Tuesday, December 11, 2012

Na Mwandishi Wetu
MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako ametamba kwamba yeye ni tajiri tishio kuliko watumishi wenzake kwani anamiliki magari sita ya kifahari na nyumba ambayo ina kiyoyozi (AC).
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo 'Mzee wa Upako'.
Akihubiria waumini wake kanisani hapo juzikati, Ubungo- Kibangu, jijini Dar es Salaam na kuoneshwa na Kituo cha Runinga cha C2C na Channel Ten hivi karibuni, Mzee wa Upako alisema magari yake hayo ya kifahari yote yana viyoyozi na si ya kutoka Japan, akimaanisha ya gharama kubwa zaidi.
“Mimi ndiye Mzee wa Upako, nikitoka nje nakuta magari yote sita yapo, nachagua leo niendeshe hili au lile. Najiambia hapana hili nililiendesha jana, nachukua lingine,” alitamba kiongozi huyo.
Mercedes Benz.
Aliyataja magari hayo kuwa ni Mercedes Benz, Land Rover Discovery, Range Rover Sport, BMW X5, Ford Escape na Range Rover Vogue ambayo Uwazi linatafiti bei zake na kuwapelekea wasomaji siku zijazo.
Aidha, mtumishi huyo wa Mungu aliendelea kutamba kuwa nyumbani mwake mna viyoyozi ‘vikali vya kufa mtu’ na kubainisha kwamba huwa akitoka kwenye gari lenye kiyoyozi anaingia katika nyumba yenye kiyoyozi.
“Mimi nasema hayo kwa sababu ni mlipaji mzuri wa kodi za serikali, sioni sababu ya kuficha mali zangu, kwa nini nifiche?” alihoji na kuongeza:
 
Land Rover Discovery.
“Magari yote nimeandika kwa jina langu ili niyalipie kodi, situmii mwamvuli wa kanisa kwa kukwepa kodi.”
Aliwaambia waumini wake kuwa kazi yake ni kugawa upako wa baraka za utajiri na kwamba kupitia kanisa lake watu wengi wameneemeka kimaisha.
“Nasisitiza kuwa kila mtu anatakiwa kuwa tajiri lakini utajiri wa halali siyo ule wa kudhulumu, ndiyo maana nasimama hapa kutaja mali zangu, magari hayo si mali ya kanisa ni yangu,” alisema.
 
BMW X5.
Pia aliyachambua makanisa kwa kusema: “Makanisa yetu haya ya kiroho ni hovyo, wameingia matapeli na ninayasema haya kwa kuwa ninayajua, nipo ndani, ndiyo maana najua kitu ninachokisema na mtu akitaka tubishane kwa hoja hii hawezi kunishinda.
“Najua hili ninalozungumza ni jambo zito na sasa ninaposema haya maneno ni sauti ya Mungu mwenyewe inatoka kupitia kinywa changu.”
Mzee wa Upako aliwahi kusema kwamba amekuwa akitumia zaidi ya shilingi 300,000,000 kwa mwaka kwa ajili ya kuendesha vipindi vyake katika runinga na fedha hizo huchangisha kupitia akaunti zake, akasisitiza vipindi vya runingani ni mali yake na si kanisa.
 
Ford Escape.
Wachambuzi wa mambo wameichambua hesabu hiyo na kugundua kwamba mchunga kondoo huyo hutumia zaidi ya shilingi 25,000,000 kwa mwezi kulipia vipindi hivyo.
Kiongozi huyo ana kanisa kubwa la ghorofa Ubungo Kibangu na mabasi makubwa  kadhaa ambayo hutumika kuwasomba waumini bure kutoka Barabara ya Mandela hadi kanisani kwake.
Hivi karibuni Mzee wa Upako amewahi kuwakemea wachungaji wenzake wa makanisa ya kiroho kwa kujitajirisha kwa kujiita manabii na mitume akidai kwamba kufanya hivyo ni kuwatapeli waumini.
Range Rover Vogue.
“Inawezekana vipi mabomu yapigwe madhabahuni halafu wewe kama mtume na nabii usifanye jambo lolote la Kimungu dhidi ya waliofanya kitendo kile madhabahuni?” alihoji Mchungaji Lusekelo.
Alidai kuwa kuna mitume hapa nchini kazi yao ni kugombania ardhi. “Kama kweli wewe ni mtume na nabii halafu unagombania ardhi ya mashamba na Wazaramo, huo ndiyo utume tulioitiwa? Ndiyo maana hata serikali haitutambui,” alisema Mzee wa Upako huku akishangiliwa na waumini wake.

No comments: