Habari na Exuper Kachenje, Andrew Msechu na Mashirika ya Kimataifa
Rais wa Marekani Obama akifuatilia kwa karibu kifo cha jaidi Osama Bin Laden
Rais wa Marekani Obama akifuatilia kwa karibu kifo cha jaidi Osama Bin Laden
RAIS Barrack Obama wa Marekani alishuhudia moja kwa moja (live) jinsi makomandoo 100 wa jeshi lake wakitekeleza shambulizi na hatimaye ‘mazishi’ ya kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa al Qaeda, Osama Bin Laden.
Operesheni hiyo ilishuhudiwa pia na Makamu wa Rais Joe Biden, Waziri wa Mambo ya Nje, Hillary Clinton, Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), Leon Panetta na viongozi wengine wa ngazi ya juu. Makomandoo hao walifanya kazi hiyo usiku wa giza nene wakiwa wamevaa miwani maalumu iliyowawezesha kuona.
Ilikuwa kama sinema wakati walipokuwa wakiendesha operesheni hiyo. Obama aliangalia tukio hilo zima akiwa Ikulu ya Marekani ya Washington-DC. Kazi hiyo ilitumia dakika 40 na kuhitimisha miaka 10 ya kujificha na kuwa tishio la mashambulizi ya kigaidi.
Kushuhudiwa huko moja kwa moja kwa operesheni hiyo, kuliwezeshwa na makomandoo hao kwani walivaa kamera maalumu zilizorekodi matukio yote yaliyokuwa yakifanyika na kuyarusha moja kwa moja hadi Ikulu ya Marekani na Makao Makuu ya CIA.
Kwa mujibu wa mtandao wa Gazeti la Daily Mail la Uingereza, shambulizi hilo lilifanyika huku kukiwa na wingu zito lililotanda katika Mji wa Abbottabad, Pakistan hali ambayo ilielezwa kwamba ilikuwa mwafaka kutekeleza kazi hiyo baada ya kuiahirisha usiku wa siku iliyotangulia.
Taarifa zinasema wachambuzi wa taarifa wa CIA walitumia mwezi mmoja wakifuatilia mtambo wa 'satellite' kujua kilichomo ndani ya nyumba alimouawa Osama kisha kuandaa ramani ilioongoza utekelezaji wa shambulizi hilo.
Habari hizo za kipelelezi zinaeleza kuwa Aprili 13, helikopta aina ya Black Hawks na makomandoo hao walikwenda hadi kituo cha anga Tarbela Ghazi, Kaskazini Mashariki mwa Pakistani ambacho CIA inaruhusiwa kutumia.
Siku ya shambulizi hilo, makomandoo hao waliruka kutoka katika helikopta hizo na kutua juu ya jumba la Osama wakiwa gizani baada kuzima taa za helikopta zote walizotumia.
Walinzi wa Osama walishtuka na kufyatua risasi kutoka katika paa la nyumba hiyo na walifanikiwa kuitungua helikopta moja kwa kutumia roketi.Maofisa wa Marekani walisema tukio hilo lilimshtua Rais Obama na kumkubusha tukio la mwaka 1993 la Somalia ambalo Black Hawk ilitunguliwa na kuua Wamarekani 18.
Makomandoo 24 waliruka uzio mrefu wa nyumba ya Osama wakaanza kutambaa na kuingia chumba hadi chumba wakimsaka. Walifanikiwa kumkuta akiwa katika chumba kimoja akiwa na watu wengine watatu akiwamo mmoja wa watoto wake wa kiume na mwanamke anayeelezwa kuwa ni mkewe.
Hata hivyo, Osama alikataa kujisalimisha huku mkewe huyo kwa kushirikiana na mtoto wa kiume wa Osama na watu hao watatu walijaribu kumuokoa kiongozi huyo wa mtandao wa ugaidi duniani kwa kukaa mbele yake. Wote waliuawa.
Baada ya kuuawa, mwili wake ulichukuliwa kwa helikopta ukiwa umening'inizwa na dakika 40 baadaye, ulizikwa baharini. Ikulu ya Marekani ulidai kwamba alizikwa kwa kufuata taratibu zote za Kiislamu.
Habari zinasema kuwa taarifa zilizofanikisha shambulizi hilo zilianza kupatika miaka minne iliyopita kutoka kwa wafungwa wa ugaidi katika Gereza la Guantanamo Bay baada ya kuteswa.
Wafungwa hao walimtaja, Khalid Sheik Mohammed kuwa ni mmoja kati ya watu wachache walioaminiwa kwa dhati na Bin Laden akisadikiwa kuwa ndiye aliyeandaa mashambulizi ya Septemba 11, 2001 Marekani na kuwa hakuwahi kutumia mawasiliano ya simu kwa miaka saba.
Mamia ya watuhumiwa ambao wengi wao ni kutoka Afghanistani na Pakistani wamewahi kuripotiwa kupata mateso makali, ikiwamo kulala ndani ya maji, kukoseshwa usingizi na kuwekwa katika vyumba vya kiza vyenye kelele.
Mwanzoni mwa mwaka huu, mtandao wa Wikileaks ulifichua mawasiliano ya siri yaliyoonyesha kwamba watuhumiwa wanaoshikiliwa katika gereza hilo walitoa taarifa kuhusu mmoja wa wasaidizi ambaye hupeleka taarifa na vifurushi kwa Bin Laden katika mji huo wa Abbottabad.
Maofisa wa CIA wanasema, awali Septemba mwaka uliopita, walipata taarifa nzito za uwezekano wa kuwapo Osama katika mapango huko Pakistani, lakini Februari mwaka huu maofisa upelelezi walipata uhakika wa makazi ya Osama na familia yake yalipo.
Wanaeleza kuwa mawakala wa CIA wa Pakistani walibainisha makazi hayo na kupachika kamera katika jengo hilo zilizowezesha kufuatilia mwenendo wa nyumba hiyo na kugundua kuwa familia inayoishi humo ni ya Osama Bin Laden.
Kwa mujibu wa CIA, ushahidi wa kwanza kwa kuwapo kwa Osama katika nyumba aliyokutwa ni wa sauti iliyorekodiwa akizungumza ambayo ilinaswa na mawakala hao wa CIA ambayo ilichunguzwa na kugundulika kufanana na sauti zake nyingine zilizorekodiwa siku za nyuma.
Baada ya hapo kamera zilizotegwa zilifanikiwa kupata picha ya Osama akiwa ndani ya nyumba hiyo na kupelekwa kwa Rais Obama Machi, 14 ambaye aliitisha mkutano wa kwanza wa siri kati ya mitano na washauri wa masuala ya ulinzi.
Uhusiano wa Pakistani, Marekani shakani
Kukamatwa kwa Bin Laden akiwa katika ardhi ya Pakistani kumeibua wasiwasi kuhusu mtazamo wa mataifa ya Magharibi na nchi hiyo, huku Serikali ya Pakistani ikisisitiza kwamba haikujua lolote kuhusu uwapo wa kiongozi huyo wa kigaidi katika eneo hilo.
Wanasiasa na wanataaluma walieleza kuwa ni vigumu kuaminika kwamba vyombo vyote vya upelelezi na vya usalama vya Pakistani havikuwa na taarifa yoyote kuwa kiongozi huyo wa kigaidi ambaye alikuwa akiishi umbali wa yadi 800 tu kutoka katika chuo maalumu cha kijeshi. Wachambuzi wanasema ushahidi wa kimazingira unaweza kuthibitisha kwamba Bin Laden alikuwa akiishi chini ya uangalizi wa Serikali ya Pakistani.
Rais Asif Ali Zardari alitoa utetezi kwa serikali yake jana akisema kuuawa kwa Bin Laden katika ardhi ya nchi yake si kigezo cha kushindwa katika mapambano ya serikali yake dhidi ya ugaidi. Katika safu ya maoni aliyoitoa kupitia Gazeti la Washington Post, Zardari alisema nchi yake “Ni moja wa waathirika wakubwa wa ugaidi duniani.”
Kwa mara ya kwanza, Zardari alieleza kwamba vikosi vyake vya usalama havikushirikishwa katika oparesheni hiyo lakini hakutoa maelezo ya kina kuhusu namna kiongozi huyo alivyoishi kwa amani jirani kabisa na Islamabad.
“Hakuwahi kutarajia kuwa atakuwapo katika eneo lolote, lakini sasa ameondoka.
Japokuwa matukio ya Jumapili hayakuwa ya ushirikiano wa pamoja, ushirikiano wa miongo kadhaa baina ya Marekani na Pakistani umechangia kummaliza Osama Bin Laden ambaye alikuwa tishio kwa ulimwengu wa wastaarabu,” alisema.
Maziko yaibua maswali mengi
Japokuwa sehemu kubwa ya dunia imekuwa katika shamrashamra za kifo cha kiongozi huyo wa al-Qaeda, maswali mengi yamekuwa yakiibuliwa kuhusu hatua hiyo, huku kukiwa hakuna taarifa zozote za kutolewa kwa picha zake baada ya kuuawa.
Hatua hiyo inaibua maswali mengi hasa kwa wapinzani wa Rais Obama, iwapo kweli Bin Laden ndiye aliyeuawa au ni hadaa.Hata hivyo, maofisa wa Marekani wamedai kwamba wana uhakika wa asilimia 99.9 kwamba waliyemuua ni kiongozi huyo wa al-Qaeda huku Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon yakieleza kwamba mwili wake ulizikwa kwa kufuata taratibu zote za Kiislamu ikiwamo kuoshwa kabla ya kupelekwa kwenye maji ya bahari ya Kaskazini mwa Uarabuni.
Maofisa wa Marekani walisema wamechukua hatua ya kuutupa baharini ili kuzuia kuwapo kwa kumbukumbu ya sehemu ya kaburi la kiongozi huyo wa al-Qaeda ambayo inaweza kutumika kama sehemu ya kumbukumbu kwa wafuasi wake.
Walisema pia ingekuwa vigumu kupata nchi yoyote ambayo ingekubali kupokea mwili wake kwa kipindi hicho kifupi wakisema sheria za Kiislamu zinaagiza mwili wa aliyeuawa uzikwe ndani ya saa 24 tangu kifo chake.
Rais Barack Obama na maofisa wa ngazi za juu wa Ikulu ya Marekani, jana kutwa nzima walikuwa wakijadili juu ya kuuonyesha hadharani mkanda wa picha za video zinazoonyesha maziko hayo.Maofisa hao hawakudhihirisha eneo halisi la bahari hiyo ambako wanajeshi waliubeba na kisha kuutumbukiza.
Lakini maofisa wa makao makuu ya jeshi la Marekani walisema kuwa mazishi hayo yalirekodiwa katika picha za video na zile za kawaida na pengine yataonyesha hadharani hivi karibuni.
Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Ugaidi cha Ikulu ya Marekani, John Brennan aliwaeleza waandishi wa habari kuwa utawala wa nchi hiyo bado uko katika mjadala mkali juu ya kuzionyesha au kutozionyesha picha za tukio zima la Osama ili kuwaridhisha wenye shaka juu ya ukweli wake.
Masheikh wametabiri kisasi dhidi ya maeneo muhimu ya Marekani kutokana na namna Serikali ya Marekani ilivyoamua kuuzika mwili wa Osama.
No comments:
Post a Comment