Meli ya LCT SPICE ISLANDERS imebinuka na kuzama katika Bahari ya Hindi huko Pwani ya Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja ikielekea Pemba.
Pichani: Meli ya LCT Spice Islanders ikiwa imezama Pwani ya Nungwi.
Picha na mdau Ahmed Muhamed Ahmed wa Zanzinet
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Mh Issa Haji Ussi akithibitisha tukio hilo amesema ajali imetokea milango ya saa 8:30 za usiku wa kuamkia leo, na kuongezea kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba abiria 610 pamoja na mizigo.
Mh Ussi amesema meli hiyo iliyokuwa imeondoka katika Bandari ya Malindi Unguja ikiwa katika hali ya uzima, lakini katikati ya safari ikapata hitilafu na kusababisha kubiruka na hatimaye kuzama.
Hadi sasa haijaweza kufahamika idadi kamili ya watu waliofariki,lakini vyombo vya uokozi vimefika katika eneo la tukio kutoa msaada.
Naibu Waziri huyo amesema Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya usafiri vya binafsi vya boti ziendazo kasi zimekwenda eneo la tukio kutoa msaada unaohitajika, huku Jeshi la Polisi Tanzania limetuma Helikopta yake kwenye eneo la tukio.
Awali, amesema Mamlaka zinazohusika zilipata taarifa za kuzama kwa meli hiyo baada ya Meli ya Mv Jitihada inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuripoti kuzama kwa meli ya Spice Islanders ambayo ililazimika kukatisha safari yake kuelekea Kisiwani Pemba na kwenda kwenye tukio.
Serikali imesema taarifa zaidi zitakuwa zikitolewa na wananchi wameombwa kuwa watulivu.
No comments:
Post a Comment