Monday, August 6, 2012

MICHUANO YA BANC ABC SUPER 8 YAANZA KIMIZINGUO


Na Prince Akbar
MICHUANO ya BancABC Super 8 jana imeanza katika sura ya kutopendeza, mjini Arusha mechi kati ya Polisi Morogoro na Mtibwa Sugar ikishindwa kufanyika kwa sababu ya Menejimenti ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kudai kutokuwa na taarifa za mashindano hayo, wakati Dar es Salaam Simba ilichezesha timu B.
Simba B imetoka sare ya 1-1 na Jamhuri ya Pemba kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam. Jamhuri ndio waliotangulia kupata bao kupitia kwa Bakari Khamis dakika ya 48, akiunganisha krosi ya Abdallah Othman, kabla ya Shomary Kapombe, mchezaji pekee wa Simba A aliyecheza, kuisawazishia timu yake kwa penalti dakika ya 83, baada ya Miraj Adam kuangushwa kwenye eneo la hatari na Mfaume Shaaban.
Michuano hiyo  ina makundi mawili, ikishirikisha timu nane, Kundi A likiwa na timu za Simba, Jamhuri, Zimamoto na Mtende FC, wakati Kundi B kuna Super Falcon, Azam FC, Mtibwa Sugar na  Polisi Moro na bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Bank ABC ataondoka na Sh. milioni 40, mshindi wa pili Sh. milioni 20, wa tatu Sh. milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5 kila moja.
Michuano itachezwa katika vituo vinne vya Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na Mwanza, ambapo timu zitasafirishwa kwa ndege kwenda kucheza mechi katika vituo vyote. Kila timu itacheza mechi mechi katika vituo vituo vitatu tofauti. Simba baada ya mechi ya leo, itakwea pipa kwenda Arusha kucheza dhidi ya Mtende FC Alhamisi na itasafiri kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi yao ya mwisho ya Kundi A dhidi ya Zimamoto Jumamosi.
Wakati huo huo: Mchezo wa tatu wa michuuano hiyo kati ya wenyeji Super Falcon imefungwa nyumbani na Azam FC 2-0.
 Gorikipa wa Jamhuri ya Permba, Jaffari Said akiokoa moja ya hatari zilizoelekezwa langoni mwake wakati wa mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya Super 8 kwenye uwanja wa Chamazi jijini Dar.
 Mashabiki wa soka wakifuatilia mchezo huo.
 Hassan Khatib akimiliki mpira
 Beki wa Simba, Hassan Khatib  akijaribu kumzuia mshambuliaji wa Jamhuri ya Pemba, Mohamed Ally.
 Mshambuliaji wa timu ya Jamhuri ya Pemba, Mohamed Ally akimtoka beki wa Simba, Hassan Khatib wakati wa mchezo wa Super 8 uliofanyika kwenye Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Timu hizo zilifungana 1-1.  PICHA ZOTE NA HABARI MSETO BLOG

No comments: