Stori: Haruni Sanchawa na Erick Evarist wa GPL
Bastola ambayo inadaiwa ilikuwa ikitumiwa kihalali na staa wa filamu
barani Afrika, Steven Charles Kanumba, inasakwa na Jeshi la Polisi
Tanzania.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Dar es Salaam, ACP Charles
Kenyela amesema kuwa anafuatilia kumbukumbu za silaha hiyo, kwani
haijarejeshwa kwenye jeshi lake.
Kenyela alisema juzi kuwa anafuatilia juu ya umiliki huo na baada ya
hapo, jeshi la polisi litawahoji ndugu wa msanii huyo kuhusu kurejesha
bastola hiyo jeshini.
“Bastola ni mali ya serikali. Kuna hatua ambazo hufuata mpaka mtu
aruhusiwe kumiliki bastola,” alisema Kenyela na kuongeza:“Endapo mmiliki
halali wa silaha hiyo atafariki dunia, ndugu zake lazima waikabidhi kwa
jeshi la polisi na baada ya hapo, kama kuna ndugu anataka aimiliki
tena, inabidi afanye maombi upya na atakapokidhi vigezo ndiyo
ataruhusiwa. “Kutokana na hali hiyo, bastola ya Kanumba lazima irudi
kwetu haraka na kama kuna ndugu yake yeyote anataka kuimiliki, itabidi
awasilishe maombi.” Kenyela aliongeza kuwa hivi sasa anafuatilia
kumbukumbu za jeshi la polisi ili awe na uhakika kama kweli msanii huyo
alikuwa anamiliki silaha hiyo. “Tukithibitisha tutawahoji ndugu zake
pamoja na wengine wanaohusika ili tuwe na taarifa za hiyo silaha. Ila
kwa sasa tunafanyia kazi taarifa hizi kwa kupitia kumbukumbu za jeshi,”
alisema. Kenyela alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa na mwandishi
wetu kama jeshi lake limeshapokea bastola ambayo alikuwa anaitumia
Kanumba enzi za uhai wake.
NDUGU WANASEMAJE? Mama mzazi wa Kanumba, Flora
Mtegoa, alipoulizwa na paparazi wetu kuhusu bastola inayodaiwa kutumiwa
na mwanaye alipokuwa hai, alikuwa na haya ya kujibu: “Sijaiona hiyo bastola humu ndani tangu nimefika hapa. Sijui ipo wapi na sijui kama kweli Kanumba alikuwa anamiliki hiyo silaha. “Najua
sheria za silaha hiyo, kwa hiyo ingekuwepo ningeiwasilisha polisi
haraka. Baba yangu alikuwa na silaha hiyo, alipofariki dunia
tuliikabidhi kwa jeshi la polisi.”
NANI ANAJUA ILIPO? Taarifa zinaonesha kuwa mdogo
wa Kanumba, Seth Bosco alikuwa karibu zaidi na marehemu lakini kwa
sababu umiliki wa silaha hiyo ni siri, siyo rahisi kujua ilipo. Mtu
mwingine ambaye alikuwa karibu na marehemu mpaka nyakati za mwisho za
uhai wake, kama ripoti zinavyoonesha ni muigizaji Elizabeth Michael
‘Lulu’ (pichani), ingawa naye inawezekana hajui kutokana na unyeti wa
silaha yenyewe.
BASTOLA NA KANUMBA Akiwa hai, Kanumba aliwahi kuripotiwa mara kadhaa kumiliki silaha hiyo, japo haikufafanuliwa kama ni kihalali au batili. Kanumba
aliripotiwa kwa mara ya kwanza kumiliki bastola miaka minne iliyopita,
akidaiwa kuichomoa baada ya kuvamiwa na kundi la watu aliohisi wanataka
kumteka. Licha ya stori hiyo kuandikwa gazetini na nyingine ambazo
zilimhusisha na umiliki wa bastola, bado Kanumba hakuwahi kufafanua
chochote kuhusu silaha hiyo.
IPO WAPI? Je, aliiacha sehemu ambayo hakuna mtu anayeweza kupafikia? Aliirejesha kabla mauti hayajamkuta ndiyo maana haionekani? Je, Kuna mtu aliiwahi baada ya kifo chake kwa kuona ni dili? Kanumba alifariki dunia Aprili 7 na kuzikwa Aprili 10, 2012 kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam. |
No comments:
Post a Comment