Tuesday, March 31, 2015

JESHI LA POLISI LAENDESHA MSAKO MKALI KWA WALIOWAUA ASKARI WAWILI

Kamishina  wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani)
…Akisisitiza jambo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Kova kwa makini.
Kova akiendelea kutoa ufafanuzi.
Baadhi ya polisi wakimsikiliza bosi wao.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Pwani linaendesha oparesheni kali ya aina yake ya kuwasaka majambazi waliowavamia, kuwaua askari wawili na kumjeruhi mmoja na kisha kupora bunduki aina ya SMG.
Tukio hilo limetokea tarehe 30/03/2015 majira ya saa mbili usiku huko barabara ya Kilwa Kata ya Vikindu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani.  Katika tukio hilo majambazI wapatao 8 hadi 10 wakiwa na mapanga na silaha zingine waliwavamia ghafla askari watatu waliokuwa kazini katika eneo la kizuizi cha Polisi kilichopo kijiji cha Kipara mpakani Kata ya Vikindu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani.  Majambazi hao waliwashambulia ghafla askari hao kisha kupora silaha aina ya SMG ikiwa na risasi 30 ndani ya magazine na kutokomea kusikojulikana.
Majina ya askari wa Wilaya ya Kipolisi ya Mbagala waliouawa ni kama ifuatavyo:
  1. D.2865 SGT FRANCIS,
  2. E.177 CPL MICHAEL,
Askari mwenye namba D5573 D/SGT ALLY amejeruhiwa kwa risasi kwenye paja la mguu wa kushoto na amelazwa katika hospitali ya Temeke kwa matibabu.  Askari huyu kabla ya kujeruhiwa alipambana vikali na majambazi hayo kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo aina ya SMG ambayo walishindwa kumpora hivyo wakatokomea kuelekea porila Vikindu.
Katika oparesheni hiyo, nguvu na mbinu zote za kipolisi zitatumika ambapo vikosi vya Dar es Salaam na Pwani vilianza kufanya oparesheni hiyo mara baada ya tukio ili kuhakikisha kwamba majambazi hao wanapatikana haraka iwezekanavyo.
Pamoja na oparesheni hiyo kali inayoendelea, Jeshi la Polisi linachunguza ili kubaini kama tukio hili linaashiria vitendo vya ugaidi au ni ujambazi wa kutumia silaha.
Natoa wito kwa wananchi wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kupitia (dhana ya polisi jamii) kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa hali na mali kwa kutoa taarifa sahihi.

IMETOLEWA NA:
S.H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAM

(PICHA ZOTE NA ISSA MNALLY)

No comments: