Monday, March 4, 2013


CHADEMA YABADILI MBINU ZA KUWANIA IKULU 2015. PIA YAZINDUA M4C JIMBO LA MBEYA


Mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe  akiongea na viongozi wa Chadema wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini katika ukumbi wa mkapa jijini Mbeya 






 Maandamano  ambayo yaliongozwa na Mbowe yaliyoanzia katika eneo la Uhasibu Mafiat hadi katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe,Mbowe aitembea kwa mwendo wa kilomita tano ambapo makundi ya waendesha bodaboda, baiskeli na watembea kwa miguu walijitokeza kwa wingi kuunga mkono maandamano hayo.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimesema kuwa kitalazimisha maandamano nchi nzima iwapo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Naibu wake hawatakubali kujiuzulu kwa kusababisha anguko la elimu nchini.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa kimeamua kuanza kutekeleza sera yake ya kuongoza kwa majimbo sasa ili kuongeza nguvu ya mapambano na harakati za kuhakikisha wanafanikisha malengo yao ya kushika dola mwaka 2015, badala ya kuendelea kutumia mfumo wa zamani ambao ilikuwa rahisi kudhibitiwa na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) .

Kadhalika, chama hicho kimesema hakitampokea mwanachama yeyote wa Chama Cha Mapinduzi atakayekosa nafasi ya kugombea kwenye chama chake na kutimkia Chadema katika dakika za mwisho kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.

Mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa Chadema wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni maandalizi ya kuzindua kanda yake kwenye kanda hiyo.

Alisema kuwa mfumo wa zamani ambao mambo yote ya harakati za chama hicho yalianzia makao makuu ya chama,  ulikuwa ni rahisi kudhibitiwa na dola ya CCM kwa kuwa walikuwa wakiwavizia viongozi wa kitaifa wanapotoka nje kwenda kuendesha harakati wanawapiga mabomu, kuwakamata na kuwafungulia kesi mahakamani.

“Tunataka dola ikusubiri viongozi wa kitaifa watoke makao makuu ili wawadhibiti, wasikie mapambano yanatokea kwenye kanda zetu kama hii ya Nyanda za Juu Kusini, kanda ya Magharibi na nyinginezo,” alisema Mbowe.

Alisema kuwa katika mabadiliko hayo pia Chadema inaachana na siasa za kiuanaharakati na badala yake inaanza kujikita kwenye siasa za maandalizi ya kushika dola.

Akizungumzia utaratibu wa baadhi ya wanachama wa vyama vingine, kikiwemo chama tawala CCM kukimbilia ndani ya chama hicho baada ya kutoswa kwenye nafasi za uchaguzi, Mbowe amesema kuwa kuanzia sasa Chadema hakitampokea mwanachama yeyote wa aina hiyo.

Mbowe alisema kuwa Chadema hivi sasa ipo kwenye maandalizi makubwa ya kunyakua dola mwaka 2015 na hivyo inao wajibu wa kuwaandaa wanachama wake ipasavyo ili kiweze kuwa na wagombea wazuri, imara na wenye uwezo wa kuwezesha chama hicho kupata ushindi mkubwa.

“Kama kuna mtu leo anakula matunda ya ufisadi ndani ya Chama Cha Mapinduzi akidhani kuwa atahamia Chadema kwa kuwa ana fedha za kununua kura za maoni, ameula wa chuya, hatutampokea mtu wa aina hiyo, ” alisema Mbowe.

Alisema kuwa kuanzia sasa Chadema itawapokea wanachama kutoka vyama vingine baada ya kuwapima uadilifu wao, kuchunguza historia yao na utayari wao wa kutumika ndani ya chama ili waweze kupata wanachama na viongozi wazuri watakaokisaidia chama kushika dola mwaka 2015.

Alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikitumia mbinu mbalimbali za kukisambaratisha Chadema, ikiwa ni pamoja na kuwatumia mamluki ndani ya chama, lakini kutokana na uimara wa Chadema mbinu hizo zimekwama na Chadema inasonga mbele.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni alisema kuwa yeye pamoja na wapambanaji wenzake wametumia zaidi ya miaka 20 kuijenga Chadema na kuipa nguvu kisiasa hadi hapo na hivyo hatakubali kuruhusu chama hicho kihujumiwe au kusambaratishwa kwa namna yoyote ile.

Alisema kuwa ikiwa wana-Chadema wataruhusu Chadema ife leo, itawachukua tena miaka 20 mingine kuijenga na kuifikisha mahali iilipo hivi leo.

Mbowe alitolea mfano wa vyama vya siasa vilivyowahi kupata nguvu na umaarufu mkubwa wa kisiasa nchini kama vile Chama cha Wananchi, CUF, NCCR – Mageuzi na TLP ambavyo alidai kuwa CCM illifanikiwa kuvizima na kuwa hata vyenyewe itavichukua muda mrefu usiopungua miaka 20 kurejesha umaarufuvilivyokuwa nao.
    
Na mbeya yetu

No comments: