Na Issa Mnally
Baada ya mateso ya muda mrefu ya Watanzania kulala nje ya Ubalozi wa China uliopo jijini Dar es Salaam wakifuatilia vibali vya kuingilia nchini humo ‘Viza’, suala hilo sasa limechukua sura mpya baada ya wananchi kufanya vurugu kwenye ubalozi huo wakishinikiza kulegezwa kwa masharti.
Tukio hili lililovuta hisia za watu wengi lilijiri Aprili 10, mwaka huu na kusababisha afisa mmoja wa ubalozi huo kutekwa na wananchi hao akishinikizwa amwite Balozi wa China nchini Tanzania, Liu Xinsheng ili aongee nao.
“Huondoki hapa mpaka umwite balozi mwenyewe. Hii ni nchi yetu, tumechoka na manyanyaso yenu. Nyiye mnaingia kila siku hapa kwetu kufanya biashara, lakini sisi tukitaka kwenda kwenu mnatutenda kama mbwa kwa kutukeshesha hapa nje ya ubalozi wenu,” walisema Watanzania hao huku wakionekana kupandwa na hasira.
Kufuatia shinikizo hilo, afisa huyo alilazimika kupiga simu kwa bosi wake huyo ili kumwita.
Hata hivyo, badala ya balozi huyo kutoka yeye, alimtuma afisa mwingine, jina lake halikuweza kupatikana mara moja, ambaye alipofika ndipo wananchi hao wakamwachia afisa waliyekuwa wamemteka na kuanza kuongea na mtu huyo.
Katika kujibu malalamiko ya wananchi hao, afisa huyo alisema hata wao wanaelewa hali ni mbaya lakini ni kwa sababu hawana wafanyabiashara wengi ndiyo maana wanachukua jumla ya watu 20 tu kwa siku ingawa wanapokea maombi kati ya 200 hadi 300 kwa siku moja.
Baada ya majibu hayo afisa huyo aliondoka kwa dharau akiwa amesusa kuongea zaidi na wananchi hao.
“Mnaona mnaona, hawa Wachina wanadharau sana. Sasa ngoja, muda si mrefu tutaanza chuki dhidi yao kama ilivyotokea kule Afrika Kusini. Tutawaondoa wote warejee kwao,” alisema mwananchi mmoja.
Tukio la Afrika Kusini alilomaanisha ni lile lililoitwa ‘Xenophobic’ ambapo wazawa waliwachinja wageni kwa chuki wakidai kwamba, waliingia nchini mwao kuchukua nafasi zao za ajira na kufanikiwa.
Aidha, kitendo cha dharau kilichofanywa na afisa huyo wa ubalozi kilisababisha wananchi waamue kutumia nguvu kuingia ndani ili waonane na Balozi Xinsheng, uamuzi uliosababisha vurugu kubwa kwenye lango la ubalozini hapo.
Hata hivyo, ghafla Askari wa Kampuni ya Ulinzi ya KK Security na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walifika kujaribu kutuliza vurugu hizo.
Ndipo uongozi wa ubalozi ukaruhusu wawakilishi kadhaa wa wananchi hao kuingia ndani kuonana na maafisa wengine wa ubalozi huo.
Ndani ya ubalozi huo yalitolewa masharti kwamba, mwandishi wa gazeti hili, Issa Mnally asiingie na kamera kitendo ambacho hakikukubaliwa na wawakilishi hao hivyo kufanya mazungumzo hayo kushindikana.
Nje nako, hali ilizidi kuwa mbaya kwani wananchi walijiandaa kufanya fujo zaidi, ndipo askari wa FFU walipoamua kuingia ndani na kuomba kuonana na balozi ili kutafuta suluhu ya tatizo hilo.
Baada ya majadiliano yaliyochukua takribani dakika ishirini, uongozi wa ubalozi ulitoa tamko kuwa, umekubali kuongeza idadi ya maombi kutoka 20 ya zamani hadi 50 ili kupunguza jazba za wananchi.
Hata hivyo, bado wananchi hao walionesha kutoridhishwa na majibu hayo wakitaka Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuingilia kati suala hilo ili utaratibu wa Viza ubadilishwe na kuwa kama balozi nyingine ambazo hazina matatizo kama ya China yaliyotafsiriwa kama unyanyasaji wa raia.
“Kwa nini wasifanye kama ubalozi wa Marekani. Kule tunajaza fomu kupitia mtandao, hakuna usumbufu kabisa?” Alisema mwananchi mmoja.
Madai hayo yaliyotolewa na wananchi na kurekodiwa na gazeti hili yamesema kuwa, kinachofanywa na Serikali ya China ni utekelezaji wa mpango kabambe wa kuwaendeleza raia wake walioko nchi za nje.
Madai hayo yakaendelea kusema kuwa, Serikali hiyo inawabana wageni kwenda kwao kununua bidhaa ili Wachina walioko katika nchi hizo waliochukua uajenti wa viwanda vya kwao waweze kufanya biashara vizuri na kutajirika huku wazawa wakizidi kufa kiuchumi.
“Tumeshaufahamu mpango wao na sisi hatukubali, kama hivyo ndivyo basi Wachina wasiingie kabisa hapa nchini kwetu,” alisema mwananchi mmoja.
Aidha, wananchi hao wamepeleka kilio chao kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, asaidie kuwaondolea kero hii ya Viza katika ubalozi huo, wanaamini anaweza kuwasaidia.
No comments:
Post a Comment