri
uliojificha chini ya Maji ya Bahari inayozunguka Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Hivi sasa Pwani ya Afrika Mashariki inarindima (trending) katika
utafutaji wa Mafuta na Gesi asilia. Huko Msumbiji Makampuni mbalimbali
yamegundua Gesi asilia nyingi inayofikia zaidi ya futi za ujazo trillion
107 (107TCF) kwa makadirio ya chini. Hapa Tanzania utajiri wa Gesi
asilia uliogunduliwa hadi hivi sasa na kutangazwa umefikia futi za ujazo
trillion 20 (20TCF) ambazo ni sawa na utajiri wa thamani ya dola za
kimarekani trillion 6. Makadirio yanakisiwa kuwa Tanzania kuna futi za
ujazo trillioni 85 (85TCF) za Gesi Asilia katika eneo la Kusini kuanzia
vitalu namba 1 mpaka namba 5 ikiwemo vitalu vya nchi kavu na vile vya
Songosongo.
Iwapo kasi ya utafutaji mafuta itaendelea kama sasa katika kipindi
cha miaka 2 ijayo Tanzania itaweza kuwa kati ya nchi mbili za Afrika
zenye Utajiri mwingi zaidi wa Gesi Asilia. Hivi sasa Nigeria ndio
inaongoza kwa kuwa na futi za ujazo trillion 189 (189TCF) ikifuatiwa na
Algeria na Angola ambazo zote zina utajiri wa juu kidogo ya 100TCF kwa
Algeria na chini ya 100TCF kwa Angola. Msumbiji sasa imeifikia Algeria
na kushika nafasi ya pili.
Katika masuala ya Mafuta na Gesi hatua ya kwanza ni kujua kama utajiri huu ambayo kitaalamu inaitwa gas exploration.
Shughuli za utafutaji zinapandisha sana thamani ya nchi na eneo la
nchi. Kwa mfano hivi sasa kitendo cha Kampuni ya Uingereza ya BG/Ophir
na ile ya Norway ya StatOil kupata mafanikio makubwa katika utafutaji wa
Gesi asilia kumeongeza thamani ya Pwani ya kusini ya Tanzania katika
medani za utafutaji (Exploration Activities).
Hata hivyo kama ilivyogusiwa hapo juu, shughuli za Utafutaji ni
shughuli za msimu. Pia huchukua muda mrefu wa kati ya miaka 5 mpaka 10
kati ya kutafuta, kupata na kuanza kuchimba. Hivi sasa ni muda wa pwani
ya Afrika Mashariki. Ni lazima kuhakikisha kwamba vitalu vyote
vilivyogawiwa hivi sasa vinafanyiwa kazi. Hata hivyo vitalu vingine
vyovyote visigawiwe kwanza mpaka hapo matunda ya vitalu vya sasa
yaonekane. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imependekeza kusimamisha
kugawa vitalu vipya. Matokeo ya utafutaji katika vitalu vya sasa yakiwa
mazuri kama ilivyo sasa, thamani ya vitalu vipya itapanda sana na nchi
itakuwa na nguvu ya majadiliano (strong negotiation position) dhidi ya
makampuni makubwa ya mafuta.
Tufanyaje kuhusu vitalu vilivyogawiwa katika eneo ambalo lina mgogoro
kuhusu suala la Muungano? Sio kazi rahisi lakini imefikia wakati
tuamue. Kwa kadri nionavyo, Itabidi kuwe na maamuzi ya mpito (interim
decisions) na maamuzi ya muda mrefu.
Kwanza, ni lazima kukiri tulipokosea. Hata kama ilikuwa ni sahihi
kiutaratibu kuweka suala la mafuta na Gesi katika orodha ya mambo ya
Muungano, haikuwa halali Shirika la TPDC lenye mipaka ndani ya Tanzania
bara kuingilia ugawaji wa vitalu na kuingia mikataba katika maeneo
ambayo ni ya Muungano. Ni Taasisi ya Muungano tu ndio inaweza
kushughulikia suala la Muungano na sio vinginevyo.
Ilikuwa ni dharau kubwa sana kwa Waziri wa Nishati ambayo sio Wizara
ya Muungano kuingia Mikataba katika eneo la Zanzibar (ambapo kikatiba
tumelifanya eneo la Muungano) bila kushauriana na kukubaliana na Waziri
wa Nishati wa Zanzibar. Kukiri kosa sio unyonge, ni uungwana. Hata
tukifanya vikao milioni moja chini ya Makamu wa Rais, bila kukiri kosa
hili tatizo hili na mengine ya aina hii hayataisha.
Pili, ni vema kukubali kwamba shughuli za utafutaji katika vitalu
vyenye mgogoro ziendelee kwenye hatua ya utafutaji tu. Kama mafuta au
Gesi ikipatikana, uchimbaji usianze mpaka uamuzi wa mwisho kuhusu suala
hili uwe umepatikana. Pia ninapendekeza ufumbuzi wa mwisho hapa chini.
Kuchelewesha utafutaji ni hasara kwa pande zote za Muungano kutokana na
taarifa za kijiolojia zitakazopatikana na hivyo kupandisha thamani ya
nchi hizi mbili kijiolojia.
Hata hivyo, utafutaji huu katika eneo lenye mgogoro kati ya pande
mbili za Muungano ufanyike baada ya mkataba wa PSA kufanyiwa marekebisho
makubwa. Marekebisho hayo ni pamoja na Mkataba kusema wazi kwamba
shughuli za uchimbaji zitafanyika iwapo tu makubaliano ya kugawana
mapato ya Mafuta na Gesi kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Zanzibar yamefikiwa. Pia Mkataba uzingatie maendeleo ya sasa ya kusini
mwa Tanzania na hivyo mkataba uboreshwe kwa faida ya nchi ikiwemo
kutolewa kwa ‘signature bonus’. Hii ni Fedha inayotolewa na Kampuni za
utafutaji Mafuta kwa Serikali kabla ya utafutaji kuanza. Kiwango
hutokana na majadiliano na kukubaliana. Nchi zenye jiolojia iliyopevuka
hutumia njia hii kuongeza mapato ya Serikali.
Mkataba pia useme kinaga ubaga kwamba utasainiwa na Mawaziri wa pande
mbili za Muungano na kwamba Kampuni inayofanya utafiti itatoa taarifa
zake za Utafiti sawia kwa Mawaziri wote kwa mujibu wa vipengele vya
mkataba.
Kwa upande wa maamuzi ya muda mrefu, ushauri wangu ni kwamba; kwa
maana ya kuandikwa kwenye Katiba mpya ni kwamba Suala la Mafuta na Gesi
Asilia liendelee kuwa suala la Muungano kwenye eneo la usimamizi wa
Tasnia na leseni za utafutaji (Upstream Regulatory mechanism). Hili ni
eneo linalohitaji usimamizi wa dhati kabisa na kwa pamoja pande mbili za
Muungano zinaweza kufanya vizuri zaidi.
Eneo la Uchimbaji na hasa kugawana mapato ya mafuta na Gesi (Profit
Oil) lisimamiwe na kila upande wa Muungano kivyake. Biashara ya Mafuta
isiwe jambo la Muungano na hivyo kila Upande wa Muungano uwe na Shirika
lake la Mafuta na Gesi ambalo litashiriki kama mbia wa Mashirika ya
Kimataifa katika uchimbaji, usafirishaji na uuzaji wa Mafuta na Gesi
Asilia. Mapato yanayotokana na Mafuta (Profit Oil) na kodi nyingine zote
isipokuwa mrahaba (royalty) yawe ni masuala yanayoshughulikiwa na
Serikali ya kila upande wa Muungano kwa mujibu wa Sheria ambayo Serikali
hizo zimejiwekea.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma ilipendekeza Bungeni
kwamba kuwepo na Mamlaka ya Mafuta na Gesi Asilia Tanzania (Tanzania
Petroleum Authority) ambayo itakuwa ni msimamizi (upstream regulator)
kama suala la Muungano. Mrahaba wa Mafuta na Gesi ambao sasa ni asilimia
12 ya Mapato ya Mafuta itakusanywa na Msimamizi huyu na ndio mapato
pekee katika tasnia ya Mafuta na Gesi yanapaswa kuwa mapato ya Serikali
ya Muungano.
Kamati pia ilipendekeza kuanzishwa kwa Shirika la Mafuta na Gesi
(Petroleum Tanzania – PetroTan) ambalo litakuwa mbia kwenye Makampuni ya
utafutaji na uchimbaji wa Mafuta na Gesi kwenye Vitalu vya Tanzania
bara. Mapato yote ya vitalu vya Tanzania bara na kodi zote isipokuwa
Mrahaba zitakwenda kwa Mamlaka za bara tutakazo kuwa tumeamua baada ya
Katiba mpya kuanza kazi. Hivi sasa TPDC inafanya kazi hii mpaka Zanzibar
jambo ambalo hata kwa akili ya kawaida halipaswi kukubalika.
Aidha, napendekeza kwamba Zanzibar ianzishe Shirika lake la Mafuta
sasa. Jambo hili halina haja ya kusubiri vikao vya kero za Muungano
kwani ni dhahiri TPDC haina mamlaka,ushawishi na uthubutu kusema uhalali
wa kusimamia vitalu vya Mafuta vilivyopo Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipeleke muswada katika Baraza la
Wawakilishi kuanzisha Shirika la Mafuta na Gesi la Zanzibar (Petroleum
Corporation of Zanzibar – PetroZan) ili liweze kushiriki katika
utafutaji na uchimbaji wa Mafuta Zanzibar. Lakini Pia PetroZan ilinde
maslahi ya Zanzibar katika tasnia hii kwa kujijengea uwezo wa kusimamia
ugawaji bora wa Mapato kutoka katika Mafuta na Gesi Asilia.
Kama Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inachelea kuanzishwa kwa Shirika
hili, Wawakilishi wa pande zote (CCM na CUF) wapeleke muswada binafsi
kuunda Shirika la Mafuta la Wazanzibari. Hawatakuwa wamevunja Katiba ya
Muungano kwani hivi sasa hakuna Taasisi yenye mamlaka ya kusimamia
Tasnia hii kwa Upande wa Zanzibar.
Wakati haya yote yanafanyika, shughuli za utafutaji Mafuta na Gesi
katika vitalu vilivyopo katika eneo la Zanzibar na hasa vitalu namba
9,10,11 na 12 na katika kitalu cha kati ya Pemba na Tanga ziendelee
kufuatia marekebisho ya Mkataba wa Utafutaji. Utafutaji wa Mafuta una
faida zaidi kwa Nchi hizi mbili kuliko kwa Kampuni za Mafuta kwani
uwekezaji wa Kampuni pekee na nchi zitapata taarifa za kijiolojia
zitakazosaidia mikataba ya baadaye kuwa bora zaidi.
Wakati nasisitiza kwamba tuendelee na utafutaji katika vitalu tajwa,
katika Katiba mpya, utafutaji wa mafuta usimamiwe na Taasisi ya
Muungano. Uchimbaji na biashara ya Mafuta ufanywe na kila Serikali ya
kila upande wa Muungano. Mafuta kuwa jambo la Muungano halafu kusimamiwa
na Shirika la Tanganyika na Wizara ya Upande mmoja ya Muungano ndio
chanzo cha mgogoro. Suluhisho sio kuifanya TPDC kuwa Shirika la
Muungano, bali kila upande upewe uhuru wa kusimamia uchimbaji, Biashara
na mlolongo mzima wa tasnia ya Mafuta (value chain from midstream to
downstream) isipokuwa utafutaji (upstream). Hili ndio suluhisho la
kudumu ninaloona linafaa.
Uwazi (declaration):
Zitto Kabwe ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na mfuatiliaji wa karibu wa
Tasnia ya Mafuta na Gesi Asilia akiwa amesomea mfumo wa uchumi wa
katika tasnia ya madini na mafuta (fiscal regime in Mineral and
Petroleum sector). Zitto pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Mashirika ya Umma ambayo inasimamia mahesabu na utendaji wa Shirika
la TPDC. Makala hii imeandikwa baada ya ziara ya Mafunzo ya Wabunge
kutembelea nchi ya Uholanzi kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya
nchi hiyo. Katika ziara hiyo Wabunge hao walikutana na Wakuu wa Shirika
la Mafuta la Shell ambapo walizungumzia pia suala la vitalu namba 9, 10,
11 na 12.
No comments:
Post a Comment