Wednesday, December 8, 2010

Matembezi ya Hisani, kuchangia Elimu Arusha, Desemba 17

Na Arusha Mambo

Ofisi ya Mbunge ya Jimbo la Arusha Mjini imeanza kazi zake rasmi na kuipa ahadi ya Elimu kipaumbele ili kuhakikisha watoto kati ya mia tano hadi elfu moja wanawezeshwa kujiunga na Elimu ya Sekondari ifikapo Januari 2011.

Huu ni utekelezaji wa ahadi ya Mbunge wa Jimbo hilo Mheshimiwa Godbless Lema aliyoitoa wakati wa Kampeni, kuwa atashirikiana na wananchi wa Jimbo lake kupata fedha ili kulipa ada kwa watoto hao wasiokuwa na uwezo watakaokuwa wamefauli kujiunga na elimu ya Sekondari na wale wanaoendelea na masomo katika shule za Serekali.

Mheshimiwa Lema amesema, tayari Kamati ya Maendeleo ya Jimbo (THINK TANKERS) imeundwa ili kuanza mikakati ya kuandaa matembezi ya hisani yatakayofanyika tarehe 17/12/2010 kufanikisha kupata fedha kabla ya mwezi Januari ili ada hizo ziweze kulipwa.

Amesema uteuzi wa wajumbe wa kamati hiyo aliyoiteua umezingatia jinsia, elimu, vigezo vya uwajibikaji, kuheshimika mbele ya jamii, uwezo wa uelewa na uhamasishaji, michango ya wateuzi katika kazi za kijamii, uwezo wa kufikiri na sifa zao kwa Jamii bila kujali itikadi.

Kazi ya kwanza ya kamati hiyo ni kuunda na kusimamia kamati ndogo itakayosimamia Mfuko wa Elimu wa Jimbo na kuandaa mchakato wa uwazi wa upatikanaji wa watoto na kusimamia tukio la upatikanaji wa fedha.

Hata hivyo Mheshimiwa Lema ameomba wananchi wa Jimbo lake bila kujali itikadi wajitokeze kwa wingi siku hiyo na kutoa michango yao ya hali na mali bila kujali udogo au ukubwa wa vipato walivyonavyo ili kwa pamoja waweze kuijenga Arusha Mpya.

Amesema kabla ya tarehe 13 mwezi huu atakuwa ameshaiapisha kamati hiyo na siku hiyo ndipo wananchi, waandishi wa habari na wadau mbalimbali wa maendeleo watakapoelezwa mfumo wa uchangiaji, uchangiaji huo utakavyoendeshwa, jinsi ya kupata watoto wenye uhitaji pamoja na matembezi yenyewe yatakavyofanyika.

Aidha ameomba mshikamano toka kwa wananchi wa Jimbo la Arusha na wale wa jumuiya za kimataifa wanaoishi Arusha kujitokeza kuchangia maendeleo na kuleta mawazo yao yatakayoleta changamato za maendeleo katika jimbo hilo na amewasihi wananchi wa jimbo lake kuwa kuanzia sasa watu wajifunze kujali na kuwasaidia wahitaji wanaoishi nao.

Amesema vipaumbele vingingine vitakavyofanyiwa kazi haraka baada ya elimu ni miundombinu, afya ikiwemo usafi wa Jiji, watoto wanaoishi katika mazingira magumu ma upatikanaji rahisi wa huduma za kijamii.

Mheshimiwa Lema (Mb.) ameomba Makampuni, Taasisi mbalimbali zilizopo Arusha na Watanzania wote waliopo nje ya Tanzania wanaopenda kuchangia maendeleo katika Jimbo lake wajitokeze kusaidia maendeleo katika jimbo hilo ili kuweka historia ya maendeleo ya kweli kupitia Nguvu ya Umma.

No comments: