JK akisalimiana na baadhi ya viongozi waliofika kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyere jijini Dar es salaam kumpokea wakati aliporejea nchini akitoka Marekani leo.Wa pili kushoto ni Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein na kushoto ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
JK amerejea nyumbani mchana wa leo- Jumatatu, Mei 25, 2009- baada ya ziara yenye mafanikio ya kikazi ya siku nane katika Marekani.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar Es Salaam, Rais Kikwete amelakiwa na Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na viongozi wengine wa Serikali.
JK na ujumbe wake alianzia ziara yake mjini San Francisco ambako alikutana na kuzungumza na Rais wa Chuo Kikuu maarufu cha Stanford, na kutembelea Silicon Valley, eneo maarufu zaidi duniani kwa shughuli za teknolojia ya kompyuta duniani.
Miongoni mwa makampuni makubwa ambayo Rais alitembelea katika eneo hilo ni CISCO, Google na IMB ambako alisisitiza shabaha ya Serikali yake ya kuifanya teknolojia ya kompyuta moja ya ngome kuu za maendeleo ya Tanzania.
Baadaye Rais alikwenda mjini Los Angeles ambako miongoni mwa mambo mengine alitunukiwa tuzo maalum la maendeleo ya afya na taasisi ya madaktari ya US Doctors for Africa.Rais Kikwete alikuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kupewa tuzo hilo kwa sababu ya mchango wake katika maendeleo ya huduma za afya katika Tanzania na Afrika.
Kilele cha ziara hiyo kilikuwa mjini Washington D.C. ambako alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Marekani, Barack Obama na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mama Hillary Clinton.
Mazungumzo kati ya JK na Rais Obama yalichukua muda wa saa moja katika Ofisi ya Rais wa Marekani ya Oval Office, na Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kualikwa ili kumtembelea na kufanya mazungumzo na Obama, tokea kiongozi huyo achukue uongozi wa Marekani Januari, mwaka huu.
Mjini Washington, JK pia alikutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Dominique Strauss Kahn, na viongozi wa taasisi nyingine muhimu kwa maendeleo ya Tanzania ikiwemo MCC na USAID.
JK pia alitembelea hospitali maarufu ya kijeshi ya utafiti ya Marekani ya Walter Reed pamoja na makumbusho ya Taifa ya kijeshi hapo hapo Washington. Katika hospitali hiyo aliweza kujiuonea shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kitengo cha huduma kwa majeruhi wa kivita, na kitengo cha utafiti wa magonjwa.
No comments:
Post a Comment