Tuesday, May 28, 2013

TANZANIA YADAI KWAMBA VITISHO VYA WAASI WA M23 HAVIINYIMI USINGIZI HATA KIDOGO
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe Dar es Salaam.

Tanzania imesema vitisho vinavyoendelea kutolewa na waasi wa M23 wanaopigana Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), haviinyimi usingizi.

Kauli ya Tanzania inakuja huku kukiripotiwa kuwapo kwa mapigano makali baina ya vikosi vya Serikali waliopambana na waasi hao, ambao wameanzisha tena harakati ya kuliteka Jimbo la Goma na maeneo mengine ya jirani.
Mapigano hayo ni ya kwanza tangu M23, kuondoka mjini humo mwaka jana kufuatia shinikizo za kidiplomasia.
Umoja wa Mataifa (UN), umesema utaongeza kasi ya juhudi zake za kutafuta amani kwa kutuma kikosi cha wanajeshi 3,000 kujaribu kuzima mapigano hayo, ambayo yalisababisha watu 19 kuuawa na wengine kujeruhiwa.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe alisema vikosi vya Tanzania vilivyoko Congo vitaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia weledi na miongozo ya UN.
Kanali Mgawe alisema kauli zozote za vitisho vinazoendelea kutolewa na waasi hao, haziwezi kurudisha nyuma juhudi hizo.
Hata hivyo, Kanali Mgawe aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kutopuuzia vitisho hivyo.
“Inawezekana kuna jambo hapa maana kwa nini Tanzania ipewe vitisho ilhali operesheni hiyo ya amani inahusisha mataifa mengine?” alihoji Kanali Mgawe.

Nchi nyingine ambazo zimekubali kutuma wanajeshi wake kupigana na waasi hao ni Malawi na Afrika Kusini.
Waasi wa M23 wamekuwa wakitoa vitisho kwa wanajeshi wa Tanzania, lakini Serikali imekuwa ikitamba kuwa hivyo ni vitisho na kazi ya kulinda amani itaendelea kama ilivyopangwa. Tayari, Katibu Mkuu wa UN, Ban-Ki Moon ametembelea nchi hiyo.

No comments: