Friday, October 5, 2012

Mahabusu amnyang'amya silaha askari na kuingia mitini jijini Arusha

Mahmoud Ahmad,Arusha

MAHABUSU mmoja ambaye hakufahamika mara moja mkazi wa jijini Arusha, ametoroka chini ya ulinzi mkali wa polisi katika mahakama kuu ya Arusha na kutokomea kusikojulikana baada ya kufanikiwa kumnyang’anya silaha aina ya SMG mmoja wa askari polisi aliyekuwa akiwalinda wakati akitolewa kwenye chumba cha mahabusu na kupandishwa kalandinga la polisi kurudishwa gerezani .

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo,lililotokea jana majira ya saa 7.30 mchana katika mahakama kuu jijini Arusha ambapo tukio hilo lilizua hofu kubwa mahakamani hapo baada ya kuwalazimu baadhi ya watumishi wa mahakama hiyo kujifungia ndani ya vyumba vya mahakama wakihofia mahabusu huyo kuwafyatulia risasi.

Taarifa zimedai kwamba mahabusu huyo alikuwa wa kwanza kutoka kwenye chumba cha mahabusu na alipomkaribia askari huyo ambaye pia hajafahamika jina lake ghafla alimvaa na kumpora silaha hiyo inayodaiwa kuwa na risasi 30 na kuruka uzio mrefu wa mahakama hiyo. 

Mashuhuda walisema kuwa mahabusu huyo wa jinsia ya kiume alitokomea na silaha hiyo kwenye mto sanawari uliopo pembezoni mwa mahakama hiyo, hata hivyo baadae aliitelekeza silaha hiyo na polisi walifanikiwa kuipata .

‘’unajua tukio hilo limewashtua watu sana hawa watumishi wa mahakama ambao walijifungia ndani wakihofia usalama wao hata hawa watu wanaokaa hapa kusikiliza kesi za ndugu zao wote walitawanyika ‘’alisema shuhuda huyo na kuongeza kuwa
‘’si jambo la kawaida kutokea ila kuna uzembe Fulani umefanywa na polisi kwani haiwezekeni askari aporwe silaha tene smg akiwa ameishikilia ,hii ni hatari sana ‘’

Baada ya tukio hilo polisi walianza kuhaha kumsaka mahabusu hiyo na kwamba wakati wakipita eneo alilokimbilia walifanikiwa kuikuta bunduki hiyo ikiwa imetelekeza kwenye mawe eneo la mtoni.Hata hivyo haikufahamika mara moja mahabusu huyo alikuwa akikabiliwa na makosa gani mahakamani hapo .

Kamanda wa polisi mkoani Arusha Liberatus Sabas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba polisi inafanya uchunguzi wa tukio hilo huku wakifanya msako mkali wa mahabusu hiyo.

No comments: