This blog is for critical thinkers, people with open mind, ready to accept criticisms and work on them. Sharing the know-how, skills and experiences of Life and Technology at large. You are warmly welcome!! ---------------------------------------------------- Blogu hii ni kwa ajili ya wenye fikra makini wapendao kupokea na kufanyia kazi ukosoaji. Walio na mtazamo chanya tena mpana katika kushirikishana maarifa, ujuzi na uzoefu wa maisha na teknolojia kwa ujumla wake. Karibuni sana !!!
Tuesday, May 19, 2009
Kinachofanywa na majaji ‘Bongo Star Search’ ni udhalilishaji wa kutisha
BILA kumung’unya wala kutafuna maneno, nathubutu kusema nimesikitishwa na wale wanaoitwa wataalamu wa kusaka vipaji vya waimbaji. Kwangu, watu hawa si wataalamu bali wababaishaji ambao wanajiona wao ndio watu na wengine hawastahiki heshima inayojali utu wa mtu.
Nimeshangazwa na kampuni ya Vodacom ambayo inadhamini kampeni hii kwa kuruhusu watu hawa kutumia udhamini wao kuwatukana Watanzania na kuonyesha ulimwengu kuwa maskini hana haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, nimehuzunishwa na wana habari wa kituo cha ITV kwa jinsi walivyoweka taaluma na heshima ya Watanzania kando na kutojali maadili na kuwaruhusu hawa wanaoitwa ma-DJ waliobobea kuwadhalilisha, kuwanyanyasa na hata kuwatukana vijana wanaosaka ajira kupitia usanii wa kuimba.
pichani kulia ni mtayarishaji wa muziki ndani ya studio za bongo records ambaye pia ni moja ya majaji ndani ya shindano la bongo star search
Ni matumaini yangu Baraza la Habari Tanzania na vikundi vya kutetea haki za binaadamu vitaangalia hivi vibwagizo vya matusi vya hawa ma DJ kwamba havirudiwi tena; na kuionya ITV kuachana na kile unachoweza kukiita uhuni uliobobea unaoonekana katika huo unaoitwa msako wa kuibua vipaji.
Kwa wale ambao hawakuona kipindi hiki cha safari iliyojaa mbwembwe za Ma-DJ watatu wanaume wawili na mwanamke mmoja, ya kusaka vipaji vya waimbaji Tabora na Kigoma, natoa maelezo ya muhtasari ya kile kilichoonyeshwa:
1. Kijana wa miaka kama 22 hivi akiwa amevalia nguo ambazo aliamini zingeliwavutia hao ‘majaji’ anaingia kwenye ukumbi. Wanaumuangalia kama kinyago na mmoja anamwambia vazi lako halituvutii.
“Tumetumia fedha nyingi kuja hapa na wewe unafanya utani; haya imba!”
Kijana anajitahidi kuimba na baada ya sekunde zisizozidi 10, wanamsimamisha na mmoja wao akisema huku ‘majaji’ wengine wakimcheka: “Katafute kazi nyingine, hujui kuimba. Unaona mlango ule..toka hapa.”
2. Dada mmoja alipongia tu aliambiwa haya imba. Alipoanza tu walimsimamisha na DJ mmoja kumwambia: “Nani kamwambia anajua kuimba?” mwingine anamwambia rudi nyumbani ufanye kazi ya kuzalisha watoto.
3. Mwingine alipoonekana sauti yake haivutii aliulizwa anafanya kazi gani. Alijibu kwa upole kuwa anapata riziki yake kwa kutia rangi viatu. Alipokaa kimya alisukumiwa makombora ya matusi na kuambiwa anaonekana kuwa ni kibaka na kilichofuata ni kuonyeshwa mlango wa kutokea.
Mengine mazito zaidi siwezi kuyaorodhesha, lakini kwa ujumla, kipindi hiki kilikuwa kielelezo cha kuvunja vijana moyo na heshima. Fikiria watoto, ndugu na jamaa za hawa vijana wataonaje wakishaona kipindi kile kilichokuwa hakina utu, nidhamu wala maadili.
Binafsi, nilipoona udhalilishaji wa aina ile dhidi ya vijana wenye nia ya kutaka kuwa wasanii (hata kama hawajui), nilijisikia kichefuchefu na kutamani hata kuzima runinga. Lakini nikaona hapana, ngoja nijiridhishe kwa kushuhudia vijana kadhaa watakachofanyia, kweli kabisa, ilichokishuhudia na kukiona kwa macho, kilitosha kupata jawabu kuwa, wanachofanya si kuibua vipaji vya wasanii, bali kuua vipaji.
Sidhani kijana aliyethubutu kujitokeza kuonyesha nia yake ya kutaka kuwa msanii na kuishia kuonyeshwa mlango na kuelezwa akazae watoto kama atakuwa na hamu ya kutaka kujiendeleza katika fani ya usanii.
Hii inatokana na ukweli kuwa, wapo wanaotaka kuimba, lakini hawana sifa hizo na baadhi yao wanazo, lakini hawajui njia za kupita. Aidha, kama hawa ma-DJ walikuwa wanaona kijana hana kipaji, kuna lugha ya kistaarabu ya kumweka kando na siyo kudhalilishana kama ambavyo wanafanya.
Hivyo, mmoja wa ‘majaji’ hawa angeliambiwa maneno ya kashfa kama yale waliyowatupia vijana wa Tabora na Kigoma angelihisi vipi? Hapana ubishi, kuwa vijana wengi wa Tanzania, kama walivyo wazee wao ni maskini.
Lakini, Watanzania ni maskini wa kipato na sio utu, heshima, ukarimu na hisani na ndio maana maelfu kwa maelfu ya watu huhama nchi zao na kuja kuishi hapa sio tu kwa vile ni nchi ya amani, bali watu wake ni watulivu na wenye kuthamini ubinaadamu.
Ni lazima vyombo vyetu vya habari na kampuni za biashara kama Vodacom, ziache kudhalilisha watu.
Unyanyasaji sio biashara nzuri na hautakiwi na Watanzania. Wahariri wa ITV na vituo vingine vya radio, televisheni na magazeti waelewe wajibu wao na maadili ya taaluma hii ya uandishi wa habari. Maadili ya taaluma ya habari yanalazimisha kuheshimu utu, ikiwa ni pamoja na watu maskini, kama wale vijana wa Tabora na Kigoma.
Kosa limefanyika, ni vizuri lisirudiwe. Lakini suala muhimu hapa kwa hawa ma-DJ, ITV na Vodacom kuwaomba radhi na hata kuwalipa fidia wale vijana waliodhalilishwa na kuwaambia Watanzania samahani.
Kuomba radhi ni ustaarabu na anayefanya kosa na kukataa kosa lake au kuomba radhi, basi huwa si mstaarabu. Kwa ma-DJ ni vizuri wakaelewa kwamba, wanachoweza kuchezea ni ala za muziki na sauti zao wakiwa juu na nje ya jukwaa, lakini sio maisha na heshima ya Watanzania wakiwemo vijana wa kimaskini kama wa Tabora na Kigoma.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment