Na Joseph Ngilisho, Arusha
USHIRIKINA umeibuka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani Arusha, ambapo
askari wake wa kike aliye kwenye kitengo cha usalama barabarani
(Trafiki) mwenye cheo cha koplo (Jina tunalihifadhi) ametuhumiwa
kumchukua msichana ili amfanye msukule nyumbani kwake, Kijenge.
Shutuma hizo nzito, zimebainishwa na Johari Abdallah (20) (pichani),
mkazi wa Kijenge jijini hapa ambaye alidai kunusurika kuchukuliwa
msukule na askari huyo baada ya kufanikiwa kumwingiza nyumbani kwake
kimiujiza na kuishi naye kwa muda wa siku tano bila msichana huyo
kujijua. Akisimulia jinsi alivyokumbwa na mkasa huo, Johari ambaye
ni yatima na anaishi na mlezi wake akiwa na mtoto mchanga, alisema kuwa
trafiki huyo amekuwa akishirikiana na mama mmoja ambaye ni rafiki yake
na ndiye aliyemfuata na kumchukua kimiujiza. “Mama huyo alinifuata
nyumbani na kuniomba nimsindikize mjini lakini tulipofika kwenye
makutano ya barabara aliniambia nisimame na nifumbe macho, baada ya hapo
akaniwekea kiganja chake usoni,” alidai msichana huyo alipokuwa
akiwasimulia viongozi wa serikali ya mtaa wa Kijenge huku akitokwa
machozi.
Johari alidai kuwa baadaye alimwambia afumbue macho na atazame mbele
yake, ambapo alimwona askari mmoja wa usalama barabarani wa kiume ambaye
hakumtambua akiwa amesimama katikati ya barabara na akaamriwa amfuate.
“Huyo mama aliniambia nimfuate huyo askari ambaye alinipa shilingi
2000 na nilipoipokea, sikujielewa mpaka nikajikuta nipo kwenye nyumba
moja ambapo niliambiwa nioge kwa kuwa nilikuwa mchafu na nikaingizwa
ndani. Humo nilikuwa nasikia sauti za watoto wadogo lakini walikuwa
hawaonekani.
“Askari huyo alikuja akanifunika kitambaa kichafu ndipo nilipoona
miujiza ya ajabu, wakiwemo watoto watano wenye umri wa miaka kati ya
mmoja hadi mmoja na nusu wa jinsi tofauti. Baadaye nikamuona msichana
(jina tunalo) ambaye alipotea akiwa na umri wa miaka 12, nilipewa jukumu
la kulea watoto hao,” alidai Johari.
Akisimulia jinsi alivyoponyoka alidai alielekezwa kwenda kumchukua
mtoto wa jirani yao na wake lakini alipofika kwao alianza kukabana na
mfanyakazi wao aitwae Rozaria Natael ili amuue na amchukue mtoto.
Akizungumza ofisini hapo Natael alikiri kukabwa na msichana huyo
lakini walimkamata kwa nguvu na wengine kuanza kumwombea kabla ya
kumfikisha katika ofisi ya serikali ya mtaa wa Kijenge.
Kwa upande wa askari huyo alipohojiwa kuhusiana na tuhuma hizo
alikiri kumtambua Johari na kueleza kuwa hakutaka kumfanya msukule na
kwamba yeye anasingiziwa kwa sababu za watu binafsi.
Naye mama aliyedaiwa kushirikiana na askari huyo katika mambo ya
kishirikina alikiri kumfahamu mtuhumiwa afande na kudai kuwa ni ndugu
yake ila alikataa kuzungumzia masuala ya ushirikina. Natael alisema
kuwa Johari alitoweka nyumbani katika mazingira ya kutatanisha tangu
Machi 26 na kupatikana Machi 30, mwaka huu baada ya kumtafuta kwa muda
mrefu sanjari na kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Kijenge na Kituo
Kikuu cha Kati bila mafanikio. |
No comments:
Post a Comment