Tuesday, November 13, 2012

MISS TANZANIA 2012 AIBU, VITUKO!

Musa Mateja na Shakoor Jongo
KAMA uliapa kwamba Miss Tanzania 2012 itakula za uso kutokana na kiingilio kikubwa kilichowekwa, imekula kwako kwani Watanzania hususan wana-Dar es Salaam, walijaa ukumbini, hivyo kutoa uthibitisho kwamba kwao laki (Tsh. 100,000) siyo pesa kabisa.

 
Miss Tanzania 2012-2013, Brigitte Alfred akiwa katika pozi baada ya kutwaa taji hilo.
Katika fainali hiyo, iliyochukua nafasi kwenye Ukumbi wa Cristal, uliopo kwenye Hotel ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar, pamoja na matukio ya aibu na vituko, ilishuhudiwa kwa mtoto mkali kutoka Kitongoji cha Sinza na baadaye Kanda ya Kinondoni, Brigitte Alfred, akibeba taji la Miss Tanzania 2012-2013.
Ushindi wa Brigitte, umerudisha heshima Kinondoni baada ya kuota mbawa kwa takriban miaka minne mfululizo, kwani aliyekuwa mrembo wa mwisho kushinda taji hilo akitokea kanda hiyo ni Richa Adhia mwaka 2007.
Kino ilitisha mno kati ya mwaka 2004 hadi 2007, kwani mara zote hizo ilishinda kupitia Faraja Kotta (2004), Nancy Sumary (2005), Wema Sepetu (2006) kabla ya Richa.
AIBU ZILIZOJIRI
Mrembo aliyeshinda taji (Brigitte), alitoka ukumbini chukuchuku, baada ya Mkurugenzi wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga ‘Anko’, kusahau ‘crown’ nyumbani kwake.

 
Miss Tanzania 2012-2013, Brigitte Alfred (katikati) akikabidhiwa ufunguo wa gari, kulia ni Mkurugenzi wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga ‘Anko’.
Ilibainishwa kuwa katika harakati za kuwahi ukumbini, Anko alisahau mfuko wenye taji (crown) chumbani kwake na alikumbuka muda mfupi kabla ya mshindi kutangazwa, kwa hiyo alikosa namna ya kukwepa aibu hiyo.
Anko, alimnong’oneza mwandishi wetu: “Dah nimesahau crown nyumbani, sijui itakuwaje?” wakati huo shindano lilikuwa limefika hatua ya nusu fainali (15 Bora).
Brigitte amekuwa mrembo wa kwanza kutangazwa mshindi bila kuvalishwa taji.
Ukumbi wa Cristal ni mdogo, hivyo ulishindwa kutosheleza idadi ya watu, matokeo yake ulijaa mno, hivyo kusababisha joto lililosababisha kero kwa wahudhuriaji.
Miss Tanzania 2012 ilikuwa ni shoo ya VIP lakini mambo yalikwenda ndivyo sivyo, kwani pamoja na watu kulipa Tsh. 100,000 kwa kichwa, wengi walisimama, kwa hiyo hawakufaidi laki zao.
Miss Tanzania 2011-2012, Salha Israel, alipopanda kukabidhi taji, alikuwa amepooza, utadhani alilazimishwa.
VITUKO VILIKUWEPO
Kwa mwendo wa kiingilio hicho, ilidhaniwa kila anayeingia ukumbini angekuwa na usafiri wake binafsi au wa kukodi lakini haikuwa hivyo, baada ya shoo kumalizika, watu kibao walijisogeza kwenye kituo cha daladala kwa ajili ya ‘kujisevia’ usafiri wa shilingi 300.
Miss Tanzania namba mbili mwaka 2006, Jokate Mwegelo ‘Kidoti’, akiwa MC wa shughuli, alishindwa kuficha hisia zake kwa mwanamuziki, Nasibu Abdul ‘Diamond’, pale alipomtambulisha kama ‘Sukari ya Warembo’.
Siyo habari mpya kwamba Diamond alishawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Jokate, kwa hiyo kitendo cha kumtambulisha hivyo kiliibua minong’ono kuwa Kidoti anamkubali ‘janki’ huyo kuwa ana ladha tamu kama sukari.
Mwanamitindo wa kiume (jina tunalo), alitolewa nishai backstage na mrembo mmoja (jina tunalihifadhi), alipokwenda kumuomba namba ya simu. Baadaye ilibainika kuwa mwanamitindo huyo alitumwa na pedeshee fulani kuchukua namba ili aanze mikakati ya kung’oa.
MENGINEYO
MOSI: Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’, alizua minong’ono, baada ya kuandika kwenye akaunti yake ya Twitter kuwa hatakwenda kwenye shoo ya fainali kwa sababu mshindi anamjua na ni mshiriki namba 26.
Matokeo ya mwisho yalipotangazwa ukumbini, FA alipatia kwa asilimia 100, kwani mrembo namba 26 ndiye Brigitte.
PILI: Warembo walioshiriki Miss Tanzania mwaka jana na miaka iliyopita, walikuwa wakizungumza huku wakisindikiza mazungumzo yao kwa vicheko kwamba huu ni muda wao kupumzika, kwani mapedeshee watawapa kisogo na kuwafuata warembo wapya, wao wakiita ‘mali mpya’.
TATU: Miss Kinondoni, ilificha nafasi zote mbili za juu, baada ya Miss Sinza, Eugine Fabian kuibuka namba mbili, wakati Miss Temeke, Eda Sylvester akiambulia namba tatu. Warembo Magdalena Loi na Happines Daniel, walikamilisha Tano Bora.
NNE: Diamond pamoja na kuingia kwa mbwembwe, alipwaya jukwaani kiasi cha kusababisha shoo yake izorote kinyume na matarajio ya wengi.

No comments: