DUNIANI tunajifunza na kuona vitu vingi tofauti vya kushangaza, kuogofya na kufurahisha. Wengi hawamjui Valentine Strasser ambaye aliwahi kuwa rais wa nchi ya Sierra Leone kati ya Aprili 29, 1992 hadi Januari 16 , 1996 akiwa ndiye amiri jeshi mkuu na kiongozi wa ngazi ya juu kwenye taifa hilo lililopo kaskazini-magharibi mwa bara la Afrika.Wakati akiingia madarakani aliweka rekodi ya kuwa kiongozi mwenye umri mdogo zaidi, yaani akiwa na chini ya miaka 25.
Kapteni Valentine Strasser kiongozi wa mapinduzi ya Rais Saidu Momoh.
Aprili 29, 1992, Strasser akiwa kijana mwanajeshi mwenye cheo cha kapteni, akiwa na umri wa miaka 25, aliwaongoza wanajeshi wenzake kuvamia Ikulu ya Sierra Leone, walimkuta rais amejificha ndani ya kabati lililopo kwenye chumba cha kuogea, kisha wakamteka Rais Joseph Saidu Momoh na wakamlazimisha kukimbia, naye akatorokea Conakry, Guinea.
Valentine Strasser baada ya mapinduzi kufanikiwa.
Strasser alichukua madaraka ya nchi hiyo siku tatu tangu ashehereke sikukuu yake ya kuzaliwa.
Baada ya Momoh kutorokea Conakry, Strasser alijitangaza kuwa Rais wa Sierra Leone. Aliwaongoza vijana wenzake sita waliofanikisha mapinduzi hayo na kuunda serikali ya mpito waliyoipa jina la National Provisional Ruling Council (NPRC).
Maisha yakabadilika, alishakuwa mkuu wa nchi, kwa hiyo hakutaka kuishi kwenye nyoyo za Wasierra Leone.
Hakulipa malimbikizo ya mishahara ya wanajeshi na watumishi wengine wa umma.
Alifuja almasi ya Sierra Leone, kwa vile jina lake ni Valentine, basi sikukuu ya Valentine’s Day akaifanya kuwa sherehe ya kitaifa yenye mapumziko huku sherehe kubwa ikiandaliwa ikulu ya nchi hiyo.
Strasser alikuwa na mbwembwe nyingi, mwaka 1993 katika mkutano wa wakuu wa serikali katika nchi za Jumuiya ya Madola, uliofanyika Limassol, Cyprus, alitinga kwa mbwembwe akiwa amevaa suruali ya jeans na fulana yenye maandishi Sunny Days in Cyprus (Siku za Jua Kali Cyprus).
Alikuwa mtu wa starehe, vurugu nyingi kwa wanawake, aliua watu wasio na hatia.
Strasser alisahau kuwa ipo siku uongozi hautakuwa kwenye mikono yake, na ambacho kinaweza kumfaa ni kuishi ndani ya mioyo ya watu ili wamtetee na kumpigania baadaye. Januari 16, 1996, Strasser alipinduliwa na msaidizi wake, Brigedia Jenerali Julius Maada Bio.
Strasser akakimbilia Uingereza, akajiunga na Chuo Kikuu cha Warwick, kilichopo mjini Coventry, akaanza masomo ya sheria, akasema anataka awe wakili ili awatetee Waafrika.
Mwaka mmoja wa masomo, Strasser aliishiwa fedha, akaacha chuo.
Maisha Uingereza yakawa magumu, akakimbilia Gambia nako kukawa pagumu, mwisho akarudi Sierra Leone, mjini Grafton, mashariki mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Freetown.
Kazi ya kwanza ambayo Strasser aliifanya, ikawa kuanzisha kichuo kidogo cha kufundisha kompyuta na teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama). Maisha ya chuo yakamshinda.
Baada ya kila kitu kwenda kombo, Strasser alirudi nyumbani kwa mama yake mzazi na kuishi kwenye banda la uani.
Hata sasa, akiwa na umri wa miaka 49, anakunywa pombe za kienyeji mtaani.
Picha ya Valentine Strasser alivyo sasa.
Hana hadhi yoyote kama kiongozi mkuu wa nchi mstaafu. Strasser anaishi kama mtu wa kawaida tu mtaani. Mlevi na hakuna anayemjali.
Hana mtu wa kumtetea wala kumpigania kwa sababu hakuishi kwenye nyoyo za watu. Strasser ndiye mkuu wa nchi wa zamani, anayeishi kimaskini kuliko wakuu wote wa nchi duniani.
Ukiwa kiongozi na kugeuka kituko kama Strasser inawezekana kabisa.
Ishi vibaya na watu wasikupende, akija mtawala ambaye hatakutambua kama mkuu uliyepita, unaweza kuishi maisha ya hovyo kama ombaomba mtaani au kuwa mnywa gongo uliyeshindikana.
Vyema sasa viongozi wote duniani watambue kwamba uongozi ni dhamana, wafanye kazi kwa kujituma na wataishi mioyoni mwa wananchi waliowaongoza milele. Kuna viongozi wengi waliofanya mema na bado wanaenziwa mpaka sasa kama Julius Nyerere na Nelson Mandela, wako wengi hawa ni baadhi tu ya viongozi walioweka mbele maslahi ya wananchi wao na watakumbukwa milele.
Na Leonard Msigwa/GPL
No comments:
Post a Comment