Tuesday, December 20, 2011

CHAKULA NDIYO CHANZO CHA MARADHI YANAYOTUSUMBUA


CHAKULA ni dawa, lakini chaweza kuwa sumu pia. Katika makala yetu ya leo tunazungumzia namna ambavyo chakula kimekuwa chanzo cha maradhi mengi sugu yanayotusumbua binadamu hivi sasa.
Vijana wengi wanapoteza uhai wakiwa bado vijana, maradhi kama shinikizo la damu (presha), saratani, kiharusi, kisukari, magonjwa ya miguu na migongo, yamekuwa sawa na ni wimbo wa taifa.

Asilimia kubwa ya magonjwa yanayotusumbua, kama vile shinikizo la damu (Low and High Blood Pressure), Magonjwa ya moyo (Cardiovascular diseases), saratani (cancer), ambayo ndiyo mengi, yanatokana na vyakula tunavyokula kila siku au tunavyoacha kula kama inayotakiwa.

Ukiangalia katika muongozo wa vyakula (Food Guide Pyramid) ambao unatuonesha kundi lipi la vyakula tunatakiwa kula kwa wingi na kundi lipi tunatakiwa kula kidogo, katika maisha halisi tuliyonayo, utaona muongozo huo umegeuzwa, miguu juu, kichwa chini.

Hii ina maana kwamba vyakula ambavyo tunapaswa kula kwa wingi tunakula kidogo au kwa nadra sana na vyakula ambavyo tunapaswa kula kidogo na kwa nadra ndiyo tunakula kwa wingi na karibu kila siku.

VYAKULA TUNAVYOTAKIWA KUVILA KWA WINGI
Katika muongozo huo wa vyakula, ambao unatambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), unaorodhesha vyakula vitokanavyo na nafaka kama vile mchele, ngano, mahindi, uwele, mtama, n.k, kama vyakula tunavyotakiwa kuvipa kipaumbele katika milo yetu ya kila siku kwa kuvila kwa wingi.

Tukizungumzia maisha ya Kitanzania, vyakula maarufu vitokanavyo na nafaka hizo, ambavyo vinatumiwa na familia nyingi ni ugali, wali, mikate, tambi, makande, uji, n.k. Uzoefu unaonesha kuwa familia nyingi za Kitanzania zinatumia ugali, wali na mikate, uji karibu kila siku katika milo yao, lakini tambi, kande na vingine vya jamii hiyo, huliwa mara moja moja.

TATIZO LIKO WAPI?
Ikiwa familia nyingi zinakula ugali, wali, mikate na maharage kila siku kama muongozo wa vyakula unavyotukata, tatizo liko wapi? Tatizo lipo, tena kubwa na familia nyingi zinaathirika nalo kwa kukosa elimu ya kutosha kuhusu vyakula wanavyokula. Kweli wanakula ugali, mikate, lakini VIMECHAKACHULIWA!

UGALI
Familia nyingi zinapopika ugali zinatumia unga mweupe, wenyewe wanaita sembe safi nyeupe, wakiamini kwamba huo ndiyo unga bora wakati siyo kweli.
Ili upate faida ya nafaka kwa kula ugali, ni lazima iwe nafaka ambayo haijaondolewa viini lishe vyake na ili vipatikane viini lishe hivyo, mahindi hayatakiwi kukobolewa bali yanatakiwa kusafishwa na kusagwa hivyohivyo.
Halikadhalika mtama na uwele.

Mahindi yaliyosagwa bila kukobolewa ndiyo yanayotoa unga safi na bora kiafya, unga huo ndiyo unaojulikana kama dona.
Kwa kutumia unga huo, iwe kwa kupika ugali au uji, utakuwa umepata faida ya kula vyakula vitokanavyo na nafaka kama inavyoagizwa kwenye muongozo wa vyakula. Ulaji wa ugali ama uji uliotokana na sembe nyeupe ni sawa na kula chakula kilichochakachuliwa!

MIKATE
Kama ilivyo kwenye ugali, tatizo hilo lipo pia kwenye mikate inayotumiwa na familia nyingi mijini karibu kila siku. Mikate inayoliwa na watu wengi ni hii inayotengenezwa kutokana na nafaka ya ngano, lakini kwa bahati mbaya nayo huwa imechakachuliwa na kukosa faida ya ngano kiafya.

Mkate unaopendwa na kuliwa sana ni mkate mweupe, huu hutengenezawa kutokana na ngano iliyokobolewa na kwa maana hiyo kiafya hauna ubora, kwa sababu viini lishe vyake vimeondolewa na mbaya zaidi hutiwa sukari kunogesha ladha.
Licha ya kasoro hiyo, mkate mweupe umeendelea kuwa chaguo la kwanza na mlo wa kwanza katika familia nyingi duniani.

Ingawa kuna aina mbili ya mikate, lakini aina moja ndiyo inayopendwa na watu wengi zaidi kuliko aina nyingine ambayo hutengenezwa kutokana na ngano isiyokobolewa, aina hii huitwa mkate mweusi au ‘brown bread’

No comments: