Wednesday, April 25, 2012

Adai alitaka kuchukuliwa msukule na askari huko Arusha

Na Joseph Ngilisho, Arusha
USHIRIKINA umeibuka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani Arusha, ambapo askari  wake wa kike aliye kwenye kitengo cha  usalama barabarani (Trafiki)  mwenye cheo cha koplo (Jina tunalihifadhi) ametuhumiwa kumchukua msichana ili amfanye msukule nyumbani kwake, Kijenge.
Shutuma hizo nzito, zimebainishwa na Johari Abdallah (20) (pichani), mkazi wa Kijenge jijini hapa ambaye alidai kunusurika kuchukuliwa msukule na askari huyo baada ya kufanikiwa kumwingiza nyumbani kwake kimiujiza na kuishi naye kwa muda wa siku tano bila msichana huyo kujijua.
Akisimulia jinsi alivyokumbwa na mkasa huo, Johari ambaye ni yatima na anaishi na mlezi wake akiwa na mtoto mchanga, alisema kuwa trafiki huyo amekuwa akishirikiana na mama mmoja ambaye ni rafiki yake na ndiye aliyemfuata na kumchukua kimiujiza.
“Mama huyo alinifuata  nyumbani na kuniomba nimsindikize mjini lakini tulipofika kwenye makutano ya barabara aliniambia nisimame na nifumbe macho, baada ya hapo akaniwekea kiganja chake usoni,” alidai  msichana huyo alipokuwa akiwasimulia viongozi wa serikali ya mtaa wa Kijenge huku akitokwa machozi.

Johari alidai kuwa baadaye alimwambia afumbue macho na atazame mbele yake, ambapo alimwona askari mmoja wa usalama barabarani wa kiume ambaye hakumtambua akiwa amesimama katikati ya barabara na akaamriwa amfuate.
“Huyo mama aliniambia nimfuate huyo askari ambaye alinipa shilingi 2000 na nilipoipokea, sikujielewa mpaka nikajikuta nipo kwenye nyumba moja ambapo niliambiwa nioge kwa kuwa nilikuwa mchafu na nikaingizwa ndani. Humo nilikuwa nasikia sauti za watoto wadogo lakini walikuwa hawaonekani.
“Askari huyo alikuja akanifunika kitambaa kichafu ndipo nilipoona miujiza ya ajabu,  wakiwemo watoto watano wenye umri wa miaka kati ya mmoja hadi mmoja na nusu wa jinsi tofauti. Baadaye nikamuona msichana (jina tunalo) ambaye alipotea akiwa na umri wa miaka 12, nilipewa jukumu la kulea watoto hao,” alidai Johari.
Akisimulia jinsi alivyoponyoka alidai alielekezwa kwenda kumchukua mtoto wa jirani yao na wake lakini alipofika kwao alianza kukabana na mfanyakazi wao aitwae Rozaria Natael ili amuue na amchukue mtoto.
Akizungumza ofisini hapo Natael alikiri kukabwa na msichana huyo lakini  walimkamata kwa nguvu na wengine kuanza kumwombea kabla ya kumfikisha katika ofisi ya serikali ya mtaa wa Kijenge.
Kwa upande wa askari huyo alipohojiwa kuhusiana na tuhuma hizo alikiri kumtambua Johari na kueleza kuwa  hakutaka kumfanya msukule na kwamba yeye anasingiziwa kwa sababu za watu binafsi.
Naye mama aliyedaiwa kushirikiana na askari huyo katika mambo ya kishirikina alikiri kumfahamu mtuhumiwa afande na kudai kuwa ni ndugu yake ila alikataa kuzungumzia masuala ya ushirikina.
Natael alisema kuwa Johari alitoweka nyumbani katika mazingira ya kutatanisha tangu Machi 26 na kupatikana Machi 30, mwaka huu baada ya kumtafuta kwa muda mrefu sanjari na kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Kijenge na Kituo Kikuu cha Kati bila mafanikio.

No comments: