Wednesday, March 9, 2011

Jerry Muro na wenzake wana kesi ya kujibu - mahakama

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema washitakiwa katika kesi ya kuomba rushwa ya Sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji nchini (TBC1) Jerry Muro na wenzake wana kesi ya kujibu.

Mwendesha mashitaka Wakili Mkuu wa Serikali Boniface Stanslaus, alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo anayesikiliza shauri hilo Gabriel Mirumbe kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa ambapo walikuwa na shahidi mmoja.

Baada ya Shahidi huyo Askari wa kikosi cha upelelezi katika ofisi ya Kamishna wa Upelelezi kanda maalum ya Dar es Salaam, Koplo Lugano kumaliza kutoa ushahidi wake, Wakili Stanslaus alidai upande wa mashitaka umefunga kesi hiyo.

Hakimu alisema anaahirisha shauri hilo kwa muda wa nusu saa ili aweze kupitia kesi hiyo na kutoa uamuzi kama washitakiwa wana kesi ya kujibu au la.

Baada ya nusu saa shauri hilo lilisikilizwa tena ambapo Hakimu Mirumbe alisema, “kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi saba na vielelezo vyote vilivyotolewa kama ushahidi katika kesi hii, Mahakama imeona washitakiwa wote wana kesi ya kujibu.”

Kutokana na uamuzi huo, Hakimu Mirumbe pia aliwauliza upande wa utetezi kama wana jambo la kuzungumza kufuatia uamuzi huo ambapo walidai hawana cha kuzungumza, ambapo aliahirisha shauri hilo hadi Machi 29, mwaka huu washitakiwa hao watakapoanza kujitetea.

Muro na wenzake Edmund Kapama na Deogratius Mgasa, wanadaiwa kuomba rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Wilaya ya Bagamoyo Michael Wage na kujifanya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Januari mwaka jana.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 5, mwaka 2010

No comments: