Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi kavu (SUMATRA) imetangaza kuanzishwa safari mpya za daladala jijini Dar es Salaam.
Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki Bw. Walukani Luhamba, alisema jana katika mahojiano na Nipashe kuwa kuanzia sasa kutakuwa na daladala zinazosafiri kati ya Kimara na Buguruni kupitia barabara za Morogoro na Mandela.
Kwa mujibu wa Bw. Luhamba, njia nyingine mpya ya daladala ni ya kutoka Ukonga hadi Stesheni kupitia barabara za Nyerere na Uhuru.
Kadhalika alisema kutakuwa na usafiri baina ya Mwananyamala na Mabibo.
Aliongeza kuwa mfumo huo mpya utahusisha njia ndefu, fupi na zile za kati na kwamba nyongeza hiyo imezifanya ruti za daladala jijini kufikia 130.
Alisema lengo la kuongeza njia mpya za daladala ni kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji.
Bw. Luhamba aliendelea kuzitaja njia hizo kuwa ni magari yatakayofanya safari kutoka Ukonga hadi Mbagala kupitia barabara ya Nyerere, kutoka Tegeta hadi Kawe kupitia barabara ya Bagamoyo na Kimara hadi Kawe kwa kupitia barabara ya Morogoro na Sam Nujoma.
Njia nyingine ni kutoka Kawe hadi Buguruni kupitia barabara ya Kawawa.
Bw. Luhamba alisema zoezi hilo linakwenda pamoja na usajili wa magari madogo ya abiria Hiace maarufu kama \'vipanya\' ambayo yatakuwa na ruti fupi fupi.
Alisema magari yatakayosajiliwa katika njia ndefu ni yale mabasi makubwa yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 25 ambayo yatafika hadi pembezoni mwa jiji.
Alisema kuanzia sasa ofisi yake itaanza kudhibiti madereva wenye tabia ya kukatisha ruti.
Bw. Luhamba pia amewapiga marufuku madereva wanaoanza kujipandishia nauli kiholela na badala yake alitaka wafuate taratibu zilizowekwa kisheria
Alivitaja viwango vya nauli vinavyopasa kutumika kwa sasa kuwa ni Shilingi 250 kwa umbali wa kuanzia kilometa 0 hadi 10, Sh. 300 kwa umbali wa kuanzia kilometa 11 hadi 15 na Sh. 350 kwa umbali wa kuanzia kilometa 16 hadi 20.
Bw. Luhamba alisema njia hizo mpya zitaanza kufanyakazi kuanzia wiki ijayo na tayari baadhi ya magari yameshasajiliwa kwa kutumia njia hizo.
No comments:
Post a Comment