Friday, August 23, 2013

HUYU NDIYE MSANII ALIYEFILISIKA KUTOKANA NA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA

WIMBI la uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya limeshika kasi hivi sasa kwa wasanii na watu mbalimbali huku Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe akilivalia njuga kulikomesha.

Wakati hayo yakiendelea, mnenguaji aliyetikisa anga la muziki wa dansi nchini, Aisha Mohammed Mbegu ‘Aisha Madinda’ amejuta kutokana na kufilisika baada ya kutumia madawa ya kulevya.

Akizungumza katika mahojiano maalum hivi karibuni, Aisha alisema alipokuwa juu kwa unenguaji alifanikiwa kumiliki mali mbalimbali zikiwemo nyumba tatu pamoja na gari lakini madawa yamemlostisha.

Akisimulia jinsi nyumba zake tatu zilivyopotea, Aisha alisema alianza kuweka rehani ‘bondi’ nyumba yake ya Kigamboni akiwa anachukua fedha kidogokidogo hadi alipoambiwa fedha zake zimekwisha.

“Baada ya kuiweka bondi nyumba ya Kigamboni na kuambiwa sina changu nikaenda kuuza nyumba ya Kimara mwisho,” alisema.


Baada ya kumaliza nyumba zake, mnenguaji huyo akadai kuwa aligeukia gari lake aina ya Toyota Mark II ambalo nalo aliliuza.

“Niliona ujinga nilikuwa nikipata tabu ya kutafuta fedha za kununulia unga wakati gari nilikuwa nalo, nikaisukumia mbali,” aliongeza huku akisikitika kwa uamuzi huo ambao sasa anaujutia.

Aidha, Aisha alisema hivi sasa anawachukia wanaouza madawa ya kulevya kwa kuwa wanatajirika wakati wao kama watumiaji wanafilisika kifedha na kuumia kiafya.

“Sisi wanunuzi tunakuwa na maisha magumu wakati wenzetu wanatajirika, binafsi sikuwahi kutegemea kama ningeishi maisha kama haya, nawashauri mastaa wengine wanaondelea kutumia madawa hayo waache mara moja kwani madhara yake ni makubwa kiuchumi na kiafya,”
 alimalizia mnenguaji huyo ambaye hivi sasa yuko fiti na anaweza kupanda jukwaani wakati wowote

No comments: