Monday, July 23, 2012

Mwalimu wa Mwalimu Nyerere afariki dunia

Hayati Mwalimu James Irenge enzi za uhai wake. Picha hii ilipigwa Novemba, 2011 katika Shule ya Msingi Mwisenge wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda mkoani Mara.
Mwalimu James Irenge, ambaye ni mwalimu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, amefariki dunia usiku wa kuamkia jana.

Habari zilizopatikana jana zilisema Mwalimu Irenge, alifariki dunia nyumbani kwake Mwisenge, Musoma mkoani Mara.

Mzee Irenge aliyekuwa na umuri wa miaka zaidi ya 120, alimfundisha Mwalimu Nyerere katika Shule ya Mwisenge, kati ya mwaka 1934-1936.

Hadi mauti yanamfika, licha ya umri wake mkubwa, bado alikuwa na uwezo wa kusoma na kuandika mwenyewe bila kutumia miwani.

Wiki kadhaa zilizopita aliandika barua yake ya mwisho kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wiki iliyopita akimshuru kwa kumwezesha kumlipa fedha za dawa na chakula; mambo yaliyokuwa kilio chake cha siku nyingi.

Mwalimu Irenge mara kadhaa alikuwa akilalamika kwamba tangu alipostaafu ualimu miaka ya 1970 hakupata kulipwa mafao yake, na kiinua mgongo.

Kifo chake kinahitimisha uhai wa walimu wa Mwalimu Nyerere. Mwalimu mwingine, Daniel Kirigini, alifariki dunia mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Mazishi ya Mwalimu Irenge yanatarajiwa kufanyika Alhamisi wiki hii katika kijiji alichozaliwa cha Busegwe- Nyanza wilayani Butiama. Ameacha mjane, watoto 12, wajukuu 30 na vitukuu 15.

No comments: