Mjumbe
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Profesa
Ruth Meena akijibu maswali ya wahariri mbalimbali katika mkutano wa TGNP
na wahariri hao uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, pembeni yake ni
Kaimu Mkurugenzi wa TGNP, Mary Nsemwa.
Mmoja
wa wahariri kutoka vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Jane Mihanji na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za
Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) akichangia mada katika mkutano wa
TGNP na wahariri wa habari.
Mhariri
kutoka Global Publishers, Walusanga Ndaki (wa kwanza kulia) akiwa na
baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia mada
zilizokuwa zikitolewa katika mkutano huo.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TGNP, Profesa Ruth Meena (kulia) pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa TGNP, Mary Nsemwa.
Mmoja
wa maofisa wa TGNP kutoka Idara ya Habari na Mawasiliano, Deo Temba
(kushoto) akichukua kumbukumbu katika mkutano huo na wahariri. Pembeni
yake ni Prof. Ruth Meena.
Na Mwandishi wa Thehabari.com
KAIMU Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Mary Nsemwa
amevipongeza vyombo mbalimbali vya habari nchini kwa kile sasa kutoa
nafasi ya kuridhisha kwa kuandika masuala mbalimbali ya kijinsia ambayo
hapo awali yalikuwa hayapewi nafasi ya kutosha.
Bi. Nsemwa ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa
akizungumza na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari katika mkutano
wao na TGNP, kuzungumzia changamoto anuai za kijinsia na vyombo vya
habari pamoja na ushiriki wa wanawake katika mchakato wa maoni ya
uundwaji wa katiba mpya.
Alisema ushirikiano mzuri uliojengeka kati ya taasisi hiyo na vyombo
vya habari umesaidia kwa kiasi kikubwa hivyo masuala ya kijinsia na hasa
yale yanaowakandamiza wanawake kusikika katika vyombo vya habari hali
ambayo imesaidia kwa kiasi fulani.
“…Tumejifunza mengi kutoka katika vyombo vya habari, vyombo hivi sasa
vimewaunganisha wanawake…sauti za wasiosikisa hasa wa vijijini sasa
zinasikika kupitia vyombo hivi. Vyombo vya habari pia vimepaza sauti kwa
kampeni yetu ya Haki ya Uchumi; ‘Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake
walioko Pembezoni’ na mkumbuke kwamba nyinyi mnanguvu zaidi yetu,”
alisema Bi. Nsemwa.
Naye mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP), Profesa Ruth Meena akiwasilisha mada katika mkutano huo
wa wahariri alisema mambo mengi ya msingi ambayo ni miongoni mwa madai
ya wananchi yameainishwa katika Katiba iliyopo sasa, hivyo kushauri ipo
haja ya kuangalia namna ya usimamizi wa sheria na mabadiliko kadhaa
kuingizwa kwenye Katiba Mpya.
“...Kwa upande mmoja Katiba Ya Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania ya
Mwaka 1977, inatoa haki sawa kwa wanawake na wanaume katika nyanja za
siasa, uchumi na ustawi wa jamii, na hapohapo kuzipokonya kwa mkono
mwingine kwa kuruhusu kuendelezwa kwa sheria, taratibu na tabia
zinazokinzana na katiba,” alisema Prof. Meena.
Aidha alishauri Katiba mpya ibatilishe sheria zote zinazokinzana na
haki za msingi za wanawake na watoto wa kike hususani kubatilisha sheria
na mila zote za ubaguzi wa jinsia, ubaguzi dhidi ya watoto hususani
watoto wa kike, katika maswala ya ndoa, mirathi, haki za kumiliki.
“Kwa mantiki hii, katiba ibainishe kwa uwazi haki za wanawake na haki
za watoto. Pamoja na kuwajibisha serikali kuchukua hatua zote za kisera
na sheria ili kulinda na kuhifadhi haki za wanawake na za watoto katika
maeneo hayo, na pia iwajibishe serikali kutekeleza mikataba yote
iliyoridhia kuhusu haki za wanawake ( CEDAW, CRC, ILO Conventon)
Mikataba hii itambulike kuwa ni sheria za nchi ili kuepusha
ucheleweshaji wa kutafsri au kuruhusu uchakachuaji wamikataba hii katika
sheria za nchi,” alifafanua Prof. Meena.
Pamoja na hayo alishauri Katiba mpya iangalie haki ya ufikiaji wa
huduma za jamii; haki ya kufikia na kufaidi huduma za msingi kama vile
maji, chakula, malazi na elimu na hifadhi ya jamii ziendelee kuwepo -
pamoja na kusisitiza wajibu wa serikali wa kuhakikisha huduma hizi za
msingi zifikiwe na ke na me ( rika zote, na hali zote).
No comments:
Post a Comment