Tuesday, May 21, 2013


Na Gladness Mallya
SAKATA la kijana Bonny Fabian Kavishe kudaiwa kumuua kwa kumpiga risasi baba yake, mzee Livingstone Kavishe akiamini ni mwizi sasa ni simulizi ya machozi kufuatia kusomwa kwa waraka mzito ulioandikwa na mtuhumiwa huyo ambaye bado yupo mahabusu ya Polisi Mlandizi, Bagamoyo, Pwani.
Majonzi na simanzi wakati wa kuuaga mwili wa marehemu, mzee Livingstone Kavishe.
Waraka huo ulizidi kuwatoa machozi baadhi ya waombolezaji siku ya mazishi yaliyofanyika Marangu, Wilaya ya Moshi Vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro kutokana na maneno yenye huruma ya Bonny kuomba msamaha.
WARAKA ULIANDIKIWA NDANI YA MAHABUSU
Habari zisizo na chenga wala kumulika tochi zinasema, mtuhumiwa akiwa mahabusu aliamua kuandika waraka huo na kumpa ndugu yake mmoja (jina halikupatikana) akimpa maelekezo kwamba usomwe siku ya mazishi ya mzee huyo kabla hajafukiwa kaburini kwa vile yeye hatakuwepo.
“Kwa kweli inauma sana! Jamaa alipoona hatapata ruhusa ya askari ili akashiriki mazishi ya baba yake aliomba karatasi na kalamu na kuandika waraka, akampa ndugu yake mmoja, akamwambia usomwe siku ya mazishi ya marehemu kabla hajafukiwa kaburini,” kilisema chanzo.
Mwili wa mzee Livingstone Kavishe ukiombewa kabla ya kusafirishwa.
MWILI WAAGWA NYUMBANI KWA MTUHUMIWA, WASAFIRISHWA NA WARAKA
Jumatano ya Mei 15, mwaka huu, mwili wa marehemu mzee Kavishe uliagwa nyumbani kwa mtuhumiwa licha ya yeye kutokuwepo na ukasafirishwa kwenda Marangu kwa mazishi.
Miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa kwenye kusafirisha mwili huo ni uwepo wa waraka huo ambao mtuhumiwa aliomba usomwe mbele ya waombolezaji siku ya mazishi.
MANENO NDANI WARAKA NI HAYA
Siku ya mazishi, mwanaume aliyepewa jukumu la kuongea kwa niaba ya familia aliusoma waraka huo huku waombolezaji wakiwa makini kumsikiliza.
Alisema waraka huo umeandikwa kwa mikono ya Bonny Kavishe, licha ya kuzungumzia mambo mengine, aliwaomba msamaha ndugu, jamaa na marafiki kwamba wamsamehe kwa kitendo cha kumuua baba yake.
Alisema alifanya kitendo hicho bila kukusudia na wala hajui nini kiliendelea. Haikuwa nia yake kumtoa uhai baba yake aliyefikia nyumbani kwake Mlandizi kwa ajili ya kusherehekea harusi ya mdogo wa mtuhumiwa huyo iliyofanyika Mei 11, mwaka huu.
Ndugu na jamaa wakiuaga mwili wa mzee Kavishe kwa majonzi.
WARAKA WAWATOA MACHOZI WAOMBOLEZAJI
Chanzo kinasema: Yaani wakati waraka huo ukisomwa ndugu na jamaa walilia sana ikawa ni machozi mara mbili. Kwanza kwa mzee Kavishe kufariki dunia, pili kwa sababu ya ndugu yao huyo ambaye yuko mahabusu kutokana na kumuua baba yake. Sehemu kubwa ya waraka huo, Bonny alikuwa akiomba msamaha.
MTUHUMIWA AFUNGA KULA NA KUNYWA
Maneno mengine yaliyopatikana ndani ya waraka huo ni mtuhumiwa kusema tangu siku ya tukio hilo, Mei 12, mwaka huu ambapo alikamatwa na kuswekwa mahabusu, hakula wala kunywa kitu chochote kwa muda wa saa 48 kwa sababu akili yake ilikinai kufuata utaratibu wa kibinadamu kufuatia kitendo cha kumtoa uhai baba yake.
TUMEFIKAJE HAPA?
Mzee Kavishe alitoka Marangu mkoani Kilimanjaro na kufika Mlandizi kwa ajili ya harusi ya mtoto wake ambaye ni mdogo wa Bonny, aitwaye Boniface Fabian Kavishe.
Baada ya harusi kumalizika, familia ilirudi nyumbani kwa Bonny kwa ajili ya kupumzika. Marehemu aliandaliwa chumba chake ambapo aliingia kulala huku akiwatakia usiku mwema wanaye.
Usiku wa saa tisa kuelekea Jumapili, mzee Kavishe aliamka, akatoka kwenda chooni. Alipomaliza alirudi ndani lakini kwa vile macho yake yalikuwa hayaoni vizuri alishindwa kutambua chumba alichokuwa amelala hivyo akajikuta akiingia chumba alicholala mwanaye Bonny na mkewe Eva.
Mwili wa marehemu wakati ukiagwa. Kichwani ni tundu la risasi.
Inadaiwa wakati huo Eva alikuwa macho, ila Bonny alikuwa usingizini. Eva alishtuka kusikia kitasa cha mlango kikishikwa na mtu kuingia, akapiga kelele za mwiziii! Mwizii jamani!
Kelele hizo zilimwamsha Bonny ambaye naye bila kujua, alichukua bastola kutoka kwenye makazi yake na kumfyatulia ‘mwizi’ huyo. Risasi ilichomoka kwa kasi na kumwingia mzee huyo kwenye paji la uso ambapo alianguka chini na kukata roho papohapo.
Baada ya tukio hilo Bonny alitoka kitandani na kwenda kuwasha taa kwa lengo la kumtambua ‘mwizi’ huyo. Hamadi! Kumbe ni baba yake ambaye muda mfupi nyuma walikuwa kwenye cherekochereko za harusi wakila na kunywa kwa furaha.
MKUU WA KITUO AMWELEZEA MTUHUMIWA
Paparazi wetu alipata nafasi ya kuzungumza na Mkuu wa Kituo cha Mlandizi, Bagamoyo, Pwani, Afande Shaban Musa ambapo alikiri kutokea kwa tukio hilo, akasema uchunguzi bado unaendelea na mtuhumiwa mpaka juzi Jumapili anashikiliwa na jeshi hilo.
Akaongeza: Hili kweli ni jambo la kuhuzunisha kwani mtuhumiwa si mtu wa shari, mpole sana lakini nilishangaa siku hiyo kumwona anakimbilia hapa kituoni mwenyewe na kusema amemuua baba yake.”
Marehemu Kavishe alizikwa Mei 17, 2013.
Mungu ailaze pema peponi rojho yake. Amina.

No comments: