ZAIDI ya wanaume 6, 500 waliokuwa wakiishi bila kutahiriwa katika
Wilaya za Nzega na Igunga mkoani Tabora, sasa wametahiriwa chini ya
mpango maalumu unaolenga katika kupunguza maambukizi ya virusi vya
Ukimwi.Meneja wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la JHPIEGO Tanzania,
Tawi la Mkoa wa Tabora, Simyoni Nyandenda, alisema hayo ni mafanikio
makubwa mno katika utoaji wa huduma hizo mkoani humo.Kwa mujibu wa
Nyandenda, Mkoa wa Tabora, una vituo vinne vinavyotoa huduma za bure za
kutahiri wanaume wanaoishi bila kutahiriwa.Katika Wilaya ya Nzega, vituo
hivyo viko katika hospitali ya wilaya na Hospital ya Missioni ya Ndala,
wakati katika Wilaya ya Igunga, vituo viko katika Hospitali ya Igulubi
na hospitali ya wilaya.Alisema idadi hiyo ya watu waliotahiriwa, imevuka
malengo ya shirika lake na Hospitali ya Mkoa wa Tabora, ya kuwafanyia
tohara wanaume 5,000 katika kipindi cha wiki tatu.Meneja huyo alisema
zoezi hilo katika wilaya hizo, limesukumwa na kasi kubwa ya maambukizi
ya virusi miongoni mwa wananchi.Alisema takwimu zinaonyesha kuwa
maambukizi ya virusi katika wilaya hizo mbili za Mkoa wa Tabora, sasa
yamefikia asilimia 6.4, kiwango ambacho alisema ni kikubwa.Nyandenda
alisema kasi ya maambukizi katika wilaya ya Nzega, inachangiwa na
mwingiliano mkubwa wa watu unatokana na migodi na mji kuwa katika njia
panda.Alisema kwa upande wake, Wilaya ya Igunga, maambukizi yanachangiwa
na mji kuwa barabarani na wimbi kubwa la wachimbaji wadogo wadogo wa
madini.Alisema watu ambao hawajatahiriwa, wako katika hatari kubwa ya
kuambukizwa virusi vya Ukimwi, ikilinganishwa na waliotahiriwa.Alitoa
wito kwa wanawake, kuwahimiza wanaume ili waende wakapate huduma hizo,
ili pamoja na mambo mengine, kuwawezesha wanawake kuepuka kupata kansa
ya shingo ya uzazi. |
No comments:
Post a Comment