Tuesday, April 9, 2013


Na Mwandishi Wetu
MAZISHI ya bilionea kijana, marehemu Nyaga Mawalla, aliyekuwa mwasisi na Mkurugenzi wa Makampuni ya Mawalla ya Arusha, yamecha mshangao.
 Mwili wa marehemu Nyaga Mawalla ukiwa katika kanisa la Kilutheri nchini Kenya usharika wa Uhuru Highway kwa ajili ya misa.
Namna bilionea huyo alivyozikwa, kaburi lake likifukiwa bila kujengwa, imefanya maziko yake yafanane na mtu wa hali ya chini.
Chanzo chetu cha habari kililiambia gazeti hili kuwa mazishi hayo yalifanyika katika Makaburi ya Jumuiya ya Langata, yameshangaza, kwani wengi walitarajia kaburi lake lingefunikwa kwa zege.
 Hata hivyo, habari zinasema, inawezekana hivyo ndivyo marehemu alivyoagiza katika wosia wake.
“Ni kweli kaburi lilichimbwa na hakukuwa na umwagaji zege au kusakafiwa. Lilikuwa kaburi la kawaida na hakukuwa na mbwembwe za kifahari, inawezekana ndivyo mwenyewe marehemu enzi za uhai wake alivyoagiza,” kilisema chanzo.
 Watoto wa Marehemu Nyaga wakiwa na ndugu zao.
Tofauti na makaburi ya matajiri wengine, la marehemu Mawalla lilichimbwa na sanduku lake lilishushwa kaburini kabla ya mchanga kutumika kulifunika na baada ya kuzikwa, watu mbalimbali waliweka mashada ya maua juu yake.
Aidha, hata wahudhuriaji wa mazishi hayo baadhi yao wakiwa wamefunga vitambaa vyekundu mkono wa kushoto, hawakuwa wengi (walikuwa kiduchu) tofauti na ilivyozoeleka katika mazishi ya watu wenye fedha au maarufu kama Mawalla.
Habari zinasema, makaburini hakukuwa na mbwembwe za vipaza sauti na muziki wa mapambio na hata wazazi wake hawakuwepo pamoja na ukweli kwamba marehemu alikuwa na uwezo mkubwa kifedha.
 Kiongozi wa Dini wa Kanisa la Kilutheri Kenya la Uhuru Highway, akiongoza mazishi.
Awali kabla ya maziko, kulizuka mvutano wa mazishi yake baada ya Wakili Fatuma Karume ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume, kupeleka wosia wa marehamu msibani uliokuwa umeelekeza kuwa ikitokea amefia nje ya nchi azikwe huko au akifia ndani ya nchini basi azikwe kwenye shamba la Momella, Arusha wakati wazazi wake walitaka azikwe kwao Marangu mkoani Kilimanjaro.
Msemaji wa familia hiyo, Joseph Nuwamanya alisema wameamua kuheshimu wosia wa marehemu.
“Familia na ndugu wote wa mpendwa wetu Mawalla waliamua marehemu azikwe jijini Nairobi kwani kabla ya kifo chake yeye mwenyewe alitaka azikwe sehemu atakayofia ikitokea amefia nje ya nchi,” alisema Nuwamanya.
Akizungumzia sababu za kifo chake alisema taarifa rasmi ya sababu za kifo chake bado hazijatolewa na uongozi wa Hospitali ya Nairobi.
  Jaji Mark Bomani naye alikuwa ni miongoni mwa waombolezaji walioshiriki mazishi hayo.
“Kumekuwa na taarifa zinazopotosha kuhusiana na kifo chake lakini nataka niseme kwamba taarifa rasmi bado haijatolewa kwani uchunguzi unaendelea na zitakapokuwa tayari kila kitu kitaelezwa,”alisema.
Mapema kabla ya mazishi hayo yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa na familia na marafiki ilifanyika misa ya kumuombea marehemu katika Kanisa la KKKK, Uhuru Highway, Nairobi.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Batilda Buriani, Sir George Kahama, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, wabunge, mawaziri, wanasheria mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania.
Mawalla alifariki dunia jijini Nairobi baada ya kuanguka kutoka kwenye ghorofa katika hospitali aliyokuwa akitibiwa Machi 22, mwaka huu, ameacha watoto wawili, Sherlyne na Margarate Mawalla.
 Familia ya Marehemu Nyaga Mawalla wakiwa wenye simanzi nzito wakati wa mazishi hayo.
(PICHA KWA HISANI YA HAKI NGOWI BLOG)

No comments: