Tuesday, November 20, 2012

Na Eliasa Ally, Iringa
MAPADRI waliovamiwa usiku  wa kuamkia Jumamosi iliyopita na majambazi  sita waliokuwa na silaha  katika Parokia ya Isimani, jimbo la Isimani Halmashauri ya Iringa Vijijini kwa nyakati tofauti wamefunguka kuwa ni Mungu tu aliyewaokoa.
Paroko Angelo Burgio akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa.
Baada ya kuvamiwa, Paroko Angelo Burgio (60) alipigwa risasi kwenye ubavu wa kushoto, Padri  msaidizi,  Herman Myala (36)  alicharangwa panga kichwani ambapo majambazi hao walifanikiwa  kupora fedha za kanisa hilo shilingi milioni 3.5 na dola za Kimarekani 100 na kutoweka.
Katika mahojiano na gazeti hili, Padri Angelo ambaye  amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa wodi namba 4 alisema: “Majambazi hao walivunja mlango wa geti la kuingilia mapadri baada ya umeme wa jenereta kuzimwa na kuingia ndani.
Mwandishi: Je, walianza kukuvamia wewe au msaidizi wako?
Paroko: Walianza kumkata kwa panga Padri Myala huku wakimtaka awaoneshe chumba ambacho nilikuwa nimelala, baada ya kuona anaendelea kuumizwa  aliwaonesha chumba changu.
Mwandishi: Wakati mwenzako anashambuliwa wewe ulichukuwa uamuzi gani?
Paroko:  Niliposikia kelele nilitaka kukimbia ndipo walinipiga risasi ubavuni nikaanguka.
Mwandishi: Baada ya hapo kiliendelea nini?
Padri  msaidizi, Herman Myala akiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa baada ya kujeruhiwa.
Paroko: Majambazi hao walijua nimekufa, walikwenda kuchukua fedha na kuondoka baada ya kuwaona wananchi wanakuja kufuatia kusikia mlio wa bunduki na mayowe yetu ya kuomba msaada.
Mwandishi: Je, ukiwaona leo unaweza kuwatambua?
Paroko: Hapana, majambazi hao walivaa mavazi ya kufunika uso na mmoja wao alikuwa na bunduki na wengine walikuwa na mapanga.Tukio hili ni baya kupindukia, lengo lao lilikuwa ni kutuua.
Diwani wa Kata ya Kihologota Tarafa ya Isimani, Costantino Kihwele alisema kuwa Padri Angelo amekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wa Isimani ambapo kwa sasa anafadhili mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 4 pia anawalipia ada baadhi ya watoto yatima wanaosoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, Wiliam Lukuvi (katikati) akimjulia hali Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Isimani mkoani Iringa, Angelo Burgio wakati alipomtembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alipohojiwa alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema watuhumiwa wanne kati ya sita wamekamatwa.
Aliwataja watu hao kuwa ni Joseph Ngwale (30), Erasto Ngwale (38), Gaitan Kitwange na Anitha Mwinuka.
Aliongeza kuwa, wahalifu hao wanahusishwa na tukio lingine la kuvamia  Kanisa la Katoliki Kihesa na kupora shilingi 500,000.

No comments: