Tuesday, February 22, 2011

Yusufu Makamba adaiwa ‘kuua majirani zake kwa kiu’

Elizabeth Suleyman wa Gazeti la Mwananchi

KATIBU Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, anadaiwa na wakazi wa Wazo Hill, jijini Dar es Salaam kujiunganishia maji nyumbani kwake yaliyopaswa kusambazwa kwa wakazi wa eneo hilo.
Hata hivyo, Makamba amepuuza madai hayo akisema ana haki ya kuunganishiwa maji kama Mtanzania, ili mradi afuate taratibu na awe analipa ankara.Mwajuma Omari, mkazi wa eneo hilo, alisema wamekuwa wakitaabika kwa kukosa maji, kwa sababu bomba walilokuwa wakitegemea maeneo yao limeunganishwa kwa Makamba.

“Hivi sasa tunataabika na hatuji hatima yetu, ukiwaeleza Dawasco wanadai wataunganisha mabomba mengine na kuendelea kuchimba visima,” alisema Omari.Mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaka kutajwa, alisema toka enzi za Mzee Rashid Kawawa, wakazi wa eneo hilo walikuwa wanategema maji yanayotoka kwenye mabomba hayo.“

Tumekuwa tukijiuliza, iweje Dawasco waunganishe mabomba hayo kijanja kwa Makamba na kutufanya tukose maji kwa kulazimika kutumia ya kisima?” alihoji.

Akizungumzia suala hilo ofisini kwake jana, Ofisa Uhusiano wa Dawasco, Merry Lyimo, alipuuza malalamiko ya wakazi hao kuwa hayana msingi wowote na kwamba, mabomba waliyofunga kwa Makamba hayahusiani na wakazi hao.

Lyimo alisema walifunga bomba hilo kwa Makamba muda mrefu, hivyo malalamiko ya wananchi hao yakosa nguzo ya kusimamia. “Mbona wanamlalamikia yeye tu! Kwa sababu kama ni mabomba hayo tumeyafunga kwa watu wengi na kama hawana maji, Dawasco imejizatiti kuwawekea kisima ili wasikose kabisa,” alisema Lyimo na kuongeza:

“Hatujaona sababu za msingi za wao kulalamika... Makamba ni mteja wetu wa muda mrefu na tayari ameuganishiwa maji, hivyo wanapaswa kusubiri, mradi endelevu wa kuwaongezea visima vingine ili wasikose maji.”

Akizungumza kwa simu kuhusu malalamiko hayo, Makamba alisema yeye ni binadamu kama walivyo wengine, ana haki zote za kuunganishiwa maji.“Hao waliokueleza malalamiko hayo… siwezi kuyajibu ni vema ukaenda kwa walioniunganishia bomba la maji,” alisema Makamba na kuongeza:“Kigezo cha kuwa Katibu Mkuu wa CCM hakimaanishi sina haki ya kupewa maji, hivyo siwezi kuzungumzia hilo kawaulize Dawasco.”

Alisema aliomba kuunganishiwa maji tangu mwaka 1994, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na alifuata taratibu zote.

No comments: