Na Juddy Ngonyani, Sumbawanga-Gazeti la Mwananchi
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza amewataka wananchi wa kijiji cha Muze wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa kumuombea dua mbaya aliyekuwa mwalimu wa shule ya sekondari Mazoka aliyempa mimba mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo.
Mahiza alisema taarifa ya shule ilimsikitisha na baadhi ya matatizo yaliyoainishwa yatashughulikiwa na serikali.
" Na hili la huyu bazazi, aliyemkatisha masomo mwanafunzi ni lazima tumuombee dua ili asisimame daima,uume wake uache kufanya kazi" alisema.
Alisema mwalimu ndiye kioo cha jamii, lakini mwalimu anapomkatisha masomo mwanafunzi ni lazima achukuliwe hatua kali za kisheria na kinidhamu na kwamba kwa vile alitoroka dua limfuate huko aliko.
Awali akitoa taarifa ya shule hiyo mkuu wa shule hiyo Anicent Mpemba alisema katika kipindi cha miaka mitatu hadi hivi sasa wanafunzi wanne wa kike walikatishwa masomo yao kutokana na ujauzito.
Hata hivyo wanaume watatu walikamatwa kwa tuhuma za kutunga mimba hizo, lakini mwanaume wa nne alitoroka.
Mpemba alisema mwalimu huyo baada ya kupatikana na hatia alifanikiwa kutoroka kabla ya kukamatwa na juhudi za kumtafuta bado zinaendelea kwa lengo la kumfikisha katika vyombo vya sheria
No comments:
Post a Comment