Tuesday, December 7, 2010

Njama hizi ni hatari

Na Luqman Maloto
Ujumbe mfupi wa maneno (SMS) unaohusishwa na mpango wa kijasusi wa kumuua Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Zuberi Kabwe (pichani), umenaswa na Uwazi.

Katika SMS hiyo, aliyeiandika alisisitiza kwamba Zitto atakufa kwa siri lakini kabla ya kutekeleza kifo chake, atanyang’anywa nyaraka zote alizonazo ambazo hazikufafanuliwa kwenye ujumbe.


SMS hiyo, iliyonaswa kwenye simu ya mmoja wa makada wa CHADEMA (jina tunalo), ametajwa kama mmoja wa watakaotekeleza mpango wa kumuua Zitto, inasomeka:

“Nawaarifu kwamba nipo Mara nimemaliza kukutana na viongozi wa Mwanza. Inaelekea hawakubaliani na hoja yetu ya kumfukuza Zitto, sasa nilikwisha kusema kwamba tuweke mkakati kwenye Media JF. Ni …, … na … (yanatajwa majina ya watu).”

SMS hiyo inaendelea: “Ni …, … na … (majina mengine ya makada wa CHADEMA) watatekeleza kazi tuliyowapa na … (anatajwa kiongozi wa CHADEMA) atawapa mtu wa kuwaongezea nguvu.”

Ujumbe huo hauishii hapo, unaendelea: “Kuweni makini, hakikisheni amewapa nyaraka zote alizonazo kabla ya kumuua, usiri unahitajika… atawasaidia kujua nyendo zake na hii tu ndiyo njia ya kukinusuru chama.”

Uchunguzi unaonesha kuwa SMS hiyo ilizunguka kwa watu kadhaa ambao wanadaiwa wapo kwenye mtandao ulioandaliwa kutekeleza mpango wa kukatisha maisha ya Zitto.

Gazeti hili limebaini kuwa mmoja wa wabunge wazoefu wa Viti Maalum (CHADEMA) alitumiwa kisha naye akaituma (kui-forward) kwa mwenzake ambaye ni memba mpya ndani ya bunge.

Gazeti hili lilifuatilia mnyororo wa SMS hiyo na kugundua kwamba wakati ujumbe ukizungushwa kwa wanaodaiwa wana mtandao, uliingia ‘kirusi’ kwa kumfikia mtu ambaye hakukubaliani na wazo la kumuua Zitto.

“Hapa hatari iliyopo ni kwamba kuna mtu ambaye hakubaliani na wazo la kumuua Zitto, ndiyo atakuwa amevujisha,” kilisema moja ya vyanzo vyetu.

Chanzo chetu kilisema kuwa mtu huyo baada ya kupata SMS hiyo, aliituma kwa mama yake Zitto, Shida Salum ambaye naye ‘aliifowadi’ kwa mwanaye.

Gazeti hili lilimpata Zitto na alikiri kupata SMS, ingawa alidai kuwa uchunguzi ndiyo utafanikisha kumnasa mhusika mkuu wa ujumbe huo.
Zitto, akijibu bila uchangamfu, alisema wakati mwingine anahisi kuna watu wanatumiwa ili kukivuruga CHADEMA.

“Nafsi yangu haisemi kama ni kweli. Inawezekana kuna watu wametuingilia, Mungu ndiye anajua,” alisema Zitto.
Alipoulizwa kuhusu kuripoti polisi, Zitto alijibu:

“Nikiripoti ni kwa ajili ya uchunguzi wa kipolisi tu. Sitaki kutoa kwenye vyombo vya habari, sihitaji mgogoro kwenye chama.”
Kwa upande wa Mama Zitto, alikiri kupata SMS hiyo na kueleza kwamba tayari amesharipoti kwenye vyombo vinavyohusika.
“Sitaki kuizungumzia hiyo SMS, inachunguzwa kipolisi,” alisema Mama Zitto.

Gazeti hili lilizungumza na Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA, Regia Mtema ambaye ni mmoja watu wanaodaiwa kutumiwa SMS hiyo ambaye alikiri.

Hata hivyo, Regia aliye pia Ofisa wa Oganaizesheni wa chama hicho alisema: “Hiyo SMS sijatumiwa mimi peke yangu, kila mtu makao makuu anayo.

“Nafikiri kuna watu wametengeneza lakini hakuna mpango wa kumuua na kwanini auawe?”
Baada ya kuzungumza hayo, simu ilikatika na alipopigiwa tena hakupokea mpaka tuliapoamua gazeti kwenda mitamboni.

Wakati Zitto akipuuza ufuatiliaji wa SMS hiyo, chanzo chetu kimoja ndani ya makao makuu ya CHADEMA, kilisema kuwa si vema kudharau vitu kwa sababu ujumbe huo una alama za hatari.

“Mimi sipendi sana kuzungumzia mambo ya marehemu Chacha Wangwe (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti CHADEMA), lakini naye kifo chake kilitokea akiwa na mvutano na viongozi wengine wa chama kama ilivyo kwa Zitto sasa,” kilisema chanzo chetu.

Mpango wa kumuua Zitto, inakuja baada ya matukio kadhaa ambayo yalikaribia kuondoa uhai wake, ikiwemo kuwekewa sumu kwenye maziwa.

Miaka minne iliyopita, Zitto alikunywa maziwa yenye sumu kwenye hoteli moja jijini Mwanza na kuokolewa na aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum (CCM), marehemu Amina Chifupa ambaye alimpigia simu na kumueleza asiendelee kunywa.

Hata hivyo, kutokana na wingi wa maziwa aliyokuwa amekunywa dakika chache baada ya kupokea simu ya Amina, aliishiwa nguvu na kukimbizwa kwenye hospitali moja jijini humo ambapo alipatiwa matibabu.

No comments: