HOFU kubwa imetanda kwa wakazi wa Kijiji cha Masukanzi, wilayani Kilolo, mkoani Iringa baada ya kichwa cha mtu anayesadikika kuwa ni mtoto kuokotwa katika eneo hilo kikiwa kwenye mfuko wa rambo.
Kuokotwa kwa kichwa hicho cha mtoto kumekuja siku chache tangu kuzuka kwa hofu ya wananchi wa kijiji cha jirani baada ya watu wasiofahamika kuvamia maeneo hayo na kukimbiza wananchi kwa mapanga kwa nia ya kutaka kuwaua.
Wakizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini kwa sababu za kiusalama, wakazi wa Masukanzi walisema kuwa kichwa hicho kimeokotwa katika mazingira ya kutatanisha kikiwa ndani ya mfuko wa rambo na kuwa inaonesha wauaji walimtenganisha na kiwiliwili ambacho hakijulikani kilipo.
Walisema kuwa, mwezi mmoja uliopita kuna mtoto alipotea katika mazingira ya kutatanisha katika eneo hilo. Licha ya jitihada za muda wa zaidi ya wiki mbili kumtafuta, bado hakuweza kupatikana .
Kutokana na kichwa hicho kutotambuliwa, kimechukuliwa na maofisa wa polisi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na utambuzi hospitalini kwa kutumia mashine maalum ya DNA.
Wananchi hao walisema kuonekana kwa kichwa hicho kumewakumbusha ‘Rama mla watu’ ambaye alikamatwa na kichwa cha mtoto kikiwa katika mfuko wa rambo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili miaka kadhaa iliyopita na akatafuna kipande. Kesi yake inaendelea katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa hakuweza kupatikana kufafanua kuhusiana na tukio hilo na gazeti hili linaendelea na uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment