Thursday, October 27, 2011

Gaddafi is NO MORE!!



Pichani juu ni Mwili wa aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, kabla ya kuzikwa.
Luqman Maloto na Intaneti
MAZISHI ya aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, yalitawaliwa na maajabu ya aina yake, kubwa zaidi likiwa ni kaburi alilozikwa kuwa na kina kirefu kupita kawaida.

Hata hivyo, haikuelezwa ni muda gani mwili wa Gaddafi ulizikwa lakini vyanzo mbalimbali vinaeleza maajabu ya mazishi hayo.

MOSI: Kaburi hilo lilichimbwa urefu wa futi 12. Baraza la Mpito la Libya (NTC) lilifanya makusudi ili kuwakomoa watu watakaotaka kuutafuta mwili wa kiongozi huyo.

PILI: Alizikwa wakati wa giza. Walifanya hivyo ili watu wasione. Lengo ni sehemu aliyozikwa ibaki kuwa siri.

TATU: Inadaiwa hakuoshwa kama sheria ya dini yake ya Kiislam inavyotaka, wala hakuhifadhiwa kwenye sanda.
NNE: Hakuna ndugu yeyote aliyehudhuria.

TANO: Hakukuwa na kiongozi wa kidini aliyeongoza mazishi. Wapiganaji wa NTC kwa muongozo wa mabosi wao, waliuchukua mwili wake na kuufukia.

AZIKWA JANGWANI
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kama lilivyopokea taarifa kutoka kwa maofisa wa NTC, jirani na Gaddafi alizikwa mwanaye aliyeuawa naye wakati wa mapambano, Mutassim.

BBC liliandika kuwa NTC ilieleza kwamba Gaddafi alizikwa jangwani kwa siri mno na hakuna alama yoyote ambayo imeachwa.

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa serikali ya Gaddafi, Libya, Abu Bakr Younis Jabr, ambaye aliuawa siku moja na bosi wake, alizikwa pia sehemu hiyo.

MWISHO MBAYA
Ulikuwa mwisho mbaya wa Kanali Gaddafi, kwani kabla hajazikwa, mwili wake ulikuwa umeshaharibika na kutoa wadudu.

Habari zinasema kuwa wananchi wa Libya, waliokuwa wanakwenda kuushuhudia mwili huo walilazimika kufunika pua zao kutokana na harufu kali.

Awali, kulikuwa na danadana kuhusu mazishi ya Gaddafi, ingawa mwishoni, Serikali ya Baraza la Mpito (NTC) ilitangaza kuukabidhi mwili wa mwanaharakati huyo wa Umoja wa Afrika kwa familia yake.

Watu wa kabila la kiongozi huyo wa zamani wa Libya, walidai wakabidhiwe mwili wa ndugu yao ili wauzike kwa heshima, lakini NTC, iliweka ngumu kwa madai kuwa ni lazima azikwe kwa siri kubwa.

NTC ilidai kwamba ni busara Gaddafi azikwe eneo la siri kwa sababu kaburi lake likijulikana, kuna watu watakuwa wanakwenda kumuabudu.

Waziri wa Mkuu wa Serikali ya NTC, Libya, Mahmoud Jibril alisema: “Ni jambo hatari sana kuuzika mwili wa Gaddafi sehemu inayojulikana. Kuna watu watakuwa wanakwenda kwenye kaburi lake kuabudu.

“Ni vema na salama mwili wake uzikwe eneo la siri. Jukumu la kuzika mwili wake lipo ndani ya NTC na tutauzika kwa siri kubwa.”

Hata hivyo, baada ya jumuiya za kimataifa kuingilia kati kwa kuilaani NTC na Nato kutokana na udhalilishaji walioufanya kwa mwili wa Gaddafi, baadaye Jibril alitangaza kuukabidhi mwili wa mfadhili mkuu huyo wa AU kwa familia yake.

Jumatatu jioni ya wiki hii, Jibril alisema: “Taratibu zinaandaliwa, mwili wa Gaddafi utakabidhiwa kwa familia yake ambayo ndiyo itasimamia mazishi, lakini hakutakuwa na maadhimisho kitaifa.”

Jumanne wiki hii (juzi), Waziri wa Habari wa Libya katika Serikali ya NTC, Mahmoud Shammam, alikwenda kwenye chumba ambacho kimetumika kuuhifadhi mwili wa Gaddafi lakini baada ya kuzidiwa na harufu, aliziba pua.

Shammam alikiri kuwa mwili umeharibika na kwamba ili kuepusha athari zaidi, inabidi uzikwe haraka.
Baadaye, NTC ilibadili uamuzi na kumzika kwa siri bila familia wala kiongozi yeyote wa kidini kuhusishwa.

Katibu Mkuu wa zamani wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) sasa Umoja wa Afrika (AU), Dk. Salim Ahmed Salim, alizungumza kupitia redio ya watu, Clouds FM na kulaani kila kitu alichotendewa Gaddafi.

Dk. Salim alisema, ni bora Gaddafi angeuawa kwenye mapambano lakini inasikitisha kwa sababu alikamatwa mzima kisha kuuawa kwa risasi.

Waziri Mkuu huyo mstaafu wa Tanzania, alilaani hata kitendo cha mwili wa kiongozi huyo kuachwa wazi kwa sababu kinapingana hata na sheria za Kiislam.

No comments: