Tuesday, January 8, 2013

Na Haruni Sanchawa
KANISA lingine la ajabu limegunduliwa Bongo ambapo linafanya ibada zake kwa utofauti mkubwa na makanisa yaliyozoeleka na wengi, Uwazi limechimbua.
Kanisa hilo ambalo linajulikana kwa jina la The Pool of Siloam lililoko Mbezi- Makonde, Kinondoni, Dar es Salaam linafanya ibada zake Jumanne badala ya Jumapili wakiamini ndivyo Neno la Mungu linavyotaka.
Jambo lingine ambalo linachagiza u-ajabu wa kanisa hio ni kupinga jina la Biblia Takatifu. Muumini mgeni anayefika kwenye kanisa hilo hulazimika kukabidhi Biblia yake kwa uongozi ambapo wao hutoa ‘kava’ ya nje yenye jina la Biblia na kuweka kava nyeupe yenye maandishi ya Kitabu Cha Bwana.
Kama vile hayo hayatoshi, kanisa hilo linaamini siku za mwezi ni 28 na si 29, 30 au 31. Wanasema Mungu alipanga hivyo na ndiyo maana  aliwapa hata wanawake mzunguko wa siku 28 kuingia katika hedhi.
“Kinachotuingiza kwenye majira halisi ya Mungu ni kufuta tarehe 29, 30 na 31 za Julius Kaisari katika kila mwezi wa kalenda ya Gregori kwa mamlaka ya Mungu wa Majeshi ili kuondoa uovu ulioambatana na tarehe hizo za ziada kwenye miezi 12 ya mwaka,” alisema muumini mmoja kanisani hapo.
Uchunguzi unaonesha kuwa, kuanzia mwaka 2008 kanisa hilo lilichapisha kitabu ambacho kinaonesha kuwa mwanzo wa mwaka si Januari bali ni Machi (wao huita Abib au Aviv). Na mwisho wa mwaka si Desemba, bali ni Februari (wao huita Adari).
Kwa ugunduzi wao huo, kuanzia mwaka 2008 kanisa hilo hawafanyi ibada ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu Desemba 25, yaani Krismasi kama madhehebu mengine ya Kikristo kwa vile wanaamini Yesu alizaliwa Februari 28.
Uwazi lilipata nafasi ya kupenya hadi ndani ya kanisa hilo ambalo limejengwa kisasa na kukutana na kiongozi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Daudi Elia ambaye alisema kuwa makanisa  mengi hayafanyi kama ambavyo Mungu ameagiza.
Aidha, Daudi alimtaja kiongozi mkuu wa kanisa hilo kuwa ni Mchungaji Elia Amu wa Pili Mungu wa Majeshi Mtume na Nabii wa kizazi cha nne na akabainisha kuwa, awali alikuwa akifanya kazi Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kama  mhandisi.
“Aliacha kazi ya uhandisi na kuanza kumtumikia Mungu wa kweli kuanzia mwaka 2003, kazi  ambayo amekuwa akiifanya hadi sasa ambapo kanisa limesimama na kuenea Tanzania nzima na duniani,” alisema Daudi.
Aliongeza kuwa, Mungu alimwambia nia ya kumteua afanye kazi za kiroho ni kuvunja misingi mibovu ya kumuabudu na kuiweka inayofaa.
Mchungaji huyo ambaye alikuwa akiongea kwa niaba ya kiongozi mkuu, alisema kanisa hilo limekuwa na maagizo ya kweli ambayo  Mungu aliagiza yafanyike.
Kiongozi huyo akizungumzia namna ya kujiunga na kanisa hilo alisema kuwa, sharti la kwanza ni mtu kubadili jina lake la awali na kupewa lingine ambalo ni matakwa ya Mungu kisha kubatizwa upya.
Alisema kanisa hilo halikubaliani na mambo ya dunia kama vile kuwa na Siku ya Kifua Kikuu, Siku ya Ukoma, Siku ya Ukimwi na kadhalika kwa vile kufanya hivyo ni kwenda kinyume na ufalme wa Mungu.
Hata hivyo, baadhi ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania (KKKT) wanaoishi jirani na kanisa hilo walipohojiwa kuhusiana na nyumba hiyo ya ibada walisema wana wasiwasi na nguvu za kishirikina ndiyo zinaratibu mwenendo wao.
“Huwezi kuchana ‘kava’ la Biblia na kukataa jina la Biblia Takatifu kwa sababu kufanya hivyo ni kama uchawi ambao kwa Mungu haufui dafu,” alisema muumini mmoja ambaye alikataa kutaja jina.
Waumini hao walitofautiana na wa Kanisa Katoliki (RC) ambao walisema mambo ya kujadili namba ni mambo ya Freemason.
 “Hawa wanaosema namba za mwezi mwisho tarehe 28 ni mambo ya Freemason. Sisi tunaona hivyo,” alisema muumini mmoja ambaye naye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.
Hivi karibuni gazeti hili liliibua kanisa lingine liitwalo Brotherhood of the Cross and Star la jijini Dar ambalo waumini wake husujudu na kuingia kanisani wakiwa pekupeku huku mabikira wakipewa kipaumbele cha kupelekwa nchini Nigeria, makao makuu ya kanisa hilo.

No comments: