Tuesday, February 22, 2011

Mmiliki Dowans utata mtupu

*Mbunge ataka akamatwe apigwe picha kwa nguvu
*Achanganya wananchi, wahoji maswali lukuki
*CTI wataka mitambo yake itaifishwe haraka

Na John Daniel-Gazeti la Majira

MBUNGE wa Ubungo Bw. John Mnyika ameitaka serikali kutumia vyombo vyake
vya dola kumtia mbaroni Bw. Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi, aliyejitaja kuwa ndiye mmiliki wa Kampuni ya Dowans Holdings SA na kampuni tanzu ya Dowans Tanzania Limited.

Mbunge huyo amesema serikali inapaswa kuchukua hatua hiyo kwa madai kuwa mtu huyo alishakana kuhusika na kampuni hiyo wakati alipohojiwa kuhusu uhusiano wake na Dowans.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bw. Mnyika kwa vyombo vya habari jana, Bw. Al Adawi anapaswa kutiwa mbaroni kwa kuwa ametii kile alichosema katika tamko lake la Februari 16, mwaka huu la kutaka mmiliki wa mtambo huo ajitokeze.

Alisema katika tamko hilo aliitaka serikali itaifishe mitambo ya Dowans na kuiwasha kama sehemu ya kupunguza makali ya mgawo wa umeme na kuwataka wamiliki wake popote walipo duniani kujitokeza hadharani iwapo wana sababu za kuepusha mitambo yao isitaifishwe.

"Nilitarajia mmiliki wa Dowans ambaye angejitokeza angekiri hadharani kama wamedanganywa na kampuni ya Richmond na vyombo vingine katika kuhamishiwa mkataba ili kuweka msingi muhimu wa majadiliano, lakini imekuwa tofauti.

"Kutokana na hilo naomba kutoa rai kwa vyombo vya dola vimkamate vimpige picha na kumuhoji Al Adawi kwa mujibu wa sheria ya uhujumu uchumi na sheria nyinginezo kutokana na maelezo tata yaliyotolewa mpaka sasa kuhusiana na kampuni ya Dowans," alisema Bw. Mnyika katika taarifa yake.

Alidai kuwa kilichomshangaza ni kuwa siku chache baada ya tamko lake Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja, alinukuliwa na gazeti moja Februari 18 mwaka huu kuwa serikali haitataifisha mitambo hiyo kwa kuwa hiyo siyo sera ya CCM.

"Ikumbukwe kwamba katika gazeti la Mwanahalisi toleo namba 128 la Machi 2009 Al Adawi alikanusha kuwa yeye sio mmiliki wa Dowans kama alivyonukuliwa katika Mahojiano na KLHN.

Kama amekuwa akikanusha kuwa si mmiliki lakini sasa amejitokeza kuwa ndiye mmiliki kuna kila sababu ya vyombo vya dola kumuhoji zaidi," alisisitiza Bw. Mnyika

Alitaka vyombo vya dola vimuhoji Bw. Al Adawi kuhusu utata wa kampuni ya Dowans Holdings SA ambayo kumbukumbu zake kamili hazipo Costa Rica inapoelezwa kusajiliwa na kuwa na ofisi zake.

"Kwa kuwa sasa wanaotajwa kuwa wamiliki wa Dowans wameanza kujitokeza ni muhimu pia wamiliki wa kampuni ya Portek Systems and Equipment PTE Ltd ambayo inatajwa kumiliki hisa takribani 40% kwenye Dowans wakatajwa na wakajitokeza," alisisitiza.

Alirejea ushauri wake wa kuitaka serikali kuitaifisha mitambo ya Dowans na kuchukua hatua stahiki dhidi ya ukiukwaji wa sheria uliyojitokeza ili kuepusha kasoro zingine kujitokeza katika hatua za dharura zinazokusudiwa kuchukuliwa hivi sasa.

"Kutaifisha mitambo ya Dowans sio kutekeleza sera ya chama chochote, ni kuzingatia maslahi ya taifa na kusimamia utawala wa sheria ikiwemo sheria ya uhujumu uchumi,"alisisitiza Bw.Mnyika katika taarifa yake.

Mbali na Bw. Mnyika, baadhi ya wasomaji wa gazeti walikerwa na kitendo cha mfanyabiashara huyo kukataa kupigwa picha ili Watanzania waweze kumuona, isijekuwa aliyejitokeza ni mtu mwingine asiyehusika.

"Biashara ni matangazo kama ilivyo siasa. Wafanyabiashara na wanasiasa ni watu wanaopenda kupigwa picha na kujitangaza Watanzania, Huyu Al Adawi ni mfanyabiashara wa namna gani asiyependa kupigwa picha na kuonekana? Sisi tuna walakini na biashara yake," alisema Bw. Jerome John, mkazi wa Kigilagila.

Mkazi mwingine wa Ilala ambaye hakutaka kutaja jina lake, alionesha hasira kwa wanahabari kwa kushindwa kumlazimisha Bw. Al Adawi kumpiga picha au kutunmia mbinu za kipaparazi kunasa picha yake ili iweze kuonekana.

Katika hatua nyingine, suala la Kampuni ya Dowans limezidi kuwachanganya wabunge baada ya watumiaji wakubwa wa umeme kuhoji Kamati ya Nishati na Madini, sababu za kushindwa kuishauri serikali kutaifisha mitambo ya kampuni hiyo haraka kunusuru taifa.

Pia kamati hiyo ya bunge imetakiwa kujibu iwapo nchi haikufanya makosa kuingia katika mkataba na Dowans wakati bunge liliazimia kusitishwa kwa mkataba wa Richmond baada ya kubaini mapungufu kadhaa.

Katika kikao kilichofanyika Ofisi ndogo za Bunge Dar es Salaam jana kati ya Kamati hiyo ya Bunge na viongozi wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Baraza la Biashara la Taifa (TNB) na Mfuko wa Sekta Binafsi (TPSF) wadau hao walitaka kamati hiyo kuchukua hatua za haraka kunusuru uchumi wa nchi.

Vyanzo vyetu ndani ya kikao hicho vilieleza kuwa viongozi waandamizi wa taasisi hizo walionyesha wazi kukerwa na mjadala wa Dowans wakati nchi ikiwa katika hali ngumu ya umeme na kuitaka kamati hiyo kutoa majibu ya uhakika na kuweka siasa pembeni.

"Viongozi wa CTI, Bi. Esta Mkwizu, Bw. Arnold Kilewo na wale wa TPSF walituhoji ni kwa nini tunakazania tu kuzungumzia mitambo ya Dowans badala ya kuitaka serikali kununua mitambo yake.

Lakini kubwa zaidi walitaka mitambo ya Dowans itaifishwe haraka ili itumike kuzalisha umeme wa dharura kama mali ya nchi, walishangaa kwa nini nchi inapoteza mabilioni ya fedha bila sababu," kilisema chanzo chetu ndani ya kikao hicho.

Kwa mujibu wa chanzo hicho viongozi hao wa wafanbiashara wakubwa ambao ndio watumiaji wakubwa wa umeme kwa asilimia 8,0 waliitaka kamati hiyo kueleza iwapo si kosa kwa nchi kuingia mkataba na Dowans wakati bunge iliazimia kuwa mkataba wa Richmond haukuwa halali.

Awali akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo yaliyojiri katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Januari Makamba alisema wadau hao walilalamikia ukosefu wa umeme na kwamba hali hiyo imelisababishia taifa hasara ya mabilioni ya fedha.

"Tatizo la umeme ni kubwa kiuchumi, kwa mfano Twiga Cement pekee licha ya kutumia jenereta bado wanapoteza karibu milioni 20 kwa siku.

Kama taifa tunapoteza karibu dola za Marekani 200,000 kwa siku kutokana na ukosefu wa umeme, hii ni hali mbaya sana, ndio maana tumelazimika kuzungumza kwanza na wadau kujua ukubwa wa tatizo kiuchumi," alisema Bw. Makamba.

Alisema katika kikao hicho ambacho kilikuwa bado haijafikia mwisho CTI waliweka wazi kuwa kati ya viwanda 280 vinavyomilikiwa na wanachama wake 50 wameshindwa kuendelea na uzalishaji na kusitisha kazi kwa muda kwa ukosefu wa umeme.

"Kama mnavyojua tunatakiwa kuanza vikao vyetu wiki mbili kabla ya bunge lakini tuliomba kibali maalumu kwa Spika kufanya vikao kutokana na ukubwa wa tatizo hili, leo (jana) tumekutana na wadau, kesho (leo) tutakutana na Wizara ya Nishati na Madini na kesho kutwa TANESCO.

"Pia Jumamosi tutaitisha public hearing (mdahalo wa wazi) pale Karimjee, tutaandaa vizuri ili tupate mawazo ya wadau kwa utaratibu mzuri," alisema Bw. Makamba.

Alisema Kamati hiyo itakutana na wadau wote wanaohusika na umeme wa gesi ili kutoa mapendekezo yatakayokidhi haja ya taifa kuondokana na adha ya sasa.

Alisema Kamati yake haijatoa mapendekezo yoyote kuhusu mitambo ya Dowans na kwamba kilichonukuliwa na vyombo vya habari yalikuwa maoni yake binafsi kabla ya kikao cha kamati hiyo.

"Kamati itatoa mapendezo yake kwa serikali Jumanne ijayo baada ya kumaliza kazi yake, kwa sasa tunaendelea na vikao ili kujua nini kinachotakiwa hasa kuokoa taifa letu na ukosefu wa umeme," alisema.

Alipoulizwa iwapo Kamati yake itamwita mtu aliyejitangaza kuwa mmiliki wa Dowans anayedaiwa kutua nchini juzi na kuzungumza na wahariri wa vyombo vya habari kwa sharti la kutopigwa picha alisema hawana sababu ya kufanya hivyo.

Hata hivyo alisema uamuzi wa serikali kutumia au kutotumia mtambo wa Dowans kuzalisha umeme wa dharura kwa sasa ni uamuzi tu na kwamba si jambo gumu na kufafanua kuwa kamati yake haiwezi kuishinikiza kufanya hivyo au kutofanya.

Alisema kabla ya kutoa mapendekezo yake kamati yake itafanya ziara kujionea hali halisi ya nishati hiyo katika vituo vyote vinavyozalisha umeme isipokuwa Mtera ambapo tayari wametembela.

No comments: