Sunday, May 6, 2012

WANAUME 6,500 WATAHIRIWA TABORA

ZAIDI ya wanaume 6, 500 waliokuwa wakiishi bila kutahiriwa katika Wilaya za Nzega na Igunga mkoani Tabora, sasa wametahiriwa chini ya mpango maalumu unaolenga katika kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi.Meneja wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la JHPIEGO Tanzania, Tawi la Mkoa wa Tabora, Simyoni Nyandenda, alisema hayo ni mafanikio makubwa mno katika utoaji wa huduma hizo mkoani humo.Kwa mujibu wa Nyandenda, Mkoa wa Tabora, una vituo vinne vinavyotoa huduma za bure za kutahiri wanaume wanaoishi bila kutahiriwa.Katika Wilaya ya Nzega, vituo hivyo viko katika hospitali ya wilaya na Hospital ya Missioni ya Ndala, wakati katika Wilaya ya Igunga, vituo viko katika Hospitali ya Igulubi na hospitali ya wilaya.Alisema idadi hiyo ya watu waliotahiriwa, imevuka malengo ya shirika lake na Hospitali ya Mkoa wa Tabora, ya kuwafanyia tohara wanaume 5,000 katika kipindi cha wiki tatu.Meneja huyo alisema zoezi hilo katika wilaya hizo, limesukumwa na kasi kubwa ya maambukizi ya virusi miongoni mwa wananchi.Alisema takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya virusi katika wilaya hizo mbili za Mkoa wa Tabora, sasa yamefikia asilimia 6.4, kiwango ambacho alisema ni kikubwa.Nyandenda alisema kasi ya maambukizi katika wilaya ya Nzega, inachangiwa na mwingiliano mkubwa wa watu unatokana na migodi na mji kuwa katika njia panda.Alisema kwa upande wake, Wilaya ya Igunga, maambukizi yanachangiwa na mji kuwa barabarani na wimbi kubwa la wachimbaji wadogo wadogo wa madini.Alisema watu ambao hawajatahiriwa, wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi, ikilinganishwa na waliotahiriwa.Alitoa wito kwa wanawake, kuwahimiza wanaume ili waende wakapate huduma hizo, ili pamoja na mambo mengine, kuwawezesha wanawake kuepuka kupata kansa ya shingo ya uzazi.

No comments: