Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Novemba 13, 2008, amewaongoza mamia ya wananchi kumzika aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Vijijini, Ndugu Richard Said Nyaulawa.
Mazishi hayo yamefanyika nyumbani kwa Mbunge huyo katika kijiji cha Inyala, kiasi cha kilomita 25 kutoka mjini Mbeya kwenye barabara kuu inayoekelea Iringa.
Rais Kikwete na mamia ya waombolezaji hao wameshuhudia mwili wa marehemu ukiteremshwa kaburini kiasi cha saa 9.20 mchana katika shamba lake kijijini hapo.
Mbali na Rais Kikwete, ambaye amefuatana na mke wake, Mama Salma Kikwete, mazishi hayo ya Ndugu Nyaulawa yamehudhuriwa na mawaziri, wabunge, wafanyabiashara, viongozi wa vyombo vya habari na mamia ya wananchi.
Rais Kikwete amewasili kwenye uwanja wa ndege wa mjini Mbeya kiasi cha saa nane mchana na kwenda moja kwa moja kijijini Inyala kwa ajili ya mazishi ya Mbunge huyo ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumatatu ya wiki hii nyumbani kwake mjini Dar Es Salaam kwa ugonjwa wa kansa ya ini.
Kabla ya mwili wa marehemu kuteremshwa kaburini waombolezaji wameshuhudia salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi mbali mbali akiwamo Mkurugenzi mwenza wa Kampuni ya Business Times Limited, Rashid Mbughuni, ambaye ameelezea ukaribu wa miaka mingi wa familia za akina Mbughuni na Nyaulawa.
Mbali na ubunge, Ndugu Nyaulawa alikuwa pia Mkurugenzi katika kampuni hiyo ya Business Times Limited.
Wengine waliozungumza kwenye mazishi hayo ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Ndugu Mullah; Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Ndugu John Mwakipesile; Naibu Spika wa Bunge, Ndugu Anna Makinda; Naibu Katibu Mkuu wa CCM, George Mkuchika; mwakilishi wa wabunge wa upinzani, Ndugu Mwadini Abbas Jecha, mwakilishi wa wabunge wa CCM, Dk. Mahenge.
Mara baada ya kukamilika kwa shughuli za mazishi hayo, Rais Kikwete ameondoka Mbeya kurejea Dar Es Salaam.
No comments:
Post a Comment