MABINGWA WA NCHI 12 AFRIKA; Yanga na Kombe la Kagame baada ya kuifunga Azam 2-0 |
MABINGWA
wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC ya Dar es Salaam leo
wanatarajiwa kutambulisha Kombe la ubingwa wa michuano hiyo, maarufu
kama Kombe la Kagame katika ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, mini Dodoma.
Yanga,
waliotwaa Kombe hilo mara mbili mfululizo sasa, wachezaji wake
waliwasili usiku wa jana na baadhi ya viongozi, Wajumbe wa Kamati ya
Utendaji, Titus Osoro, Mohamed Bhinda na George Manyama pamoja na Katibu
Mkuu, Celestine Mwesigwa na Meneja, Hafidh Suleiman, wakati Mwenyekiti,
Yussuf Manji na Makamu wake, Clement Sanga na Wajumbe wengine
watawasili mapema leo.
Kwa
upande wa timu, wachezaji walifika pia jana na makocha wasaidizi,
Freddy Felix Minziro na Mfaume Athumani Samatta, wakati kocha Mkuu,
Mbelgiji Tom Saintfiet atakuja leo pamoja na viongozi wakuu.
Mbali
na Manji, Sanga na kocha, katika msafara unaokuja leo wanatarajiwa
kuwamo, Wajumbe wa Baraza la Wadhamini, Francis Mponjoli Kifukwe na Mama
Fatuma Karume.
Yanga
ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki iliyopita,
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo
yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider
Man’.
Hiyo
kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo,
baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao
1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa
siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga
ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena
Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na
Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua
tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC
Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa
marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua
tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa
penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga
ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru
kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti
mbili za Waganda.
No comments:
Post a Comment