Wednesday, April 4, 2012

MAHABUSU MWINGINE ALIYETOROKA BAADA YA KUCHIMBA UKUTA AKAMATWA.

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Vasco Lwenje (28) mkazi wa Songwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoani Mbeya mmoja wa wahabusu wanne waliotoroka kwa kuchimba ukuta wa Kituo Kuu cha Polisi cha Kati Machi 22 mwaka huu amekamatwa.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa Advocate Nyombi, amesema mtuhumiwa amekamatwa katika nyumba ya Bwana Reuben Sanga mkazi wa Iwindi nje kidogo ya mji mdogo wa Mbalizi, majira ya saa nne usiku Machi 29 mwaka huu alikoomba hifadhi.

Amesema kupatikana kwa Lwenje ni juhudi za jeshi lake pamoja na ushirikiano wa kiintelejinsia baina ya jeshi hilo na wananchi hadi kufanikisha kukamatwa mahabusu watatu kati ya wanne waliotoroka kwa muda wa juma moja tu.

Kamanda Nyombi ameongeza kuwa amesalia mahabusu mmoja aliyemtaja kwa jina la Jonas Jackson (28), mkazi wa Tunduma na mwenyeji wa Mbozi ambapo pamoja na Lwenje walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji.

Aidha amesema kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa Jonas Jackson, jeshi lake litatoa zawadi nono kwani pamoja na wengine waliorejeshwa mahabusu ni watu hatari sana.

Lwenje alikuwa kwenye nyumba ya Mzee Sanga ambako alipewa hifadhi na mzee huyo ambapo waliwahi kukutana gerezani, alipokuwa kifungoni kabla ya kuachiwa.

Hata hivyo Kamanda Nyombi amebainisha kuwa kukamatwa kwa Lwenje kunafanya jumla ya waliokamatwa kufikia watu watatu na kwamba mbali ya makosa ya mauaji watakabiliwa na kosa la kutoroka chini ya ulinzi wa dola.

No comments: