Serikali imeanzisha kampeni ya kupambana na ugonjwa wa malaria inayojulikana kama "Zinduka Malaria haikubaliki" ambayo itazinduliwa na Rais Jakaya Kikwete Februari 13, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kampeni hiyo ilianzishwa jana jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi.
Kadhalika, Profesa Mwakyusa, amesisitiza kuwa serikali itatumia dawa ya DDT pamoja na njia nyingine ili kutokomeza ugonjwa wa malaria hapa nchini.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam na kusema serikali pia itatumia nyenzo zilizopo kwa kushirikiana na wananchi ili kupunguza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2013.
Aliongeza kuwa lengo la serikali ni kupunguza malaria kwa asilimia 80 kufikia mwaka 2013 na kwamba hatua nyingine itakayosaidia zoezi hilo ni pamoja na serikali kuanza kutumia kifaa kipya cha utambuzi wa vimelea vya ugonjwa huo.
Profesa Mwakyusa alisema serikali imeweka mikakati ya kutokomeza ugonjwa huo ikiwemo kuanza kugawa vyandarua viwili kwa kila kaya ifikapo Aprili, mwaka huu na kuhamasisha mama wajawazito kuvitumia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, alisema vita vya kupambana na malaria si ya mtu mmoja au serikali pekee bali ni ya jamii nzima.
Alisema ili kuweza kupiga vita ugonjwa huo, ni lazima watu wajue madhara yake katika jamii.
"Mtu akifahamu kwanini anakwenda vitani kupigana ndiyo ataweza kupigana vizuri zaidi," alisema.
Alisema Balozi wa zamani wa Marekani hapa nchini, Mark Green, ambaye anaongoza kampeni ya kupambana na ugonjwa huo katika nchi za Afrika, ndiye aliyemuomba kusaidia katika kampeni hiyo.
Aliongeza kuwa mfanyabiashara akichuma na kupata faida anatakiwa kurudisha sehemu ya faida aliyopata kwa jamii ambayo imemwezesha.
Alisema wafanyabiashara wanatumia watu kuzalisha mali na kwamba wazalishaji hao wanapougua tija inapungua na kwamba mtu yeyote anayetaka kupata faidi lazima ahakikishe wafanyakazi wake wana afya nzuri.
Mengi alisema Watanzania wengi wamejiajiri wenyewe na kwamba wanapougua malaria kipato chao hushuka hivyo kuwafanya wafanyabiashara kushindwa kuuza bidhaa zao kwa watu wasiokuwa na kipato.
Aidha, Mengi alisema umaskini unaongezeka kwa mtu anayeugua malaria na kwamba wananchi lazima wawaonee huruma wenzao wanapopatwa na tatizo hilo.
Aliipongeza serikali kwa kuonyesha njia madhubuti ya kutokomeza ugonjwa huo hapa nchini.
Naye Balozi wa zamani wa Marekani hapa nchini, Mark Green, aliwataka wananchi kushirikiana kwa pamoja katika kutokomeza ugonjwa huo ikiwemo kujikinga wasiupate.
No comments:
Post a Comment