Kamanda Kova akiwatambulishwa watuhumiwa Edmunda Kapama (shoto) na Deogratius Ngassa kwa wanahabari leo sentro, akiwahusisha katika sakata la Jerry Muro

JESHI la Polisi linasita kumfikisha mahakamani mwandishi wa habari za uchunguzi, Jerry Muro, ambaye ni maarufu kwa kufichua uozo, baada ya kumkamata kwa tuhuma za kudai rushwa kwa nguvu, lakini Baraza la Habari (MCT) limetaka afikishwe mahakamani haraka ili haki itendeke.
Muro, mfanyakazi wa Shirika la Utangazaji (TBC), aliachiwa huru juzi jioni baada ya kushikiliwa kwa saa saba kwenye Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es salaam akidaiwa kutaka fedha kwa njia ya vitisho kutoka kwa mhasibu aliyesimamishwa wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alimsimamisha kazi Wage pamoja na viongozi wengine wa halmashauri hiyo kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za serikali. Watakuwa chini ya uchunguzi ingawa nafasi zao zimeshazibwa na watu wengine.
Kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es salaam, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa jeshi lake halitapeleka mahakamani shitaka la Muro hadi wakili wa serikali atakapolipitia na kujiridhisha kama kuna ushahidi wa kutosha wa kufanya hivyo.
Ushahidi huo unaotarajiwa kufikishwa kwa mwanasheria huyo wa serikali ni pamoja na taarifa zilizorekodiwa katika vyombo vya kurekodia picha za matukio (CCTV) zilizopo katika baadhi ya hoteli walizowahi kukutana Wage na Jerry pamoja na kufuatilia mazungumzo yao waliyoyafanya kwa njia ya simu tangu mwanzo wa sakata hilo hadi kukamatwa kwa Jerry.
Kamanda Kova alisema tukio hilo lilianzia Januari 28 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani nyumbani kwa Wage ambaye anadaiwa kuieleza polisi kuwa siku hiyo majira ya saa 12:00 jioni alifuatwa na watu watatu ambao wawili walijitambulisha kuwa makamanda wa Takukuru na mmoja ni mwanajeshi wa cheo cha nyota tatu lakini pia ni mwandishi.
"Wage alidai kuwa watu hao watatu walimfuata nyumbani kwake Bagamoyo na kumweleza kuwa ni fisadi mwenye majumba mkoani Morogoro, mali nyingi na akaunti zake nyingi wanazifahamu hivyo wanamtaka atoe Sh10milioni au wamchukulie hatua za kisheria na kumtoa katika kipindi cha Usiku wa Habari cha TBC 1," alisema Kamanda Kova.
Kamanda Kova alisema baadaye Wage alidai aliwataka watu hao kukutana nao Hoteli ya City Garden jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukabidhiana fedha hizo, lakini kabla ya kwenda huko alifika polisi na kutoa taarifa kuwa kuna matapeli watatu wanamsumbua.
Kova alisema Wage alidai kuwa watu hao wanataka awape fedha, lakini hakuwa tayari na ndio maana akatoa taarifa hizo polisi ili wakamatwe.
Kova alisema baada ya kupokea taarifa hizo jeshi lake likajua kuwa hao ni matapeli wanaojitokeza jijini hivyo wakaweka mitego ili kuwakabili, lakini walipofika eneo la tukio mtuhumiwa alikataa kutoka kwenye gari lake lenye namba za usajili T 545 BEH aina ya Toyota Cresta aliyoenda nayo eneo hilo na kumtaka Wage kwenda kumalizana naye ndani ya gari hilo.
"Wage alitupa uthibitisho kuwa kwenye gari hilo kuna miwani yake na karatasi nyepesi (tissue) alizozisahau baada ya kukutana na watu hao kwa mara ya kwanza.
Pia Kova alisema Wage alidai kuwa alipopanda gari hilo kwa mara ya kwanza aliona bastola na pingu ambazo alidai mwandishi huyo alizitumia kumtishia, jambo lililowastua askari alioongozana nao na kuvamia gari hilo kwa uchunguzi ili kutopoteza ushahidi,’’ alisema Kova.
Kova alinukuu sheria namba 292 ambayo alisema inakataza mtu yeyote kutumia vibaya silaha yake kwa kumtishia mtu ama kuomba rushwa na hivyo inaruhusu mtu huyo kukamatwa na kwamba ndivyo ilivyokuwa kwa Jerry Muro.
Alisema walipolichunguza gari hilo walikuta bastola aina ya CZ97B ya yenye namba A6466 iliyokuwa na risasi 10 ambayo iliyotengenezwa Jamhuri ya Check. Alisema pia walikuta pingu moja sehemu ya mbele ya gari hilo.
Kova alidai kuwa Jerry aliwaambia kuwa alinunua pingu hiyo na bastola aliyokuwa akimiliki, lakini alishindwa kuthibitisha kwa kutoa risiti za manunuzi ya pingu hizo. Pia polisi walikuta miwani ambayo Wage alidai kuisahau kwenye gari hilo.
"Ukweli baada ya kumkamata mtuhumiwa askari walishangaa kumkuta Jerry Muro wa TBC1, hivyo wakalazimika kumchukua hadi Central kwa mahojiano na kisha tukakubali awekewe dhamana kwa kuwa tunamwamini lakini tumemtaka hadi leo jioni (jana) atuletee risiti ya pingu aliyokutwa nayo kwenye tukio na tunajua hataipata kwa kuwa hakuna maduka yanayouza pingu kwa wananchi," alisema Kamanda Kova.
Kova alikana polisi kumpa Jerry pingu hizo na kwamba hakuna tukio la kutishiwa kwa Jerry Muro lililowahi kuripotiwa polisi.
Alisisitiza kuwa jeshi lake haliangalii nani aliyetenda kosa bali linafuata haki na sheria kwa yeyote atakayetenda kosa hata kama ni afisa wa ngazi za juu wa jeshi hilo atakapotenda kosa atachukuliwa hatua za kisheria.
"Tuhuma hizi zisihusishwe na ugomvi na Jeshi la Polisi kwa kuwa polisi haina ugonvi wowote na Jerry. Jerry ni rafiki yetu kikazi na hatuna ugomvi wowote pia tunamshauri atulie na aache kuzungumza hovyo na vyombo vya habari kwa kuwa anaweza kujiharibia katika kesi yake kama atazungumza vitu tofauti na vilivyorekodiwa katika CCTV za baadhi ya mahoteli alikowahi kukutana na Wage,"alisema Kova.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji (TBC), Tido Mhando aliliambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa Jerry Muro bado ni mfanyakazi wa shirika hilo kwa kuwa hawajapokea taarifa zozote za kiofisi za kimaandishi kutoka polisi zinazoeleza tuhuma hizo kwa mfanyakazi wao.
"Nasi tunazisikia juu juu; hatujapata barua kamili hivyo tukipata tutajua nini cha kufanya,’" alisema Tido.
Wakati huohuo, Baraza la Habari Tanzania(MCT) limetaka uchunguzi wa sakata hilo ufanyike haraka ili Muro afikishwe mahakamani ambako haki hutendeka.
"MCT inataka apelekwe Mahakamani haraka iwezekanavyo ili hukumu itolewa kama ana makosa au la," alisema jana katibu wa baraza hilo, Kajubi Mukajanga jijini Dar es Salaam.
Mukajanga alifafanua kwamba hatua ya kuomba mtuhumiwa Muro kufikishwa haraka mahakamani ni kutokana na suala hilo kuvuta hisia za watu wengi.
"Tayari wananchi wamekuwa na hisia tofauti kuhusu tuhuma hizi, sasa chombo kinachoweza kuweka mambo sawa ni mahakama. Na sisi tutakuwa tayari kumuwekea wakili," alisema.
Mukajanga alisema tuhuma hizo zinatia doa na kuweka maswali mengi katika tasnia ya habari nchini, hivyo ameziomba taasisi zote za kiusalama zimchukulie Muro kama mtuhumiwa na si mhalifu.
Pia Mukajangaa alisema kabla ya kukamatwa, Muro alikuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha kipindi ambacho kilikuwa kinaonyesha jinsi vigogo wa serikali, wakiwemo baadhi ya mawaziri wakifanya vitendo vya rushwa.
"Tulikuwa na taarifa kuwa alikuwa anakamilisha habari nzito ya rushwa iliyokuwa ikiwahusisha viongozi wa serikali, wakiwemo baadhi ya mawaziri," alisema Mukajanga.
Muro alianza kupata umaarufu baada ya kutoa taarifa iliyoonyesha jinsi askari wa usalama barabarani wanavyochukua rushwa kutoka kwa madereva wa magari yaendayo Morogoro. Taarifa hiyo ilitingisha Jeshi la Polisi na kabla ya kurekebisha mambo, Muro alitoa tena kipindi kingine kinavyoonyesha rushwa kama hiyo mkoani Iringa.
Kukamatwa kwa mwandishi huo ni mwendelezo wa wimbi la matukio ya kukamatwa kwa waandishi mara baada ya kuripoti uozo katika taasisi za serikali. Mwaka 2004, mwandishi mwandamizi wa IPP, Zephania Musendo alikamatwa kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa kigogo wa
Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takuru).
Alikamatwa baada ya kutoa habari mfululizo kuhusu uozo uliokuwa unaihusu taasisi hiyo, hasa migongano ya vigogo wa Takuru, ambayo kwa sasa imeongezewa majukumu na kuitwa Takukuru. Mwandishi huyo alitiwa hatiani mwaka 2005 na kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Mwaka 2002, mwandishi wa Mwananchi, George Maziku alikamatwa na polisi kwa madai ya ya kuingilia uhuru wa Bunge baada ya kuandika habari kuwa baadhi ya mabadiliko ya sheria yalilenga kukipa upendeleo chama tawala na kwamba suala la takrima lingechochea rushwa.
Maziku alihojiwa na polisi kwa saa kadhaa na baadaye kuachiwa bila ya kufunguliwa mashtaka.
Mwaka 1996, mwandishi wa IPP mkoani Ruvuma, Adam Mwaibabile alikamatwa kwa tuhuma za kukutwa na nyaraka za serikali. Mwandishi huyo alikuwa anachukiwa na uongozi wa mkoa kutokana na kuripoti uozo uliokuwa ukifanywa na viongozi wa juu wa serikali ya mkoa.
Inadaiwa alikutwa na nyaraka kutoka kwa mkuu wa mkoa ambayo ilikuwa ikimuelekeza mkurugenzi kutompa mwandishi huyo leseni ya biashara. Alipatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela mwaka mmoja, lakini juhudi za wanaharakati na wadau wa habari zilimrejesha mahakamani kupinga hukumu hiyo na akashinda na kuachiwa huru.
Imeandikwa na Festo Polea, Fatma Aziz na Sadick Mtulya
No comments:
Post a Comment